Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amesema kama Lowassa atafanikiwa kuingia madarakani Watanzania walioficha fedha nje ya nchi watazirudisha.Sumaye alitoa kauli hiyo jana alipohutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Laini Polisi mjini Nzega, Mkoa wa Tabora.
Kwa mujibu wa Sumaye, fedha hizo ambazo Serikali ya CCM imeshindwa
kuzirudisha zitatakiwa kurudi kwa sababu ni mali ya Watanzania.
“Jana (juzi) mmemsikia Magufuli (Mgombea urais wa CCM, Dk. John
Magufuli), akisema atakapoingia madarakani atarudisha mashamba ya
wananchi yaliyoporwa.
“Kwanza kabisa namwambia Magufuli kwamba Ikulu haingii, lakini sisi
tutakapoingia madarakani tutahakikisha walioiba fedha za Watanzania na
kuzificha huko Ulaya au Uswisi wanazirudisha,” alisema Sumaye.
Sumaye pia alizungumzia suala la rushwa nchini na kusema kama CCM
wangekuwa waungwana wasingemsimamisha mtu yeyote kugombea urais kwa
sababu wameshindwa kuwaletea maisha bora Watanzania.
“Magufuli anasema akiingia madarakani atakomesha rushwa sasa kama ana
uwezo huo kwa nini ameshindwa kuikomesha wakati na yeye ni waziri
katika Serikali iliyokithiri kwa rushwa?
“Magufuli anasema akiingia madarakani atakuza uchumi, kama kweli ana
uwezo wa kukuza uchumi kwa nini ameshindwa kuukuza kupitia Serikali ya
CCM ambayo yeye ni waziri?
“Magufuli hana lolote, msimchague kwa sababu ameshiriki kununua feri
mbovu inayotoka Bagamoyo kwenda Dar es Salaam,” alisema Sumaye.
Katika maelezo yake, Sumaye alizungumzia pia taarifa za viongozi wa
CCM wanaodaiwa kuwatisha wananchi wasimchague Lowassa kwa kisingizio
kwamba nchi itaingia katika vita kama ilivyotokea Libya na katika nchi
nyingine za Afrika Kaskazini.
Sumaye alisema hakuna vita itakayotokea wapinzani watakapoingia
madarakani na kwamba vita hiyo itatokea kama Serikali ya CCM haitataka
kuondoka madarakani.
No comments:
Post a Comment