KAIMU
Mufti wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shekhe Abubakar Zuberi
Ally ni miongoni wa mashehe wanne waliojitokeza kuwania kuchaguliwa
kwenye nafasi ya Mufti kwenye uchaguzi utakaofanyika kesho jijini hapa.
Akizungumza
jana, Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajab aliwataja mashekhe wengine
waliochukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo kuwa ni Ally Muhidin
Mkoyogole, Khamis Abbas Mtupa na Hassan Ibrahim Kiburwa.
Alisema
maandalizi ya mkutano mkuu kwa ajili ya uchaguzi huo, yamekamilika na
kwamba wajumbe zaidi ya 550 kutoka mikoa mbalimbali, wameanza kuingia.
Katika mkutano huo wa uchaguzi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Chiku Gallawa
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Alisema
wajumbe wa mkutano huo wa kumchagua Mufti wa kuiongoza Bakwata ni wengi,
ambapo utawashirikisha mashekhe wote wa mkoa, wilaya, mwenyeviti na
makatibu wa mkoa na wilaya na Baraza la Maulamaa, pia viongozi wa
serikali wataalikwa.
Alisema
Mufti atakayechaguliwa atakuwa wa awamu ya tatu, ambapo walitanguliwa na
Mufti Hemed Bin Jumaa bin Hemed na Mufti Issa Bin Simba aliyefariki
dunia Juni 22, mwaka huu katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment