CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Hai kimemtaka Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili kuhusu gari alilokuwa akitumia kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 100 mwaka jana.
Katika
tukio hilo lililojiri Machi 26, 2014 pembe hizo zilikutwa zikiwa
zimebebwa na gari lenye namba za usajili STK 8394 lililokuwa likitumiwa
na Sumaye. Gari hilo lilikamatwa eneo la Ulanga mkoani Morogoro ambapo
katika majibu yake (Sumaye) alidai ni mchezo mchafu uliofanywa na
mafisadi kuzuia ndoto zake za kugombea urais.
Mwenyekiti
wa CCM wilayani Hai, Amini Uronu alisema hayo jana mjini hapa wakati
akijibu baadhi ya madai yaliyotolewa na Sumaye ambaye kwa sasa amejitoa
ndani ya CCM na kuungana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Katika
madai ya Sumaye kwa wananchi katika viwanja vya Half London wilayani
Hai, alitaka CCM iwaeleze Watanzania kuwa nani anafanya biashara ya
pembe za ndovu.
“Viongozi
wa Ukawa juzi, walifanya mikutano wilayani Hai na kufanya upotoshaji wa
masuala mbalimbali, moja ya mambo Sumaye alihoji juu ya biashara ya
pembe za ndovu… Sasa sisi tunataka ajibu tuhuma baada ya gari lake
kukutwa na pembe hizo, asiwahadae wananchi amtaje mmiliki wake,” alisema Uronu.
Uronu
alidai pia katika madai yake kwa wakati huo, Sumaye alimtaja Waziri
Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambaye sasa ni mgombea wa urais
kupitia Chadema, kuwa ni miongoni mwa waliofanya njama hizo.
“Pia
Sumaye katika kauli zake alidai kuwa iwapo CCM ingemteua Lowassa kuwa
mgombea urais kupitia chama hicho yeye angejitoa, leo anakuja kuwahadaa
wananchi wakati sasa ndiyo anamnadi kuwa ni mtu mwadilifu na
mchapakazi,” alisema.