unnamed
Kampuni ya simu ya Tigo Tanzania itasitisha huduma zake maarufu za kutuma na kupokea fedha ya Tigo Pesa wikendi hii kwa muda wa saa 17 ili kufanya  maboresho ya huduma hiyo.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kampuni ya simu jijini Dar es Salaam inasema kuwa kusitishwa kwa huduma ya Tigo Pesa kuanzia Jumamosi usiku hadi Jumapili mchana utakuwa mwendelezo wa zoezi la uboreshaji wa huduma za kifedha za simu kwa takribani siku saba, “ kuifanya huduma ya Tigo Pesa kuwa ya kasi, imara na rahisi kupatikana.”
Huduma za Tigo Pesa zitakazo athirika kutokana na zoezi la marekebisho ni pamoja na ubadilishaji wa nenol a siri na usajili wa wateja wapya ambazo hazitakuwepo kuanzia Septemba 8 hadi 15, ubadilishaji namba ya simu kuanzia Septemba 12 hadi 15 na uboreshaji wa simu utakosekana kuanzia Septemba 6 hadi 16
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza katika kipindi chote tutakapokuwa tukipambana kukuboreshea huduma yako ya Tigo Pesa kuwa ya kasi, imara na upatikanaji rahisi,” ilisema sehemu ya habari hio. Taarifa inayofanana na hii imechapishwa kwenye vyombo vya habari pamoja na kwenye mitandao ya kijamii.
Tigo Pesa ni huduma maarufu ya kifedha kwa njia ya simu za mkononi nchini Tanzania ikiwa na zaidi ya wateja zaidi ya milioni 4 kote nchini.Huduma zinazotolewa na Tigo Pesa ni pamoja na ubadilishanaji wa fedha kati ya wateja wanaotumia mtandao wa Tigo na kati ya wale watumiao mitandao mingine, pia uhamishaji wa pesa kutoka kwenye simu kwenda Benki na kutoka Benki kwenda kwenye simu.   
Mwaka uliopita Tigo Pesa ilikuwa huduma ya kwanza ya kifedha kwa njia ya simu duniani kwa kuvuka mipaka na kuwezesha uhamishaji wa fedha iliyobadilishwa kwenda Rwanda na pia kuwa huduma ya kwanza ya kifedha kwa njia ya simu duniani kwa kutoa gawio la faida kwa wateja wake kulingana na kiasi cha fedha walichokihifadhi kwenye mfuko wao wa Tigo Pesa.