ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha (45) amewasilisha mahakamani pingamizi juu ya kesi inayomkabili ya kutumia lugha ya matusi kwa maofisa wa Jeshi la Polisi, akisema mashitaka aliyofunguliwa ni batili.
Kupitia kwa wakili wake, Peter Kitabala, Masha aliwasilisha pingamizi
hilo akiwa na hoja tatu za kisheria katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilikuwa umekuja kwa kutajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi
Mkuu, Waliarwande Lema ambapo Wakili wa Serikali, Sakina Sinda, aliomba
iahirishwe kwa kuwa upelelezi haujakamilika.
Ndipo Wakili Kibatala akasema wamewasilisha pingamizi, kupinga
uhalali wa mashitaka dhidi ya Masha na kwamba Septemba Mosi, mwaka huu
walipeleka nakala ya pingamizi hilo kwa upande wa Jamhuri, hivyo
walitarajia jana wangesikiliza.
Kutokana na hoja hiyo, Sakina aliiomba mahakama iwape muda ili
wapitie pingamizi hilo na kuwasilisha majibu kwa sababu bado
hawajaliona.
Katika pingamizi hilo, Masha anadai kwamba hati ya mashitaka ni
batili, haina hadhi ya kisheria kwa kuwa maofisa wa polisi siyo miongoni
mwa watu wanaohusishwa na kifungu cha 89 (1) cha Sheria ya Kanuni ya
Adhabu.
Anazidi kudai kwamba hati hiyo ni batili kwa kuwa imeshindwa kueleza
ni kwa jinsi gani lugha ya matusi anayodaiwa kuitoa inaweza kusababisha
uvunjifu wa amani. Aidha pingamizi linasema hati hiyo ni batili kwa kuwa
maneno yanayodaiwa siyo ya udhalilishaji na ya matusi, hivyo hayawezi
kutumika kama sheria inavyoeleza.
Hakimu Lema aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba mosi mwaka huu, itakapokuja kwa haua nyingine.
Katika shitaka hilo, Masha anadaiwa kwamba Agosti 24, mwaka huu
katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, alitoa lugha ya matusi kwa
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Juma Mashaka na wenzake akiwaambia ni
“wajinga, washenzi, waonevu, hamna shukrani, huruma wala dini,” maneno
ambayo polisi katika mashitaka yao wanadai yangesababisha uvunjifu wa
amani.
No comments:
Post a Comment