Mfugaji na mkulima wa kijiji cha Ibumila kata ya Kichiwa wilayani Njombe Huruma Mhapa (kulia) akielezea namna alivyo nufaika na matumizi ya biogesi kwa kutumia samadi alipotembelewa na kamati ya uhamasishaji wa matumizi ya biogesi (NBSC) pamoja wataalum kutoka Programu ya uenezi wa mitambo ya biogesi ngazi ya kaya (TDBP). Maadhimisho biogesi kitaifa yalifanyika katika Kitongoji cha Lunyunyu, Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe jana. (Picha na Friday Simbaya).
Mratibu wa Program ya Biogesi Tanzania (TDBP), Lehada Shilla.
Mwandishi wa Habari Friday Simbaya akijaribu kukoroga kinyesi cha Ng’ombe kwa ajili ya kuzalisha biogesi.

Na Friday Simbaya, NJOMBE,
Huruma Mhapa amekuwa akijaribu kumshawishi mumewe kumsaidia kukusanya kuni—hata hivyo, jitihada zake ziligonga mwamba kwa kuwa mumewe anaona kazi hiyo ni ya wanawake.
Hata hivyo, licha ya kuzongwa na majukumu mengi, Huruma, mkulima kijiji cha Ibumila, mkoa wa Njombe, Nyanda za juu kusini, alikuwa akitumia masaa mawili kila siku kukusanya kuni ili kukidhi mahitaji ya nishati nyumbani.
“Ilikuwa inachosha sana kusema ukweli, nilikuwa natembea umbali mrefu sana kukusanya kuni. Ni baridi sana hapa wakati wa usiku,” alisema.
Hata hivyo, tangu afunge mtambo wa gesi anuai unaotumia mbolea ya ng’ombe, miaka micheche iliyopita ikiwa ni sehemu ya mradi unaofadhiliwa na Programu ya Biogesi Tanzania (TDBP) kwa shirikiana chuo kikuu cha sokoine (SUA), kumetokea mapinduzi makubwa sana ya kijinsia kuhusu matumizi ya nishati kwa familia.
Alisema Mumewe Huruma, ambaye alikuwa akidharau kazi za nyumbani, sasa hivi anashiriki kuendeleza mtambo wa gesi anuai, na nyakati zingine hupika kwa gesi—akimwacha mkewe aendelee na majukumu mengine shambani.
“Mtambo huu umerahisisha sana kazi, mume wangu na mimi tunajivunia sana mradi huu,” alisema.
“Licha ya harufu nzito ya mbolea inayooza, mzee Huruma hufurahia sana kutifua mbolea ya ng’ombe na kuitumbukiza kwenye mtambo uliojengwa nje kidogo ya nyumba yao.
Mchakato huo huhusisha kuchanganya maji na mbolea na kuondoa uchafu unaoweza kudhorotesha uzalishaji wa gesi.
Mtambo huo unauwezo wa kuzalisha gesi ya kutosha kupikia na kuwasha taa za karabai, alisema, na mabaki ya mbolea hutumika kama mbolea kwenye shamba lake la mahidi.
Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya Biogesi Tanzania (TDBP) Lehada Shilla alisema kuwa biogesi imebadili mwelekeo wa familia nyingi, huku wanaume wakionekana kushiriki kikamilifu kulisha mbolea kwenye mtambo na hata kutumia gesi yenyewe na kurahisisa mzigo wa majukumu yanayowakabili wake zao—hasa kukusanya kuni.
Mratibu huyo alitoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya biogesi Tanzania ambayo alifanyika kitaifa mkoani Njombe hivi karibuni.
Pia alisema kuwa matumizi ya biogesi yamepunguza garama ya kununua nishati mbadala kama vile mafuta ya taa.
Watu wengi waishio vijijini Tanzania ambao hawana umeme, hutegemea kuni na mafuta ya taa kupikia na kuwashia.
Kwa mujibu wa serikali, ongezeko kubwa la mahitaji ya kuni limeweka shinikizo kwenye matumizi ya misitu na kuathiri vyanzo vya maji.
Shila Lehada, mratibu wa Tanzania Domestic Biogas Programme, mradi unaofadhiliwa na wahisani, amesema kuacha kutumia kuni na mafuta ya taa huwezesha familia zinazotumia gesi hifadhi hadi shilling 600000 ($375) kwa mwaka na kutoa fursa kwa wanawake na watoto kusoma na kufanya shughuli zingine za kuwaingizia kipato kwa familia.
Kwa mujibu wa wakulima, kiwango cha gesi kinacho zalishwa hukidhi mahitaji ya familia.
Mratibu huyo alitoa wito kwa Watanzania kuanza kutumia nishati mbadala ya biogesi kwa kupitia kilimo hifadhi ambacho alisema ni mkombozi kwa wakulima.
Awamu ya kwanza ya program hii ulilenga kusimkia mitambo 4000 lakini awamu hii ya pili imelenga kusimika mitambo ya biogesi kwenye kaya 27,000 ili kuweza kuhifadhi misitu.
Kaulimbiu,“biogesi kwa maisha bora na uhifadhi wa mazingira”