Siku moja baada ya taasisi ya Twaweza kutoa ripoti ya maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi wa Oktoba 25, maswali yameibuka kwenye mijadala mbalimbali miongoni mwa wananchi, yakihoji jinsi maoni hayo yalivyokusanywa, wafadhili wa utafiti na namna maamuzi kadhaa yalivyofikiwa.
Kadhalika
maswali mengine yaliyozua utata kuhusu utafiti huo ni sababu za maoni
hayo kuanza kukusanywa siku mbili kabla ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) kupitisha wagombea urais, na iwapo uamuzi huo haungeweza kuathiri
matokeo. Baadhi ya maswali hayo yamejibiwa na Twaweza.
Hata
hivyo, baadhi ya maswali yamejibiwa na Twaweza ikisema maswali hayo
hayashangazi kwa kuwa hii si mara ya kwanza kwake kufanya utafiti kwa
kukusanya maoni.
Kuhusu
aliyefadhili utafiti huo, Mshauri Mkuu na Meneja wa Mawasiliano wa
Twaweza, Risha Chande alisema kwa kawaida taasisi hiyo inatumia fedha
zake kufanya utafiti.
Kwa
mujibu wa matokeo ya utafiti huo mpya yaliyotangazwa juzi, asilimia 65
ya wananchi wa Tanzania Bara wangempigia kura mgombea urais wa CCM, Dk
John Magufuli iwapo uchaguzi ungefanyika kati ya Agosti 19 na Septemba
7.
NEC
ilipitisha majina ya wagombea nane wa urais Agosti 21 na kampeni
kuruhusiwa kuanza Agosti 22, lakini utafiti huo umetaja majina ya
wagombea wawili, licha ya kipindi cha utafiti kudumu kwa takriban mwezi
mmoja baada ya kampeni kuanza.
Utafiti
huo unaonyesha kuwa asilimia 25 wangempigia kura mgombea wa Chadema,
Edward Lowassa, iwapo uchaguzi ungefanyika kipindi hicho.
Katika
utafiti wa taasisi hiyo wa mwezi Novemba mwaka jana, Lowassa akiwa
ndani ya CCM alikuwa akiongoza kwa mbali wakati Dk Magufuli hakuwamo
kwenye tano bora.
Huu ni utafiti wa kwanza mkubwa wa kisiasa uliofanywa tangu kipenga cha kampeni kilipopulizwa Agosti 23, mwaka huu.
Katika
maelezo ya methodolojia ya utafiti, Twaweza imeeleza kuwa ilikusanya
maoni hayo bila kuwauliza wahojiwa jina la mgombea na kwamba watu
waliohojiwa ndio waliotaja jina la mgombea ambaye walimtaka, lakini
ripoti ya utafiti huo haikutaja baadhi ya majina yaliyojitokeza zaidi ya
Dk Magufuli na Lowassa.
Kadhalika,
Twaweza ilisema haikutaka kukusanya maoni kwa kuangalia wingi wa watu
katika mikutano ya kisiasa au vichwa vya habari vya magazeti bali
waliona kura ya maoni ya wananchi ndiyo inayoweza kueleza ukweli
kisayansi.
Kwa
mujibu wa Twaweza, utafiti huo ulitumia mawasiliano ya simu kukusanya
maoni, ikieleza kuwa huo ni utafiti wa kwanza barani Afrika wenye
uwakilishi wa kitaifa uliotumia simu za mkononi walizogawiwa wahojiwa.
“Ili
kuhakikisha kwamba uchaguzi nasibu unawakilisha vilivyo Tanzania Bara,
simu za mkononi na chaja zinazotumia mwanga wa jua ziligawiwa kwa kaya
zilizoshiriki. Kaya zisizowakilishwa ni zile tu zilizopo katika maeneo
ambayo hayafikiwi na mitandao ya simu,” ilisema ripoti ya Twaweza.
Maswali 14 yaliyoibuliwa na tafiti ya Twaweza
1.
Kwa mara ya kwanza Twaweza walisoma ripoti ya utafiti na kuonyeshwa
moja kwa moja na TV. Nani alidhamini utafiti, matangazo hayo na kwa
madhumuni gani?
2. Kwa nini waliamua kutoa matokeo ya utafiti wao katikati ya kampeni zenye ushindani mkali na mhemko mkubwa wa kisiasa?
3. Je, ni jinsi gani watu waliohojiwa walichaguliwa?
4. Je, watu waliohojiwa ni wa kutoka maeneo gani, makundi gani ya watu, ukiacha jinsia?
5. Je, waliohojiwa wamejiandikisha kupiga kura, mashabiki tu au mchanganyiko?
6.
Twaweza wanajua kwamba kampeni za wagombea urais huanza baada ya Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuidhinisha wagombea waliopendekezwa na
vyama. Kwa nini shirika hilo lilianza kufanya utafiti siku mbili kabla
ya hapo?
7.
Twaweza wanasema wahojiwa hawakupatiwa orodha ya majibu ya kuchagua.
Je, ni kweli hawakuwa wanawajua wagombea wengine waliotajwa zaidi ya Dk
John Magufuli na Edward Lowassa wakabaki kusema “mwingine?”
8.
Katika nafasi ya ubunge na udiwani, wahojiwa wameonyesha kuwajua na
kuwapigia kura wagombea wa ACT-Wazalendo. Inakuwaje watu hao hao
washindwe kumtaja mgombea urais wa chama hicho badala yake Twaweza
ikamweka katika kundi la “mwingine?”
9.
Takwimu zote asilimia huwa ni 100 iliwezekanaje mgawanyo wa takwimu
katika ripoti ya Twaweza katika baadhi ya maeneo asilimia zilizidi na au
kupungua 100?
10.
Tafiti zilizopita za Twaweza zilikuwa zinajumuisha watu wengi na
zilikuwa zinaonyesha mtu aliyeshika nafasi ya kwanza pengine hadi 10.
Kwa nini katika utafiti huu waliwalenga wawili tu Lowassa na Magufuli?
11.
Ripoti inasema kwamba dodoso la utafiti huu liliandaliwa kabla ya
uteuzi wa wagombea urais wa vyama vingine (nje ya mseto wa Ukawa),
kikiwamo ACT-Wazalendo. Je, dodoso hilo lilikuwa na maelekezo gani kiasi
kwamba ikawa vigumu kuwaingiza wagombea wengine?
12. Kwanini matokeo ya utafiti na kinachoonekana nje ni picha mbili tofauti?
13.
Matokeo ya awali ya Twaweza yalionyesha Lowassa alipokuwa CCM aliongoza
kwa ushawishi, iweje ndani ya wiki mbili baada ya kuhamia upande wa
pili aporomoke hivyo?
14. Kwanini Twaweza hawakushirikisha Zanzibar katika utafiti wakati urais ni wa Muungano?