Mgombea urais iliyesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ametua katika Jimbo Singida Kaskazini la Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazoro Nyalandu, huku akiwatahadharisha wananchi wasipompigia kura za kuitosha kuiondoa CCM madarakani watakuwa wamejiangamiza.
Aidha,
alimwelezea Nyalandu kuwa anamfahamu mbunge huyo kwa mbwembwe na nguvu
ya fedha na kuhoji kama mgombea ubunge kupitia Chadema katika jimbo
hilo, David Jumbe atamuweza.
Akizungumza
na mamia ya wananchi wa kijiji cha Ilongero, Jimbo la Singida
Kaskazini jana ikiwa ni mfululizo wa ziara zake ya kuomba ridhaa kwa
wananchi wamchague awe rais wa awamu ya tano, Lowassa alisema CCM
itaondolewa madarakani kama wananchi wengi watajitokeza kupiga kura ya
kuikataa.
“Watu
wanataka mabadiliko ya maisha yao na sisi tumejitolea kuleta mabadiliko
hayo,suala la kura ni muhimu sana mabadiliko yatakuja kwa kupiga kura
tusipopata kura za kutosha tumeeangamia,” alisema.
Lowassa
ambaye hadi sasa amefanya mikutano ya kampeni zaidi ya 32 katika
majimbo ya mikoa 11 aliyotembelea, alisema CCM imeshindwa kuleta
mabadiliko ya maendeleo na maisha ya wananchi yameendelea kuwa magumu.
“Wakati
wa mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM Nilisema huwezi
kuzuia gharika kwa mkono, sasa wameona gharika ya watu, tumekwenda
Mpanda, Tabora, Iringa na leo (jana) hapa kwenu hivyo hivyo watu ni
wengi,” alisema.
Mgombea huyo wa Ukawa aliwataka wananchi wasikubali kura ziibwe na kutaka apatiwe kura si chini ya milioni 12 ili awe Rais.
Alisema
serikali ya CCM imekuwa ikiahidi mambo mengi lakini haiyatekelezi na
kwamba serikali atakayoiunda itakuwa ya vitendo kwa kutekeleza mambo
yote.
Lowassa aliahidi akichaguliwa ataanzisha viwanda vya alizeti na vitunguu ili viwe vinasafirishwa kwenda masoko ya nje.
Kuhusu Nyalandu
Akimzungumzia Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Nyalandu, alisema anamfahamu kwa mbwembwe nyingi.
“Namfahamu
Mbunge wenu wa sasa, namfahamu kwa mbwembwe zake sasa namulize Jumbe
(mgombea Chadema) utamuweza maana kuna nguvu ya pesa na nguvu ya mtu,” alisema.
Hata hivyo, Jumbe alijibu kuwa tayari ameshamshinda Nyalandu.
Katika
hatua nyingine wazee wa mila wa kabila la kimasai na kinyatulu
walimkabidhi Lowassa fimbo na mgolole ili aitumie kwa ajili kuwachapia
wezi ili wasimzue kuingia Ikulu na kumtaka asiiache kila aendako.
Mgombea Ubunge CHADEMA
Naye
mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Singida Kaskazini, David Jumbe,
alimweleza Lowassa kuwa jimbo hilo linakabiliwa na kero za ubovu wa
barabara, ukosefu wa soko la kuuzia mazao na hivyo wakulima kulanguliwa
na wafanyabiashara.
“Mfano
soko la vitunguu ikifika wakati wa mavuno wafanyabiashara kutoka Kenya
wanakuja kwa wingi na kununua vitunguu na kwenda kuviuza nje kama bidhaa
iliyozalishwa nchini mwao,” alisema.
Alisema
kama akichaguliwa, askari wote wa mgambo watapewa majembe wakalime kwa
sababu kazi ya kusimama kwenye mageti kwa ajili ya kutoza ushuru
haitakuwapo na miti iliyopo katika mageti hayo itageuzwa kuwa kuni.
Tundu Lissu
Kwa
upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema CCM
haiwezi kuleta mabadiliko yeyote na hata ahadi ya Sh. milioni 50 kwa
kila kijiji ni danganya toto.
“
Lowassa ametukanwa na tumemsema sana lakini ukweli wa Mungu hakufanya
kosa lolote binafsi na hata wanaomtukana leo ni kwa sababu ameondoka CCM
na siyo kwa sababu ya kashfa ya Richmond” alisema.
Laurence Masha
Naye
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha, aliwataka wananchi
waiogope CCM, akisema imesababisha mateso makubwa kwao.
“Mtakayemuona ananunua shahada za kupigia kura katika eneo lenu, makamateni, mshughulikie na mtoweni katika eneo lenu,” alisema.
Mgeja
Kwa
upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis
Mgeja, alisema wanaotoka ndani ya CCM ni watu safi na waonang’ang’ania
ni wachafu.
“Tunapofanya
mabadiliko tujiamini, Ikulu siyo ya Mangula wala Nape, nchi nyingi za
Kiafrika zimefanya mabadiliko kwa kuviangusha vyama tawala kwanini
isiwezekane Tanzania,” alisema.
Jimbo la Iramba Magharibi
Akihutubia
wananchi wa mjini Kiomboi katika Jimbo la Iramba Magharibi, Lowassa
aliahidi kuwa akichaguliwa ataanzisha benki ya bodaboda.
No comments:
Post a Comment