Baadhi ya viongozi wa dini na wananchi wamesema shutuma za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa kuwa baadhi yao walihongwa na Mgombea Urais wa Ukawa kupitia Chadema, Edward Lowassa, ni upuuzi mtupu.
Wamemtaka
atoe ushahidi wa madai hayo kwa kutaja majina ya viongozi na kiasi
walichohongwa, wakisisitiza kuwa hizo ni siasa za majitaka na kwamba
anaifanyia kazi CCM ili apate njia ya kurudi katika chama hicho.
Rais wa TEC azungumza
Akizungumzia
shutuma hizo, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki
Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, amemtaka Dk. Slaa kutoa
ushahidi wa madai yake kuwa maaskofu wa kanisa hilo wamehongwa na Edward
Lowassa.
“Hizo
taarifa ndiyo nazisikia kwako, lakini kama kweli amesema hivyo kwa nini
hakuweka ushahidi kuanzia majina ya maaskofu hao waliopewa fedha, kiasi
na zilikopokelewa. Lakini kwa upande wangu binafsi sijapokea kiasi
chochote kutoka kwa mtu yeyote." Amsema askofu huyo
Askofu
Niwemugizi alimtaka Dk. Slaa kutoa uthibitisho wa maaskofu wa kanisa
hilo kupokea fedha kutoka kwa Lowassa waweze kutoa uamuzi.
“Lowassa
nimewahi kukutana naye nilimwalika kwenye shule yangu ya seminari kule
Biharamulo… shule yenyewe inaitwa Katoke na nilimuweka wazi sababu za
kumwalika na sikupokea kiasi chochote cha fedha kutoka kwake,”alisema askofu huyo na kuongeza:
“Athibitishe
hilo aonyeshe kiasi cha fedha na majina ya maaskofu, mimi sijapata
kiasi chochote labda kama nimetupiwa kwenye akaunti yangu bila mimi
kujua lakini nasisitiza atoe ushahidi.”
Wakati
huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa
Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la
Kipentekosti, William Mwamalanga alisema kauli za Dk. Slaa zina dalili
ya kuleta kisasi fulani.
“Angekuja
mapema kabla ya taratibu hizi kuanza tungemwelewa lakini kwa sasa yupo
nyuma ya wakati. Kwanza ameonekana amesukumwa afanye aliyofanya na hilo
haliwezi kuwabadilisha Watanzania walioamua kutaka mabadiliko,”alisema na kuongeza:
“Hotuba yake haina mashiko na taifa halihitaji watu wabinafsi,”alisema Mchungaji Mwamalanga.
Askofu Gwajima azungumza
Naye
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekana kuwa
mshenga wa Edward Lowassa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendelea
(Chadema) .
Pia
amekana kuhusika kuwarubuni kwa fedha maaskofu 30 wa Kanisa Katoliki
ambao wanadaiwa kumuunga mkono Lowassa katika mbio zake za urais baada
ya kuhongwa fedha.
Askofu Gwajima amesema Dk. Slaa ndiyo risasi ya mwisho iliyokuwa imebakia ndani kati ya bunduki ya CCM ili kuwaokoa.
Amesema
yote yaliyosemwa na Dk. Slaa ni tuhuma za uongo hivyo wananchi
wazipuuze kwa kuwa mwanasiasa huyo anatafuta uungwaji mkono kwa wananchi
aelekee CCM.
“Yaani
ni uongo kabisa tena uongo mweupe, imedhihirisha wazi kuwa huyu mtu
asingefaa kuwa rais. Ni dhahiri ameona akiwasema wanasiasa wenzake
watamjibu kwenye majukwaa yao ya siasa, lakini sasa amewasema maaskofu
kwa kuwa wao hawana majukwaa.
“Kwa
hiyo namshauri hayo mambo ya kuwahusisha maaskofu na uchaguzi aache
uongo wa namna hiyo. Nafikiri awaseme wanasiasa wenzake kuzungumzia
mambo ya siasa ila kuwahusisha maaskofu si mambo ya busara,” alisema.
Akizungumzia
suala la kuwa mshenga wa Lowassa na Chadema, Askofu huyo amesema
anafikiri Dk. Slaa ametumwa na waliomtuma, hivyo anawafanyia kazi watu.
“Kwa
kawaida inashangaza kwamba kama watu wawili wanagombana, inatakiwa
awepo mtu wa kuwaunganisha, ila anaposema maaskofu 34 haileti maana,
haiingii akilini… ameingiza Gwajima, Rostam (Aziz) na maaskofu,
haeleweki anachozungumza. Lakini ninachosema kuna waliomtuma ni watu
ambao anawafanyia kazi.
“Kikubwa
ni kwamba baada ya Lowasaa kuchaguliwa kugombea urais kwa Chadema
alichukia, alifikiri Lowassa hataendelea kuwa na umaarufu, sasa anaona
Lowassa anakwenda, hiyo imemtia hasira anataka kumchafulia Lowassa,
ndiyo maana anaongelea Lowassa Lowassa tu.
“Kwa
mfano alisema Lowasa angekuja na wabunge wenyeviti wa CCM, ina maana
angemkubali Lowassa aje nao, sasa angekuja nao asingekuwa fisadi? Ni
swali zuri ila amekwepa kulijibu.
“Nafikiri
Dk. Slaa ndiyo risasi ya mwisho iliyobakia ndani ya bunduki ya CCM.
Natoa wito kwa waumini wangu wafahamu kuwa hizi tuhuma ni za uongo na
namsihi huyo daktari asihusishe maaskofu na uongo wake abaki nao
mwenyewe,” alisema Askofu Gwajima.
No comments:
Post a Comment