MPASUKO
ndani ya vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, umeanza kushika kasi
baada ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kunyimwa eneo la kukaa kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni
za chama cha NCCR-Mageuzi Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro.
Uzinduzi
huo ulifanywa juzi na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, ambaye pia ni
mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia katika viwanja vya Chuo
cha Ualimu Marangu (TTC), ambapo madiwani wa Chadema hawakutengewa eneo
la kuketi wala kunadiwa, jambo walilodai ni kudhalilishwa.
Kutokana
na mpasuko huo, Mbatia bila kumtaja mgombea na chama, alisema hawezi
kumnadi mgombea anayechana mabango yake kamwe, huku madiwani hao wa
Chadema wakiahidi kuendelea na kampeni zao na wana uhakika wa kushinda
kwa sababu wanakubalika.
Wakizungumza
na gazeti hili kwenye mkutano huo kwa masharti ya kutoandikwa majina
yao, madiwani hao wa Chadema, walisema licha ya vyama vinavyounda Ukawa
kuweka makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja kwenye kila jimbo na
kata, NCCR wameshindwa kutekeleza agizo hilo kwa kusimamisha wagombea wa
udiwani kata zote huku Chadema nao wakifanya hivyo.
Mmoja wa
madiwani hao kupitia Viti Maalumu, alisema ni vigumu kukubaliana na hali
kutokana na wao kutumia gharama nyingi, na kubainisha kuwa katika jimbo
hilo Chadema ndicho chenye kukubalika zaidi, hivyo ingekuwa vyema
wangeachiwa nafasi za udiwani kutokana na wao kuwaachia kiti cha ubunge.
Alisema
licha ya kunyimwa kuketi kwenye mkutano huo na kushindwa kutambulishwa,
wataendelea na msimamo wao hata kama wakipelekwa kwenye kamati ya
maridhiano kama ilivyokuwa awali, hakitabadilika chochote.
“Tumetumia
gharama nyingi sana kutangaza chama chetu cha Chadema, na tumeanza kuwa
na mizizi muda mrefu, lakini Mbatia kaja juzi tu tena kwa sababu ya
Ukawa, isitoshe mgombea urais anayefanya Ukawa uuzike yupo kwenye chama
chetu, hivyo ukiona watu wanaukubali Ukawa ujue ni Chadema,” alidai
mgombea huyo.
Alisema
endapo wagombea udiwani kupitia NCCR- Mageuzi, hawataondolewa na wao
hawatakubali kujiengua na kuwaachia nafasi hizo, watahakikisha wanapiga
kampeni zao wenyewe kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo, kutokana
na kudai wao ndio wanaokubalika.
Akizungumza
wakati akihutubia wananchi, Mbatia ambaye pia ni Makamu Mwenza wa
Ukawa, James Mbatia alisema madiwani walipewa maelekezo na makao makuu
ya vyama vyao kwa maandishi, yakieleza kuangalia vigezo vya nani
anayekubalika, mtandao wa mtu, uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulivyokuwa
mwaka jana, na sio kila mtu kulalamikia kuwa yeye ndiye anayefaa.
Mbatia
alitumia mkutano huo, kuwataka wabunge wote nchini kupitia Ukawa,
kuheshimu makubaliano ya kile walichosaini kwa kutekeleza, na sio kila
mgombea wa kila chama kung’ang’ania yeye wakati makubaliano yapo.
Alisema
anashangazwa kuletewa malalamiko ya madiwani wakati tayari
alikwishaongea na Katibu wa Chadema na kumweleza watumie busara kwa
kuamua matatizo hayo, ambapo alibainisha hadi sasa wameshindwa
kusuluhisha mgongano huo ina maana pia wameshindwa uongozi.
Kutokana
na mpasuko huo, Mbatia bila kumtaja mgombea na chama, alisema hawezi
kumnadi mgombea anayechana mabango yake kamwe. Aliwataka wananchi
kuwapima madiwani wanaotaka kuchaguliwa ni vyema wakaangalia sifa za
uwezo, kiongozi mkweli kwa maneno na matendo, kiongozi anayechukia
uonevu na vitendo vya dhuluma katika jamii.
“Makubaliano
tulishasaini na wagombea wote wanayajua kupitia vyama vyao, sasa kila
mmoja anasema yeye ndiye anayekubalika....tuheshimu makubaliano
yaliyowekwa na Ukawa, lakini mimi bila ushabiki sitamnadi mgombea
anayechana mabango yangu...hata kidogo,” alisema Mbatia.
Wakati
madiwani wa Chadema wakitengwa kwenye mkutano huo, awali Mbatia
alipokewa na wananchi waliobeba mabango yaliyoandikwa “Hatuwataki
madiwani wa NCCR-Mageuzi, tunamtaka Mbatia pekee.”
Kumekuwa
na kutoelewana kati ya wagombea wa vyama vinne vya Ukawa - Chadema,
NCCR-Mageuzi, CUF na NLD kuhusu kuachiana kata na hata majimbo, kiasi
kwamba licha ya makubaliano ya wakuu wa vyama hivyo, wapo wagombea
waliogoma kutii maagizo hayo na sasa wamesimama kutetea nafasi
walizoomba.
No comments:
Post a Comment