Wanajeshi wamelakiwa kwa shangwe na waandamanaji ambao wamekuwa wakipinga mapinduzi
Viongozi wa mapinduzi Burkina Faso wamekataa kutii makataa ya kusalimu amri na kutishia kupigana vita wakishambuliwa.
Walinzi
wa rais walioongoza mapinduzi walikuwa wamepewa hadi saa nne saa za huko
kuweka chini silaha na wanajeshi ambao walifika katika mji mkuu
Ouagadougou usiku.
Hayo
yamejiri huku marais wa mataifa ya Afrika Magharibi chini ya muungano wa
Ecowas wakikusanyika Abuja, Nigeria kufahamishwa na Rais wa Senegal
Macky Sall kuhusu hatua zilizopigwa katika kutatua mzozo huo.
Duru
zinasema mashaurino ya kupatanisha wanajeshi hao na walinzi waliopindua
serikali yaligonga mwamba usiku, suala tata likiwa hatima ya walinzi hao
wa rais.
Rais Sall amekuwa akiongoza mashauriano akishirikiana na mwenzake wa Benin Yayi Boni.
Barabara za kuelekea ikulu ya rais hazina watu wala magari huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda Ouagadougou.
Kiongozi
wa mapinduzi Jenerali Gilbert Diendere alikuwa awali ameambia BBC kwamba
yuko tayari kurejesha mamlaka kwa uongozi wa kiraia, lakini baada tu ya
mpango wake wa kumaliza mzozo wa sasa kuungwa mkono na viongozi wa
mataifa ya eneo hilo.
Akiongea
kutoka mafichoni, Jenerali Diendere aliambia BBC: “Kuwa tayari kusalimu
amri? Hatujafika huko bado ...Tungependa kuendelea na mazungumzo na
tunawaambia wote kwamba tuko tayari kutekeleza maamuzi ya Ecowas (kundi
la mataifa ya Afrika Magharibi).”
Aidha, aliomba radhi kwa raia, akisema hilo tu ndilo wawezalo kufanya kwa sasa.
Walinzi wa rais waliopindua serikali ni watiifu kwa kiongozi aliyetimuliwa mamlakani mwaka jana Blaise Compaore.
Walimzuilia Kaimu Rais Michel Kafando Jumatano iliyopita, na kumtangaza Jenerali Diendere kuwa kiongozi mpya.
Tangu
wakati huo, watu 10 wameuawa kwenye makabiliano kati ya waandamanaji
wanaopinga mapinduzi hayo na maafisa wa usalama. Watu zaidi ya 100
wamejeruhiwa.
Balozi wa
Ufaransa nchini Burkina Faso, Gilles Thibault, aliandika kwenye Twitter
kwamba Bw Kafando ameachiliwa huru na sasa yumo kwenye makao ya balozi
huyo.