Watahiniwa darasa la saba zaidi ya 700,000 kuanza mitihani leo - LEKULE

Breaking

9 Sept 2015

Watahiniwa darasa la saba zaidi ya 700,000 kuanza mitihani leo


Dar es Salaam.
Wanafunzi 775,729 walioandikishwa kufanya mtihani wa darasa la saba nchini, kesho wanaanza kufanya mtihani huo, huku idadi ya watahiniwa ikipungua ukilinganisha na walioandikishwa mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Charles Msonde amesema masomo yatakayotahiniwa kesho na kesho kutwa ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
Dk Msonde amesema watahiniwa 748,514 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 27,215 watafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia kujifunzia.
“Watahiniwa wasioona walioandikishwa kufanya mitihani ni 76 na watahiniwa wenye uoni hafifu ambao wanahitaji maandishi makubwa ni 698, kati yao wavulana ni 330 na wasichana ni 368,” alisema Dk Msonde.
Amesema maandalizi ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa fomu maalumu za kujibia mtihani (OMR) na nyaraka nyingine zinazohusu mtihani huo. Alisisitiza kuwa mtihani huo unalenga kupima uelewa wa wanafunzi kwa yale waliyojifunza katika kipindi cha miaka saba.
Katibu huyo wa Necta alizitaka Kamati za Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa taratibu zote za mitihani zinazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu.
“Mtihani huu ni muhimu kwa Taifa kwa sababu hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari. Ni matarajio yetu kwamba wanafunzi wataufanya mtihani huo kwa kuzingatia taratibu zote za mtihani ili matokeo yaonyeshe uwezo wao,” alisema.

No comments: