MWENYEKITI Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, amewataka Watanzania kumpuuza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa kwa kauli zake zilizojaa uchochezi na propaganda za siasa.
Pia
alionya kauli za ovyo zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwamba wapinzani wakishinda vyombo vya ulinzi vitachukua
nchi.
Alisema
jeshi la Tanzania linasimamia misingi yake na kiongozi yeyote
atakayeingia madarakani litafanya naye kazi kwa kuwa wote ni Watanzania.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kufafanua mambo mbalimbali
yalitamkwa na Dk. Slaa juzi, Mbatia alisema tuhuma alizozitoa kiongozi
huyo zinalenga kuleta mpasuko katika taifa na kuvunja amani ya nchi.
Alisema
hotuba nzima ya Dk. Slaa ililenga kumshambulia moja kwa moja Mgombea
urais wa Ukawa, Edward Lowassa kwa sababu amekuwa tishio kwake na kwa
CCM.
Mbatia
ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema mara zote propaganda
kama hizo huwa zinafanywa na chama tawala ambacho kimekwisha kuona
viashiria vya kuondolewa madarakani kupitia sanduku la kura.
Mbatia
alitoa mfano kuwa kitendo cha Dk. Slaa kuwasingizia baadhi ya viongozi
wa dini kwamba walihongwa na Lowassa ili wamuunge mkono ni hatua ya
kuwataka waumini wasiwaamini viongozi wao jambo ambalo ni hatari kwa
amani ya nchi.
“Hoja
alizozitoa ni nyepesi ambazo Watanzania wanatakiwa kuzipuuza na
wasikubali mpasuko hasa unaoletwa kwa mlengo wa imani ya dini.
“Kuwahusisha viongozi wa dini na tuhuma za uongo ni siasa nyepesi za mtaroni.
“Kusema eti Lowassa anaungwa mkono na Walutheri kwa sababu ni wenzake ni mpasuko mkubwa katika nchi,” alisema.
Mwenyekiti
huyo wa NCCR Mageuzi alisema alisikitishwa na uongo uliosemwa na Dk.
Slaa kwamba hakuunga mkono kuingia kwa Lowassa Chadema kwa sababu
mwanasiasa huyo alishiriki kwa ukamilifu mchakato mzima wa kumshawishi
Lowassa na wenzake kujiunga na Ukawa.
“Nimesikitishwa
sana na uongo uliosemwa jana na kaka yangu Dk. Slaa kwa sababu
alishiriki katika kumshawishi Lowassa na wengine kujiunga nasi katika
harakati za mabadiliko ya kweli,”alisema Mbatia.
Alisema
kusema kwamba Lowassa alitoa ahadi ya kujiunga na Ukawa akiwa na kundi
kubwa la wana CCM ni kutunga na hauna mashiko ya katiba na kanuni kwa
vile hakuna katiba yoyote ya chama cha siasa yenye masharti kama hayo.
“Lowasa
alipokuja Ukawa hakutoa ahadi ya kuja na viongozi na pia hakuna
masharti aliyopewa kwa sababu alifuata taratibu zote za kujiunga
Chadema.
“Mbona mwaka 1995 yeye (Dk. Slaa) alipokatwa na CCM na kuhamia upinzani hakupewa masharti wala kubaguliwa?
“Katiba
ndiyo inayotoa utaratibu wa mtu kujiunga na chama sasa yeye ni nani
mpaka awe juu ya Katiba ya Chadema? Mbona yeye hakubaguliwa na
aliendelea kufaidika hadi akagombea urais?” alihoji Mbatia.
Kuhusu
kauli kwamba Dk. Slaa alikuwa hajaomba wala kuteuliwa na chama chake
kugombea urais, Mbatia alisema kabla ya kuingia Lowassa Ukawa, tayari
Chadema kilikuwa kimekwisha kumteua Dk. Slaa kuwa mgombea ambaye
angepambana na wenzake kutoka Chama Cha Wananchi (CUF) na NCCR.Mageuzi.
“Si
kweli kwamba Dk . Slaa hakuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais,
bali chama chake kilikwisha kumteua na yalipojitokeza majina ya Profesa
Ibrahim Lipumba na Dk. George Kahangwa, alisema yeye ndiye mwenye vigezo
vyote vya kuteuliwa kuwa mgombea wa umoja huu.
“Tulifanya
vikao mbalimbali kikiwamo tulichofanya nyumbani kwa Profesa Lipumba
lakini hatukufikia muafaka, lakini baada ya Lowassa kujiunga tulimwomba
kwa pamoja agombee urais.
“Sababu
iliyotufanya tumshawishi Lowassa agombee nafasi hiyo ni nyota yake ya
siasa aliyonayo. Je, haya mafuriko tunayoyapata na tuliyopata pale
Jangwani tungeyapata?
“Hizo
tuhuma za ufisadi wanazozitoa juu ya Lowassa …tukianza kuwataja kwa
masakata yaliyotokea katika uongozi wa Rais Kikwete (Jakaya) hakuna hata
mtu mmoja atakayebaki.
“Sakata
la EPA, BoT (Benki Kuu), Deep green, Richmond, vichwa hewa vya treni…
hakuna atakayebaki msafi. Hivyo ufisadi si mtu bali mfumo,” alisema Mbatia.
Alisema
mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, anaweza kueleza namna
alivyosimamia uuzwaji wa nyumba za serikali. Je, huo siyo ufisadi?
Mbatia alisema wale wanaotaka mdahalo na Lowassa si saizi yake bali yeye ndiye anaweza kupambana nao.
Alimtaka
Waziri wa Uchukuzi, Samueli Sitta, kuwaeleza Watanzania fedha za
serikali alizotumia kujengea nyumba ya Spika kule Ulambo wakati akijua
usipika ni kazi ya muda tu.
No comments:
Post a Comment