Mwigulu awashukia wapinzani wanaotumia hotuba za Baba wa Taifa - LEKULE

Breaking

5 Sept 2015

Mwigulu awashukia wapinzani wanaotumia hotuba za Baba wa Taifa


nch
Mwigulu Nchemba akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Kata ya Nkungi, wilayani Mkalama (Picha ya Maktaba yetu)
Naibu Waziri wa fedha, Mwigulu Nchemba, amewataka Viongozi/ watu wanaojifanya mabingwa wa kutumia baadhi ya hotuba za hayati Mwalimu Julius Nyerere kujinufaisha kisiasa, watumie pia hotuba za hayati Nyerere zenye mwelekeo wa kuwakosoa,ili waweze kuthibitisha ubingwa wao.
Amedai mabingwa hao wakiweza kutoa ufafanuzi hata kwa hotuba zinazowakwaza,kwa njia hiyo, watakuwa wanawajengea wananchi mazingira mazuri ya kutoa maamuzi stahiki Oktoba 25 mwaka huu wakati wa kuchagua viongozi wanaowataka.
Mwigulu ambaye anatetea nafasi yake ya ubunge jimbo la Iramba kwa awamu ya pili mfululizo, ametoa wito huo juzi kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge na udiwani, jimbo la Mkalama mkoani Singida.
Akifafanua,alisema hivi karibuni baadhi ya wagombea mbalimbali wakiwemo wa nafasi ya urais, wamekuwa wakitumia baadhi ya hotuba za hayati baba wa Taifa, wakilenga kuwaaminisha wananchi kuwa wawachague kwa madai watafuata nyayo za hayati baba wa faifa, na kwamba wanauchungu na wananchi.
“Wengi wa viongozi hawa wanajaribu kuwahadaa wananchi kwa kitendo chao cha kuhama CCM kimezingatia maneno yaliyowahi kutolewa na hayati baba wa taifa kuwa, mabadiliko usipoyapata ndani ya CCM, unaweza kuyapata nje ya CCM”,alisema.
Akifafanua alisema mabadiliko ya kweli yaliyokuwa akiyazungumzia hayati Nyerere, sio ya kuhama vyama, ni mabadiliko ya kiutendaji ambayo yatafanyika ndani ya CCM na si kwa kukimbilia upinzani.
Mwigulu alisema kuwa itapendeza zaidi endapo mabingwa hawa watazungumzia pia maneno yaliyotolewa na hayati rais wa kwanza,Nyerere,kwamba ‘anayekimbilia kwenda ikulu kwa kutumia fedha,fedha hizo atazirejeshaje’.
“Kama wao ni mabingwa,basi wazungumzie maneno ya hayati Julius Nyerere ya ‘ikulu kuna nini pale hadi mtu apakimbilie,mtu aote rushwa hadi kwenye vyuo mbalimbali,hizo pesa amezitoa wapi na kama amekopa,atazirejeshaje.Wakizungumzia maneno hayo ambayo yapo kwenye hotuba ya hayati baba wa taifa na kutupa majibu ya kuridhisha,pengine kidogo tunaweza tukawaelewa”,alifafanua zaidi.
Katika hatua nyingine,Mwigulu alisema wana CCM waliokihama Chama cha Mapinduzi baada ya kushindwa kwenye kura za maoni, huko walikokimbilia kutimiza azma yao au tamaa zao za kutaka uongozi, wasipopata wanachokihitaji, baada ya Oktoba 25 mwaka huu, watarejea CCM.
“Wewe fikiria mtu kama Lowassa amelelewa na CCM takribani miaka 40 sasa, kichwa chake chote hakina kitu kingine kimejaa CCM. Mambo ambayo atataka kuyaanzisha kwenye Ukawa yatakuwa na harufu kubwa ya CCM tu. Kwa hiyo, huko walikokimbilia kusaka uongozi njia yo yote ikiwemo ya matumizi ya makubwa ya rushwa, wamekwenda kuanzisha CCM (B) hakuna cha ziada”,alisema.
Akisisitiza, alisema upinzani kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu haupo kabisa, ni kilichopo ni CCM (A)na CCM (B ndizo zitakazochuana kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Aidha, Mwigulu ambaye hotuba yake ilikuwa ikikatishwakatishwa kwa kushangiliwa, amewataka wakazi wa mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla, wasikubali hadaa inayotolewa na mgombea urais kupitia Ukawa, eti akichaguliwa serikali yake ataiendesha kwa kasi ya aina yake ambayo haijawahi kutokea nchini.
Mwigulu amesema mgombea huyo, yeye mwenyewe hana kasi aina hiyo anayoisema.
“Ongea ya mgombea huyo, ninyi ni mashahidi, anaongea kwa kasi inayofanana na mwendo wa kinyonga, hotuba zake hazizidi dakika tano, kunyanyuka kwake kutoka kwenye kiti, ni kwa kasi ya kinyonga vile vile,hapo alipo hana kabisa kumbukumbu ya kitu cho chote kichwani mwake,na mbaya zaidi hawezi kusafiri kwenye barabara za vumbi kiuno kitamletea matatizo makubwa”,alisema.
Alisema chaguo la Watanzania kwa nafasi ya urais wa awamu ya tano, ni DK. John Pombe Magufuli, ambaye ni mtu asiyekuwa na makandokando, mwadilifu na mchapakazi wa kupigiwa mfano.
Mwigulu,alisema anayoimani kubwa kwamba Watanzania wote watampa DK. Magufuli kura ya ndio na watachagua wabunge na madiwani wote kutoka CCM A na si vinginevyo.

No comments: