Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na vijana wa barza mbali mbali katika jimbo la Mfenesini.(Picha na Salmin Said, OMKR).
Katibu
Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema
anakusudia kumaliza matatizo ya maji na umeme katika visiwa vya Unguja
na Pemba iwapo wananchi wa Zanzibar watamchagua kuwa Rais katika
uchaguzi mkuu ujao.
Amedai
kuwa Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi imeshindwa kumaliza
matatizo hayo kwa kipindi cha miaka 53, hivyo wakati umefika wa kufanya
mabadiliko ya kiuongozi ili kumaliza matatizo hayo.
Akiwa
katika ziara ya kutembelea matawi na barza za Chama hicho Jimbo la
Mfenesini, Maalim Seif amesema katika kumaliza changamoto hizo
hatowabagua wananchi kwa misingi yoyote ikiwemo ya kidini, kabila, siasa
au eneo mtu analotoka.
Amesema
huu ni uchaguzi wa kufanya maamuzi juu ya hatma ya Zanzibar na mamlaka
yake, na kwamba chama chake ndicho chenye dhamira ya kuongoza mabadiliko
kwa kuzingatia maslahi mapana ya Wazanzibari.
Amewakumbusha masheha kutekeleza majukumu yao bila
kuingiza utashi wa kisiasa, kwa kuzingatia kuwa wao ni watumishi wa serikali na kamwe hawatakiwa kuwa wanasiasa.
Amesema wananchi wana haki ya kikatiba ya kujiunga na vyama wanavyotaka, hivyo amewataka kutoogopa kutekeleza wajibu huo.
Amefahamisha
kuwa dhamira ya CUF ni kuwaunganisha wazanzibari sambamba na kuleta
mabadiliko ya kweli, ili wananchi watumie uhuru wao kikamilifu bila
kunyanyaswa.
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amewataka
wananchi kuungana na kuendelea na mshikamano wao, ili kuhakikisha kuwa
wanakipatia ushindi chama hicho.
Miongoni
mwa maeneo aliyoyatembelea ni pamoja na Mashimo ya mchanga shehia ya
Kihinani, barza ya CUF meli nane, Bumbwisudi na Mfenesini.
No comments:
Post a Comment