Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imepuuza malalamiko ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) juu ya kauli ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Abdallah Bulembo, kuwa chama chake hakitakuwa tayari kuiachia Ikulu kwa namna yoyote ile, ikisema ni ya kisiasa na hayana madhara yoyote.
Mwenyekiti
wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema kwa sasa kila chama kipo
kwenye kampeni za kutafuta ushindi, hivyo kauli kama hiyo inaweza
kutolewa na upande wowote ikiwa ni mbinu ya kujipatia ushindi.
“Ingekuwa
kauli yake tafsiri yake ni kuwa hawatakubali matokeo ya uchaguzi hapo
tume ingekuwa imehusika na ingezungumza kwa kuwa tulishasema kila chama
shindani katika uchaguzi huu kinatakiwa kukubali matokeo
yatakayotangazwa na tume,” alisema.
Alisema hadi sasa NEC haijaona cha kujibu juu ya kauli hiyo na inaichukulia ni matamshi ya kisiasa ya kampeni.
Hivi
Karibuni Bulembo akiwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini
Kigoma, alidaiwa kutoa kauli kuwa chama chake hakitakuwa tayari kuiachia
Ikulu kwa namna yoyote ile.
Mwenyekiti
wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
akizungumza na waandishi wa habari, juzi alilalamikia kauli hiyo na
kuitaka NEC kulaani kauli hiyo kwa kuwa uchaguzi ni ushindani na hakuna
mwenye maamuzi zaidi ya wapiga kura.