Makamu wa Rais Aadhimisha Kilele cha Siku ya (MARA DAY) Butiama Mkoani Mara. - LEKULE

Breaking

16 Sept 2015

Makamu wa Rais Aadhimisha Kilele cha Siku ya (MARA DAY) Butiama Mkoani Mara.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwasha Mshumaa katika Kaburi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kama ishara ya Kumbukumbu wakati alipofika katika Jumba la makumbusho Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015 baadda ya kuadhimisha Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) iliyofanyika Butiama
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiweka Shada la Maua katika Kaburi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kama ishara ya Kumbukumbu wakati alipofika katika Jumba la makumbusho Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015 baadda ya kuadhimisha Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) iliyofanyika Butiama. Kushoto ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Kenya, Eugene Wamalwa
CHIMBUKO LA MAADHIMISHO YA SIKU YA MARA.
1.  Utangulizi:
Maadhimisho ya siku ya Mara hutoa taswira ya jinsi viongozi na wananchi wanchi mbili za Kenya na Tanzania wanavyoshirikiana katika kusherehekea maadhimisho ya siku hiyo. Hii ni mojawapo ya shughuli muhimu katika kuimarisha ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kilele cha Maadhimisho hayo huwa ni tarehe 15 Septemba ya kila mwaka.
2.  Bonde la Mto Mara:
Bonde hili ni moja kati ya mabonde yenye mito inayoingiza maji katika Ziwa Victoria. Bonde hili linahusisha nchi za pande mbili ambazo ni Kenya ambayo inamiliki takribani asilimia 65 ya eneo bonde na Tanzania asilimia 35. Asili ya mto Mara ni chemichemi ya Enapuyapui iliyoko kwenye misitu ya milima ya Mau katika nchi ya Kenya na maji yake hutiririka kuelekea katika pori la akiba la hifadhi ya Taifa ya Maasai-Mara kwa upande wa Kenya, na kwa upande wa Tanzania mto Mara unapita katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti kabla ya kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria nchini Tanzania ambapo mto huo hupita katika Wilaya nne za Serengeti, Tarime, Butiama na Rorya. Ikolojia ya Bonde la mto Mara ni moja kati ya Ikolojia muhimu katika Bonde la Ziwa Victoria ambayo inachangia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii pamoja na utumiaji na uhifadhi wa uoto wa Asili.
3.  Chimbuko la Maadhimisho ya Siku ya Mara.
Maadhimisho hayo ni kufuatia maamuzi yaliyofanywa na Baraza la Mawaziri wanaohusika na masuala ya Bonde la Ziwa Victoria kwenye Mkutano wa kumi uliofanyika tarehe 04 Mei, 2012 huko Kigali Rwanda. Katika Mkutano huo iliamuriwa kuwa maadhimisho hayo yafanyike kwa kupokezana baina ya nchi zote mbili za Kenya na Tanzania.
4.  Faida ya maadhimisho haya:
Siku ya Mara hutumika katika kuendelea kulitangaza na kulifuatilia tukio muhimu la wanyamapori hasa nyumbu kuhama kutoka mbuga za hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda katika pori la hifadhi ya Taifa la Maasai-Mara katika Jamhuri ya Kenya na baadaye kurudi Tanzania na mara zote mbili wanyama hao huvuka mto Mara.
Uamuzi huo wa kuadhimisha Siku ya Mara, ulitokana na kutambua umuhimu wa Ikolojia ya Bonde la mto Mara ambapo siku hiyo itatumika kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mto Mara. Aidha, maadhimisho ya siku ya Mara pia hutumika katika kufanya yafuatayo:
i.                 Kujengea jamii uwezo juu ya uelewa wa masuala ya mazingira na changamoto za kijamii zinazojitokeza katika Bonde la mto Mara.
ii.                Kuwawezesha wadau kushiriki katika fursa zinazohusiana na Bonde la mto Mara
iii.              Kuitambulisha sura ya Bonde la mto Mara kama eneo muhimu la uwekezaji
iv.              Kujadili mwendelezo wa utekelezaji wa shughuli zilizoratibiwa katika Bonde la mto Mara.
5.  Changamoto zinazolikabili Bonde la mto Mara
Jamii inayoishi katika Bonde la mto Mara pamoja na wadau mbalimbali wameendelea kushuhudia upungufu mkubwa wa kiwango cha maji pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibinadamu, hali inayopelekea kuwa kikwazo kwa jamii inayoishi katika Bonde la mto Mara katika juhudi zao za kujiongezea kipato, kuwa na afya imara, kuwa na chakula cha uhakika pamoja na kukuza uchumi.
Changamoto hizi zinazotishia kutoweka kwa maliasili (Ikolojia) ya Bonde la mto Mara zinatokana na shughuli za kila siku za kibinadamu ambazo ni pamoja na matumizi ya ardhi yasiyo endelevu, ukataji miti holela kwa ajili ya kuchoma mkaa na ujenzi, uchimbaji holela wa madini, uchafuzi wa vyanzo vya maji, kilimo kisicho endelevu na ufugaji usio endelevu.
Shughuli zingine ni sera na sheria za nchi mbili kutofautiana, ukosefu wa elimu ya hifadhi ya mazingira kwa wakazi waishio katika Bonde la mto Mara, umaskini kwa wakazi wengi wanaoishi katika Bonde, udhaifu wa kusimamia sheria pamoja na ukosefu wa chombo shirikishi cha kusimamia rasilimali za bonde la mto Mara, hizi zikiwa ni baadhi tu ya changamoto. 

Makamu wa Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika  kwenye Uwanja wa Mwitongo, Butiama mkoani Mara. 

No comments: