RAIS Jakaya Kikwete, amesema hamshangai mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.John Magufuli kwa kukosoa utendaji kazi wa Serikali yake katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea.
Rais
Kikwete, alitoa kauli hiyo juzi, wakati akizungumza na wafanyakazi wa
Taasisi ya NDI yenye uhusiano na Chama cha Democratic, IRI yenye
uhusiano na Chama cha Republican, IFES na United States Institute of
Peace (USIP) mjini Washington nchini Marekani.
Taarifa
iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mjini Dar es Salaam jana,
ilisema Rais Kikwete anaunga mkono mwenendo wa kauli za Dk. Magufuli
kwa sababu kila kiongozi anapoingia madarakani anakuwa na aina yake ya
uongozi.
“Wamepata
kuja watu kwangu,wakaniambia mgombea wetu wa CCM anashutumu na
kusahihisha Serikali yangu na utendaji wake kwenye mikutano ya kampeni.
Niliwaambia hivi anavyofanya mgombea wetu ni jambo sahihi kabisa,lazima
afanye hivyo.
“Niliwaambia
nchi yetu, inahitaji mawazo mapya na mwelekeo mpya ulio tofauti na
uongozi wangu. Niliwaambia tusiporuhusu jambo hilo kufanyika, nchi yetu
itabakia pale pale ambako nimeifikisha mimi.
“Haya yatakuwa na makosa makubwa kwa sababu nchi yetu lazima isonge mbele kwa mawazo mapya,uongozi na staili mpya ya uongozi.
“Haya
ndiyo anayosema mgombea wetu. Vinginevyo ni jambo lisilokuwa na maana
kubadilisha uongozi kama hatuko tayari kukubali, kila kiongozi lazima
awe na staili yake ya uongozi na namna ya kuongoza na kuendesha nchi
yetu,” alisema.
Katika
mikutano yake Dk. Magufuli amekuwa akieleza namna asivyoridhishwa na
uwepo wa huduma mbovu katika sekta mbalimbali ikiwamo afya na maji, hali
inayowafanya wananchi waendelee kutaabika.
Dk.
Magufuli amekuwa akishangaa kuona dawa zinakosekana katika hospitali za
Serikali huku dawa hizo zikipatikana katika maduka binafsi na kuahidi
kupambana na majizi na mafisadi.
Mgombea
huyo pia amekuwa akishangaa pale ambapo baadhi ya watumishi
wanapoharibu aidha kwa kuiba fedha za umma au uzembe kazini kuhamishwa
vituo vya kazi, badala ya kufukuzwa na kushitakiwa.
Atamani kupumzika
Katika hatua nyingine,Rais Kikwete alisema anatamani muda uende kwa kasi zaidi ili akabidhi madaraka kwa rais wa awamu ya tano.
“Natamani
muda uende nikabidhi madaraka kwa rais wa tano ili nipate muda wa
kumpumzika,baada ya kazi ngumu ya miaka 10 ambayo ni kama mzigo
mkubwa,”alisema Rais Kikwete.
Miswada Kandamizi
Katika
hatua nyingine, Rais Kikwete aliwataka watu binafsi ama taasisi yoyote
wenye matatizo na Sheria ya Takwimu au Muswada wa Habari, wawasilishe
mapendekezo serikalini ili yafanyiwe kazi.
Alizitaka taasisi hizo kuacha kulalamika pembeni au kupitia vyombo vya habari.
Rais
Kikwete alitoa kauli hiyo, baada ya kuulizwa swali kuhusu madai ya
Sheria ya Takwimu na Muswada wa Habari, kuwa inavuruga sifa za
kidemokrasia chini ya uongozi wake.
“Nimelizungumza
hili siku za nyuma, napenda kurudia tena. Sheria ya Takwimu inahusu
takwimu rasmi za Serikali tu na wala si takwimu zote.
“Pili
sheria hii, inatokana na matakwa na taratibu za Umoja wa Mataifa na
sheria yetu imetungwa kwa kutilia maanani matakwa ya kimataifa…kwa nini
hili linakuwa tatizo kwa Tanzania pekee ni jambo gumu kueleza,”alisema Rais Kikwete.
Kuhusu Muswada wa Sheria ya Habari, Rais Kikwete alisema.“Nimelisema
hili huko nyuma,inaelekea halijaeleweka. Nilipata kusema pale Dar es
Salaam na hata wakati nazungumza na wabunge wa Sweden mjini Stockholm
kuwa kama mtu ana tatizo ama maoni na maudhui ya muswada ule, ayafikishe
serikalini tutafanyia kazi.
“Hatuna tatizo na jambo hili, ajabu nasikia wanalalamika tu na hakuna yeyote ambaye amefikisha maoni yake kwetu.
“Jambo
muhimu ambalo lazima sote tuelewane hapa ni kwamba muswada wowote, uwe
wa habari ama wa jambo jingine, lazima ulinde maslahi ya nchi
yetu,umoja,utulivu na usalama.
“Haya
ni mambo ambayo hatuna haja ya kujadiliana na yeyote kwa sababu nchi
zote duniani zinalinda kwa namna hii na zinaendeshwa namna hii,”alisema Rais Kikwete.