ASILIMIA
46 ya wananchi wameripoti kuwa sera ndio kigezo muhimu watakachokitumia
kumchagua Rais. Vigezo vingine vilivyotajwa na wananchi wengi ni
uadilifu na maadili (17%). Hakuna mtu hata mmoja aliyetaja dini au
utajiri kama kigezo muhimu cha kumchagua Rais na kigezo cha umri
kilitajwa na asilimia moja tu ya wananchi.
Matokeo
haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina
la Je, Wanajua? Takwimu kuhusu uelewa wa wapiga kura. Muhtasari
umetokana na Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye
uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za
mkononi. Matokeo yametokana na takwimu zilizokusanywa kwa wahojiwa 1,335
kutoka Tanzania Bara (Zanzibar haikuhusishwa) kati ya tarehe 12 na 26
mwezi Juni 2015.
Aidha,
wananchi wanaamini kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 utakuwa huru na wa
haki - asilimia 82 wanaamini kwamba maamuzi yao yataheshimiwa. Hata
hivyo, asilimia 18 wanafikiri kuwa viongozi walio madarakani watavunja
sheria ili washinde.
Asilimia 65 ya wananchi wanaamini kwamba mgombea mwenye sera nzuri atamshinda yule mwenye pesa nyingi.
Katika
suala la vyombo vya habari, asilimia 76 ya wananchi wanaamini kwamba
vyombo hivyo vitaripoti kwa usahihi masuala yanayohusu uchaguzi mkuu,
wakati asilimia 24 wanafikiri kuwa vyombo vya habari vitakuwa na
upendeleo kwa sababu ya motisha ya fedha.
Pamoja
na matumaini haya, wananchi wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa machafuko
na vurugu wakati wa uchaguzi mkuu. Hili ni jambo linalowatia shaka
asilimia 54 ya wananchi (Twaweza haikukusanya takwimu kuhusu nani
anaweza kuwa chanzo cha vurugu hizo). Asilimia 18 walishawahi kushuhudia
vurugu kwenye vituo vya kupigia kura wakati wa uchaguzi wa serikali za
mitaa mwishoni mwa mwaka 2014 (Sauti za Wananchi, awamu ya 30,
uliofanyika mwezi Februari-Machi 2015).
Wananchi
wanafahamu sheria muhimu zinazosimamia mwenendo wa vyama vya siasa
wakati wa kampeni. Asilimia 75 ya wananchi wanafahamu kwamba wagombea
hawaruhusiwi kugawa fedha kwa wapiga kura ili wawachague. Na asilimia 79
wanaelewa kwamba wagombea hawaruhusiwi kutoa vyakula na vinywaji katika
mikutano ya kampeni. Hata hivyo, asilimia 60 ya wananchi hawajui kuwa
wagombea vinatakiwa kutunza kumbukumbu za fedha na michango walizopokea
na jinsi zilivyotumika.
Pia,
asilimia 62 wananchi wanaijua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia
kazi zinazofanywa na tume hiyo. Hata hivyo, asilimia 51 wanaamini NEC
ina uwezo wa kusimamia uchaguzi huru na wa haki mwaka 2015. Vile vile
walipoulizwa kuhusu vipengele mahususi vya utendaji wa NEC kwenye
uchaguzi wa mwaka 2010, nusu ya wananchi waliridhishwa na utoaji elimu
kwa wapiga kura (49%), usahihi wa matokeo (54%) na mwenendo wa
wafanyakazi wa tume (52%).
Aidan
Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza alisema "Kuna mengi ya
kufurahia kuhusu uelewa wa wananchi juu ya wajibu wao wa kiraia kama
wapiga kura. Kwanza, ni dhahiri kabisa kwamba Watanzania wanalenga sera
zaidi kuliko haiba ya wagombea. Pili, wananchi wana matumaini kuwa
uchaguzi utafanyika katika hali ya uhuru na haki, ingawa wana wasiwasi
kwamba vurugu inaweza kutokea. Tatu, ni jambo la kufurahisha zaidi kuona
wananchi wakifahamu kuwa kupewa fedha, chakula au vinywaji ili
wamchague mgombea ni kosa.
Ujumbe
unaotolewa hapa kwa wagombea ni kwamba, ni lazima wajenge hoja kwa
wapiga kura zinazolenga kuboresha huduma za jamii, badala ya kujikita
kwenye tabia za watu binafsi. Wananchi wanataka mijadala makini kuhusu
sera mbadala, ili waweze kufanya maamuzi sahihi kati ya sera hizo
zinazoshindana. Hii ni changamoto mpya na inayotia hamasa kwa kila mtu
–wagombea, waandishi wa habari na wananchi wenyewe kama wapiga kura."
No comments:
Post a Comment