Mgombea
urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa amesema
akichaguliwa kuwa rais wa Awamu ya Tano, ataunda tume tatu ikiwamo ya
kuchunguza upya sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili ambalo
utekelezaji wake ulilalamikiwa na wananchi.
Akizungumza
katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi
Kashaulili mjini Mpanda mkoani hapa, Lowassa alitaja tume nyingine kuwa
ni za kuchunguza mgogoro wa ardhi kati ya Kanisa la Efatha na wananchi
na mgogoro kati ya wakulima.
“Kuhusu
Operesheni Tokomeza wananchi wengi wamekuwa wakija kuniona na kunieleza
wazi kuwa licha ya madhara yaliyojitokeza katika operesheni hiyo
hawakulipwa, pia walipoteza haki zao, ndugu na mifugo."
Lowassa
aliyetokea Namanyere alikofanya mkutano mwingine wa kampeni, aliwataka
wananchi kuichagua Ukawa, kwa maelezo kuwa umoja huo utaleta mabadiliko.
Operesheni
Tokomeza Ujangili ilibuniwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo
la kupambana na ujangili ambao ulikithiri hadi taasisi za kimataifa
kuingilia kati.
Hata
hivyo, ilisitishwa Novemba Mosi, 2013 ili kupisha uchunguzi wa
malalamiko yaliyojitokeza, yakiwamo ya wananchi kuuawa, kuteswa na
kuporwa mali zao.
Uchunguzi
huo ulifanywa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na
sakata hilo lilipowasilishwa bungeni na kamati hiyo, lilisababisha
mawaziri wanne kushinikizwa na Bunge kujiuzulu, kutokana na kuhusishwa
na yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo.
Mawaziri
waliong’oka ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi
Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Balozi Hamis Kagasheki
(Maliasili na Utalii) na Dk Mathayo David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi).
Hata
hivyo, hivi karibuni Ikulu iliwaondolea doa mawaziri hao kutokana na
ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza tuhuma za
ukiukwaji wa haki za binadamu, wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo
kwa maelezo kuwa waliwajibika kisiasa na hawakuhusika moja kwa moja na
vitendo hivyo na hakuna hatua inayostahili kuchukuliwa dhidi yao.
Kuhusu mgogoro wa kanisa la Efatha na wananchi alisema: “Suala
hili linalalamikiwa sana na kwa muda mrefu linawatesa wakulima na
wawekezaji. Katika kuwalinda wakulima wadogowadogo itaundwa tume ili
kuchunguza suala hili ili hatua za haraka zichukuliwe.”
“Kwa
muda mrefu kumekuwa na ugomvi kati ya wakulima na wafugaji, hasa
waliopo katika Bonde la Mto Rukwa. Nitaunda tume ili kuhakikisha kuwa
naondoa migogoro hii ambayo imedumu kwa muda mrefu,” alisema.
“Serikali
yangu itanunua mahindi kwa wakulima na itawalipa riba. Haya ndiyo
mabadiliko ninayoyataka. Wanaosema hawana sera wanajidanganya sana
nawaambieni mkinipa kura nikaingia Ikulu wataisoma namba,” alisema.
Mbowe: Tumeunganisha nguvu
Akizungumza
katika mkutano huo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema:
“Tumeunganisha nguvu za Watanzania wenye dhamira na mapenzi mema
wanaotaka kuona mabadiliko ya nchi yetu. Tumempokea Lowassa kwa sababu
tunaamini atatusaidia safari yetu ya kuwakomboa Watanzania.
“
Mgombea (Lowassa) ameteswa sana CCM na ndoto yake ya uongozi ilikuwa
siku nyingi, lakini CCM hawakuiona hiyo na wakampuuza kwa maneno ya
uongo.”
Mbowe
alisema Rais Kikwete alimtosa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika
mchakato wa CCM kupata mgombea wake wa urais na kushangazwa na kitendo
cha Pinda kuendelea kubaki CCM.
Mawaziri
wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Lowassa nao walichukua fomu za
kuomba ridhaa ya CCM, lakini baada ya kutopitishwa kuwania urais
walihamia Ukawa.
Kada
mpya wa Chadema, Hamis Mgeja alisema: “Miradi ambayo Magufuli (Dk John)
alishindwa kuijenga kwa ubora itajengwa na kumalizwa chini ya utawala
wa Lowassa.
No comments:
Post a Comment