Balozi
Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Hemed Iddi Mgaza
kulia akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha rasmi na
kuaga baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Balozi Hemed
Iddi Mgaza akimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif kwenda kutekeleza vyema majukumu yake ya Kidiplomasia wakati
atapowasili kwenye Kituo chake cha Kazi Nchini Saud Arabia.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipongeza Serikali ya Mamlaka ya Saud Arabia
kupitia Mfuko wake wa Misaada ya Maendeleo { Saud Fund } katika kuiunga
mkono Zanzbar kwenye miradi ya Maendeleo katika Sekta ya Mawasiliano ya
Bara bara.
Pongezi
hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi wakati akizungumza na Balozi Mteule wa Serikali ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Nchini Saudi Arabia Balozi Hemed Iddi Mgaza
aliyefika Ofisini kwake Vuga kuaga rasmi baada ya kuteuliwa rasmi
kushika wadhifa .
Balozi
Seif Ali Iddi alisema misaada ya Maendeleo inayotolewa na Serikali ya
Saud Arabia imewezesha kukamilika kwa ujenzi wa Bara bara za Wete -
Gando yenye urefu wa Kilomita 11.4 na Wete - Konde Kilomita 14.9 ambao
umekifanya Kisiwa cha Pemba kufungua milango ya Kiuchumi.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameelezea faraja yake kutokana na Nchi hiyo
kuahidi tena kugharamia ujenzi wa Bara bara ya Chake chake - Wete
yenye urefu wa Kilomita 22.1 kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa
Maendeleo ya Afrika { Badea } unaotarajiwa kutumia zaidi ya Dola za
Kimarekani Milioni 11.9.
Alisema
kwa vile Saudi Arabia imeonyesha kuendelea kuunga Mkono harakati za
kiuchumi za Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla alimuomba Balozi huyo Mteule
wa Tanzania Nchini Saud Arabia Balozi Hemed Iddi Mgaza kupeleka salamu
za shukrani kwa misaada hiyo.
Balozi
Seif alifahamisha kwamba licha ya majukumu makubwa yatakayomkabili
Balozi Hemed lakini lakini pia atakuwa na kazi ya ziada katika
kuhakikisha kwamba Waumini wa Dini ya Kiislamu kutoka Tanzania
wanatekelezea Ibada yao ya Hijja Nchinu humo katika hali ya amani na
utulivu.
Alisema
licha ya kwamba Wauimini hao wanasimamiwa na Vikundi mbali mbali vya
kusafirisha Mahujaji lakini bado jukumu la Ofisi ya Kibalozi ya
Tanzania iliyopo Nchini humo ina jukumu la kuhakikisha usalama wa Raia
zake.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Balozi Hemed Iddi Mgaza
kushajiisha Wawekezaji wa Saud Arabia kutumia fursa zilizopo Zanzibar
za Uwekezaji kuanzisha miradi yao ya Kiuchumi kwa lengo la kuendelea
kuimarisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya pande hizo mbili.
Balozi
Seif alisema ni vyema shajiisho hilo likaenda sambamba na kuomba
nyongeza zaidi za nafasi za masomo kwa Wanafunzi wa Zanzibar na Tanzania
ili wapate fursa za elimu ya juu kwenye vyuo vikuu vya Nchi hiyo.
Alimpongeza
Balozi Hemed Iddi Mgaza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo ukionyesha
wazi uwezo alio nao katika kutekeleza jukumu katika Nyanja ya uhusiano
na Diplomasia ya Kimataifa.
Naye
Balozi Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Saud Arabia
Balozi Hemed Iddi Mgaza alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba atatekeleza makujumu yake kadri ya uwezo na Taaluma
aliyonayo.
Balozi
Hemed aliahidi kwamba moja kati ya kazi yake kubwa ni kusimamia
Uhusiano na ushirikiano wa Kihistoria ulioanzishwa kati ya waasisi wa
Mataifa hayo mawili.
Mradi
wa Ujenzi wa Bara bara za Wete – Konde na Wete – Gando ulioendeshwa na
Kampuni ya Ujenzi ya Mecco na kuchukuwa kipindi cha Miezi 29 umegharimu
Dola za Kimarekani Milioni 17,325,593.96 sawa na Shilingi za Kitanzania
Milioni 23,389,551,848.75.
No comments:
Post a Comment