Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameendelea kujinadi katika kampeni zake, huku akitumia kauli mbiu ya Movement for Change (M4C) inayotumiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenye mikutano yake.
Chadema
hivi karibuni waliilalamikia hatua hiyo ya Dk. Magufuli na kumtaka
aache kutumia kauli mbiu hiyo ambayo ina maana ya ‘vuguvugu la
mabadiliko’, huku wakitishia kumpandisha kizimbani kwa kile walichoeleza
ni alama yao waliyoisajili.
Akizungumza
kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa mpira wa Kyerwa
Mjini, mkoani Kagera juzi, mgombea huyo wa CCM aliuambia uliojitokeza
kumsikiliza kuwa kama wanataka mabadiliko wamchague yeye kwasababu yeye
ndiye mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli na kuibadilisha kauli
mbiu hiyo kwa kuweka jina lake: Magufuli for Change (M4C).
“Mimi ni Magufuli for Change, haya imbeni Magufuli for Change,” aliwaambia wananchi hao ambao nao walianza kuimba wakimfuatisha.
Katika
mkutano huo, Dk. Magufuli pia alimrushia kijembe Waziri Mkuu Mstaafu,
Fredrick Sumaye, ambaye amekuwa akizunguka na mgombea urais
aliyesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chadema,
Edward Lowassa na kuinanga serikali kuwa haijafanya lolote kwa miaka
yote tangu uhuru.
Ingawa
hakumtaja kwa jina, Dk. Magufuli alisema kuna mtu alikuwa na madaraka
makubwa serikalini ambaye alidumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka 10 lakini
amekuwa akiilalamikia serikali aliyokuwa akiitumikia.
Sumaye
alikuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa
ikiongozwa na Rais Benjamin Mkapa kwa kipindi cha miaka 10 mfulizo.
“Mtu
alikuwa msaidizi wa karibu wa Rais na amekaa kwenye nafasi hiyo kwa
miaka 10 mfululizo anasema hatujafanya kitu, ina maana yeye ndiye
aliyetukwamisha akiwa madarakani,” alisema.