Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu THRDC pamoja na kituo cha haki za binaadamu LHRC wameamua kufungua kesi kupitia wakili Jebra Kambole kupinga baadhi ya vipengele kwenye sheria ya makosa ya mtandao mpaka pale vitakapofanyiwa marekebisho.
Vipengele
vinavyopigwa ni kifungu cha 4, 5 na 45 (4) cha Sheria ya Makosa ya
Mitandaoni ambacho kinazuia haki ya kupata na kutoa taarifa ambacho
kinakinzana na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano Tanzania.
Vipengele
vingine ni Kifungu cha 6, 7, 8, 10, 11, 14, 19, 21 na 22 ambavyo vina
maneno yasiyo na tafsiri na kuweza kusababisha tafsiri mbaya kwa
watekeleza sheria na hivyo kupelekea uvunjifu wa haki za binadamu
ambavyo vinakiuka Ibara ya 17 ya Katiba.
Vifungu
vya 31,33,34,35 na 37 vya sheria hiyo vinatoa mamlaka kwa Polisi
kufanya upekuzi bila idhini ya Mahakama hivyo ni uvunjufu wa haki za
binadamu na inakinzana na Ibara ya 16 ya Katiba.
Vipengele
vingine, Kifungu cha 38 cha sheria hiyo kinanyima haki ya mtu
kusikilizwa na Mahakama huvyo inakinzana na Ibara ya 13 (6) ya Katiba
pamoja na kifungu cha 47 (1) cha sheria hiyo kinanyima Polisi kufanya
kazi zao kama ilivyo katika Sheria hii.
Hatua
hiyo ya kufungua kesi imekuja baada ya Aprili mwaka huu Bunge kupitisha
sheria ya makosa ya mitandaoni (Cybercrime Act 2015) ambapo watetezi wa
haki za binadamu hapa nchini kwa kushirikiana na mashirika ya Kimataifa
yalifanya uchambuzi na kubaini kuwa baadhi ya vipengele katika sheria
hiyo vilikuwa na mapungufu makubwa.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam nje ya Mahakama Kuu,
Mkurugenzi wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema uchumbuzi uliofanyika
ulibaini kuwa sheria iliyopitishwa ni mwiba kwa uhuru wa vyombo vya
habari, haki ya falagha na haki ya watu kupata taarifa na kutoa maoni.
Olengurumwa
alidai, baada ya wadau hao kuyagundua makosa hayo ambayo yalikuwa
yanafinya haki za binadamu waliamua kutoa maoni ambayo serikali
iliahidi kuyafanyia marekebisho. Lakini licha ya sheria hizo kufanyiwa
marekebisho bado kunavipengele ambavyo vinamakosa.
Ndani
ya sheria hizo waligundua kuwa endapo sheria hiyo itaendelea kutumika
itakuwa imekiuka haki za binadamu kama, Uhuru wa habari, uhuru wa maoni,
uhuru wa kutafuta habari, Haki ya faragha, Haki ya kuifikia Mahakama na
Haki ya kusikilizwa.
Anasema
Mei 22 mwaka huu Serikali ilitangaza kutumika sheria ya makosa
mitandaoni pasipo kufanyiwa marekebisho ambayo yalipendekezwa na wadau
wa haki za binadamu.
“Ikumbukwe
kuwa kabla ya sheria hiyo kupitishwa Mashirika yasiyopungua 55 mwaka
huu chini ya uratibu wa THRDC yalimwandikia barua Rais Kikwete ya
kumsihi asitie saini kabla ya sheria hiyo kufanyiwa marekebisho lakini
pia ilipuuzwa”. anasema Olengurumwa.
Aidha
alisema, kutokana kwamba sheria hiyo imeanza kutumika THRDC pamoja na
mashirika mbalimbali ya Haki za Binadamu wakiungana na jopo la
wanasheria saba tumeamua kumuunga mkono na kufungua kesi kupitia wakili
wa kujitegemea Jebra Kambole ambaye ndiye mlalamikaji katika kesi hiyo
katika kuhakikisha kuwa baadhi ya vipengele katika sheria hiyo
vinapigwa.
“Ikumbukwe
kuwa taratibu za kisheria zinapendelea zaidi kesi kama hizi
zifungukuwe na mtu binafsi na si shirika hivyo tunamuunga mkono hadi
mwisho. Na endapo Mahakama itashidwa kutenda haki katika kesi hii basi
tutaipeleka mbele zaidi katika Mahakama ya Afrika Mashariki kwa ajili ya
kupata utatuzi,” anasema Kambole.
Jopo
la Mawakili hao saba ni, John Seka, Massawe Fulgence, Harold Sungusia,
Benedict Ishabakakaki, Jebra Kambole (wakili wa kujitegemea), Boka
Iyamuya, Neema Ndemno na Geremia Mtobesia ambapo kesi imepewa jarada la
Miscellaneous Civil Case namba 32 ya mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment