Maoni:NEC Iwamulike Wanasiasa Wanaofanya Kampeni za MATUSI Ili Kuepusha Vurungu Nchini - LEKULE

Breaking

21 Sept 2015

Maoni:NEC Iwamulike Wanasiasa Wanaofanya Kampeni za MATUSI Ili Kuepusha Vurungu Nchini


Ndugu wasomaji,ni matumaini yetu kuwa mnaendelea vizuri na majukumu yenu ya kila siku ikiwemo kufuatilia kampeni za wanasiasa ikiwa ni kuelekea  uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwezi oktoba 2015.

Leo napenda nizungumzie  viashiria vya uvunjifu wa  amani  vinavyojitokeza  katika kampeni za wanasiasa mbalimbali kuanzia ngazi ya madiwani, wabunge na marais katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Kwanza nianze kwa kuwapongeza wananchi kwa kuwa wavumilivu kutokana na kampeni zinazoendelea hivisasa nchini za kushafuana, matusi, kejeli pamoja na chama A kutuma wafuasi wavamie chama B au kuvuruga mikutano.

Watanzania ni watu wavumilivu na wenye kupenda kuienzi amani tuliyoachiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa tuna amini kuwa machafuko yakitokea hatuna pa kwenda pia tumejionea jinsi majirani zetu na nchi nyingine wanavyopata shida yote haya ni kwa sababu ya machafuko yanayosabaishwa na baadhi ya watu au kikundi fulani cha watu kwa maslahi yao binafsi.

Aidha,Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo iliyobeba dhamana ya kuangalia kama kuna viashiria vya uvunjifu wa amani kwa wanasiasa  katika kampeni zao zinazo endelea hivisasa nchi Tanzania ikiwa ni siku 34 zimebaki kufikia uchaguz mkuu unaodaiwa utakuwa wa Kihistoria tangu miaka 50 ya uhuru.

Kwa mujibu wa  maadili ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa uachaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 kifungu cha 2.2 (a) Viongozi wa Vyama vya Siasa, kinabainisha kuwa Wagombea hao hawatakiwi kufanya fujo au kusababisha vurugu ya aina yoyote katika mkutano wa Chama kingine.

(b) Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wagombea wao hawatakiwi kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjaji wa amani,  au kuashiria ubaguzi wa kijinsia, ulemavu au maumbile kwenye mikutano ya Kampeni.

Aidha, Maadili hayo kifungu (c) kinaeleza kuwa mtu yeyote haruhusiwi kuwa na/au kubeba silaha yoyote ikiwa ni pamoja na silaha za jadi au zana yoyote inayoweza kumdhuru mtu katika mkutano wa Kampeni au mkusanyiko wowote wa kisiasa,na kifungu

(d) kinaeleza kuwa hairuhusiwi kuwa na/au kubeba sanamu, kinyago au kitu chochote ambacho kinaonyesha kudhalilisha, kukebehi au kufedhehesha Chama kingine cha Siasa au Kiongozi wake au Serikali katika mkutano au mkusanyiko wowote wa Kisiasa.

Licha ya wanasiasa kuwa wanajua au wanapaswa kujua hivi vifungu vinasema nini, wanasiasa hao wamekuwa wanakiuka maadili hayo kwa wazi kabisa kana kwamba wapo juu ya kanuni na maadili ya NEC  pasipo Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchukua hatua ikiwemo kukemea vikali viashiria hivyo vya uvunjifu wa sheria husika, sheria zilizowekwa kwa madhumuni maalumu.

Wanasiasa wamekuwa wakitukana matusi hadharani ikiwemo Chama A kutukana chama B.
 
Lakini kinachoshangaza Tume ambayo tunasema inatakIwa  itende  haki na usawa kwa wanasiasa hao imekuwa ikiegemea chama kimoja au upande mmoja.

Nina imani watanzania mtakubaliana na mimi kwamba kinacho endelea kwenye kampeni za wanasiasa ni aibu hata kwa watoto kusikiliza kauli za wanasiasa tunao dhani eti ndio watakuwa watawala wetu siku zijazo huku wafuasi wao wakishangilia; najiuliza utu wetu uko wapi ?, je, huu ndio uzalendo tunao sema kwa wanasiasa wetu?

Kwa maoni  yangu  naomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi imulikwe ili  iweze kuchukua hatua kwa haraka  kwani sisi wananchi wa kawaida machafuko yakitokea hatutakuwa na pa kwenda kwa sababu wenzetu wanasiasa watapanda ndege  na kuelekea Ulaya  wakati wananchi wa kawaida hatujui  ata Pasipoti ya kusafiria  inafananaje  na  inapatikana wapi.

Wanasiasa wengi wamekuwa hawaelezi sera kwa wapiga kura, wamekuwa wakitukana Chama kingine au mgombea mwingine.

Kwa mfano, Jana huko Chato,Geita Chama kimoja kati ya vyama vikubwa kilifanya  kampeni zake za kuomba ridhaa ya wananchi kuingia Ikulu. 
 
Mmoja wa wanasiasa wazungumzaji alipopanda jukwaani alianza  kumshambulia mgombea wa chama kingine huku akisahau  kunadi sera za chama chake.

Kilichonisikitisha zaidi ni pale alipodiriki kusema mgombea huyo wa urais katika chama Chenye nguvu  kubwa  hivisasa  alijinyea akiwa stendi. 

Sasa najaribu kujiuliza, kama ni kweli alijinyea;
1.Ni  nani Alikizoa kile kinyesi?
2.Kuna ushahidi wowote unaoonyesha jinsi mgombea huyo alivyojinyea hadharani?
3.Hivi wafuasi wake wangekuwepo eneo hilo, amani ingetawala kweli?


Badala ya watendaji wa NEC  kukaa maofisi  tu, wangesambaza mawakala wao nchi nzima kuangalia mienendo ya wanasiasa katika kampeni zao kwa maana ya kufuatilia  kwa karibu  nini kinaendelea na kuchukua hatua endapo kuna uvunjifu wowote wa sheria ikiwemo kampeni za matusi.