Mke wa zamani wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Rose Kamili jana aliibuka na kumtuhumu mzazi mwenzake huyo kwamba anatumiwa kuvuruga upinzani katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamili
alitamka bila kuthibitisha moja moja kwamba mumewe huyo wa zamani
anatumiwa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku
akihoji uadilifu wake katika jamii.
Lakini
jana alipotafutwa kwa njia ya simu kujibu madai hayo ya chama chake
kumtumia Dk. Slaa kuusambaratisha upinzani, Katibu wa Itikadi na Uenezi
wa CCM, Nape Nnauye, alisema hana taarifa na hivyo apewe muda kabla ya
kutoa taarifa kamili.
“Sina
taarifa kama Rose Kamili kazungumza na vyombo vya habari leo. Ndiyo
kwanza nasikia kwako, naomba unipe muda niweze kusoma yote aliyoyaeleza
ndipo nikujibu,” alisema Nape.
Katika
mkutano wake jijini Dar es Salaam juzi, Slaa aliyekuwa kimya kwa siku
kadhaa alitangaza kuachana na shughuli za siasa kutokana na kile
alichoeleza kuwa ni kutoridhishwa na mwenendo wa chama chake, hasa
katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais uliompa nafasi Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wa Chama hicho.
Dk.
Slaa alimuelezea Lowassa kama mtu asiye na maadili wala sifa ya kuwa
Rais wa Tanzania kwa sababu anahusika katika tuhuma kadhaa za ufisadi
ikiwemo ile kashfa ya zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura iliyohusisha
kampuni ya Richmond LLC na baadaye Dowans.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamili anayedai kuzaa
watoto wawili na Dk. Slaa, alisema anachofanya sasa kiongozi huyo wa
zamani wa Chadema, ni kukamilisha sehemu ya kazi aliyotumwa na baadhi ya
makada wa chama tawala kwa nia ya kuisaidia katika kampeni za uchaguzi
mkuu kwani ni kwa muda mrefu alikuwa akifuatwa na kuahidiwa ubunge na
uwaziri pindi akikubali kuachana na Chadema.
Hata
hivyo, Kamili naye hakuweza kufafanua kama naye kwa hatua yake hiyo ya
kujitokeza hadharani kumshambulia mumewe huyo wa zamani, naye alikuwa
katumwa, au ulikuwa ni utashi wake binafsi.
Aidha
hakuweza kuweka bayana ni kwa nini hakujitokeza siku zote kuhoji
uadilifu wa mume wake huyo wa zamani tangu alipojitokeza kugombea urais
mwaka 2010 kupitia chama cha Chadema.
Alisema
baadhi ya vigogo wa CCM ndiyo waliokuwa wakiongoza mpango huo,
wakimuahidi Dk. Slaa vyeo hivyo huku yeye akiahidiwa kiasi kikubwa cha
fedha kama akikubali pia kuachana na Chadema.
Hata
hivyo, Kamili aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum kupitia Chadema katika
Bunge lililovunjwa Julai 9 mwaka huu, alisema kuwa yeye alikataa ‘ofa’
hiyo na kubakia katika chama chake, lakini kwa anachokifanya Dk. Slaa
sasa, ni dhahiri kuwa mzazi mwenzake amekubali kutumika na hivyo
hatashangaa akimuona kwenye majukwaa ya kampeni za CCM ili kumchafua
mgombea wa Ukawa na kukinadi chama tawala katika kampeni zinazoendelea.
Lakini
katika mkutano wake na waandishi wa habari Dk. Slaa alitamka bayana
kwamba anaachana na siasa na hana mpango wa kurudi CCM. Kamili alidai
kwamba Dk. Slaa vilevile aliitwa na kigogo mmoja ndani ya Kanisa
Katoliki na kushawishiwa akubali mpango huo wa kujiweka pembeni Chadema
na kuitumikia CCM.
Alisema
baada ya kumalizana na Dk. Slaa ndipo wakamgeukia yeye na kumtaka
ahamie kwao (CCM) ili washirikiane katika kampeni za CCM.
“Mimi
nimekataa... ila yeye amekubali na wakati wowote anaweza kutekeleza
kazi aliyoianza kwa kupanda majukwaani kushiriki kampeni za CCM,” alisema.
Lowassa na ufisadi
Aidha
alihoji Dk. Slaa kumuita mgombea urais wa Chadema kuwa ni fisadi,
akimtaka ajihoji yeye mwenyewe kuhusu matendo anayoyafanya katika
familia, kabla ya kuwahubiria wengine kuhusu maadili na misingi bora.
Kamili
alisema kabla ya Dk. Slaa kuhoji mambo ya Lowassa ajihoji yeye mwenyewe
kuhusu sababu zilizomfanya aondoke Baraza la Maaskofu Katoliki (Tec)
akiwa kama Katibu mkuu na pia Kasisi wa kanisa hilo.
Aidha
alikanusha taarifa zilizotolewa na Dk. Slaa kwamba yeye (Slaa) na
familia yake wamekuwa wakila mihogo kama sehemu ya kutunza uaminifu
wake, na kusisitiza kwamba kuwa siyo za kweli.
Kwa nini kajitokeza
Kamili
alisema aliamua kujitokeza kuzungumza hadharani ni baada ya mzazi
mwenziwe huyo kugusia masuala ya familia wakati alishaitelekeza kwa muda
mrefu, pale alipoamua kuishi na mchumba wake mpya Josephine
Mushumbusi.
Kwa
mujibu wa Kamili, mbali na mzazi mwenziwe kuitelekeza familia yake,
hakuwa, pia hajawahi kuwa na maisha magumu kiasi cha kula mihogo kama
alivyodai, na kuongeza kwamba labda kama alikuwa anazungumzia watoto
wake (Slaa) ambao amewatelekeza.
“Alisema
yeye na familia yake wamekuwa wakila mihogo…hata kama mihogo ni
chakula, watoto wangu hawajawahi kula mihogo hata kama aliwatelekeza
labda watoto wake anaoishi nao. Huo ni uongo, ni upotoshaji. Atoe
ufafanuzi kw Watanzania hao watoto anaowazungumzia ni watoto gani. Kama
wewe ni muongo, huwezi siasa.” Kamili alisema
Kuhusu ndoa
Kamili
alisema katika mkutano wa juzi, Slaa hakueleza kwa usahihi juu ya suala
la ndoa kwa kudai kuwa serikali ya CCM ndiyo iliyoweka pingamizi dhidi
ya maamuzi ya kufunga ndoa na mchumba anayeishi naye, Josephine
Mushumbuzi.
Badala
yake, Kamili alisema maneno hayo si ya kweli kwani yeye (Kamili) ndiye
aliyeweka pingamizi hilo kwavile ndiye mke wa halali na kwamba, haiingii
akilini kwa taasisi kama CCM kuweka pingamizi la ndoa ya mtu.
Alisema
maneno hayo ni ya uongo kwani yeye ndiye aliyeweka pingamizi hilo
kwa sababu ndiye aliyefunga naye ndoa na kwamba ingewezekana kuwekwa
pingamizi na CCM iwapoa alifunga ndoa na chama hicho.
Alisema
yeye na familia yake ya watoto wawili, Emiliana na Linus Slaa, wamekuwa
wakimfichia siri nyingi lakini kwa taarifa hizo zimemfanya kuibuka
huku akimtaka kuomba msamaha kwa kuwasema viongozi wa dini kwamba
walipokea rushwa ya mamilioni kutoka kwa Lowassa.
Kugombea urais
Kamili
alipinga madai ya Dk. Slaa kwamba hakuwa tayari kugombea nafasi ya
urais kupitia Chadema, akisema ukweli wa suala hilo unadhihirishwa na
ziara yake (Slaa) ya Ujerumani alikojifunza namna ya kuvaa na kujieleza
mbele ya hadhara wakati wa kampeni za uchaguzi.
Aidha,
Kamili alihoji ujasiri wa Dk. Slaa kumuita mgombea urais wa Ukawa,
Lowassa kuwa ni fisadi anautoa wapi wakati yeye (Slaa) amejawa na
matendo yanayotilia shaka uadilifu wake, baadhi yakiwa ni kumuacha mke
wa ndoa (yeye Kamili) na kuishi na mwanamke mwingine.
Kadhalika,
alidai sababu mojawapo ya Slaa kuondoka katika nafasi ya Katibu Mkuu wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec) ni kukosa uaminifu na hivyo,
kamwe hastahili kumnyooshea kidole Lowassa kwa tuhuma za kuzushiwa
kuhusu kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond.
No comments:
Post a Comment