Na Timu ya Uwazi, Mkuranga
HOFU kubwa
imetanda kwenye Kijiji cha Mamndi Mkongo kilichopo Wilaya ya Mkuranga,
mkoani Pwani kufuatia Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa
kushirikiana na wale wa mkoa huo kunasa silaha nyingine za kivita
zikiwa zimefukiwa kwenye shimo msituni.
Tukio hilo la unasaji wa silaha
lilifanikiwa Agosti 29, mwaka huu katika msitu mmoja uliopo katika
kijiji hicho kilichopo umbali wa kilomita 23 kutoka mjini Mkuranga.
NI KAWAIDA YA UWAZI
Baada ya Uwazi kuzipata
taarifa za polisi kuzinasa silaha hizo lilifunga safari hadi kwenye
eneo la tukio na kushuhudia shimo ambalo silaha hizo za kivita
zilifukiwa kwa utunzaji wa siri.
Silaha za kigaidi zilizokamatwa.
MKUU WA MGAMBO ASIMULIA
Katika Mahojiano maalum na kiongozi wa
wanamgambo wa Kata ya Bup iliyopo kwenye kijiji hicho, Mussa Mohammed
Koti alisema wamekuwa wakifanya doria katika mazingira magumu na hasa
baada ya vikosi vilivyokuwepo kuondoka. Awali huku kulikuwa na vikosi
maalum vya ulinzi na usalama.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akizungumza na wandishi wa habari.
SIKU SILAHA ZILIPOKAMATWA
Koti alisema hata silaha hizo za
kivita zilizokamatwa Agosti 29, mwaka huu zilikuwa juhudi za
wanamgambo wake, polisi walikuja kujulishwa baadaye.
“Siku hiyo nakumbuka, ilikuwa mchana.
Wanamgambo waliingia msituni kwa lengo la kufanya doria. Wakafika sehemu
na kukuta mti umepandwa kwa kupinduka, juu chini, chini juu.
“Mmoja wao akashtuka na kuwaambia
wenzake kwamba, pale pana tatizo. Akasimama eneo lile na kupiga mguu
chini, ukatoka mlio kama sehemu yenye shimo kwa chini. Tulipanga kufukua
ili kujua ndani yake mna nini!”
Ngome ya magaidi hao iliyoteketezwa na Jeshi la Polisi.
“Lakini kwanza tulifanya mawasiliano na
Jehi la Polisi Mkuranga na kuwaelezea tunachotaka kukifanya, wao
wakatupa kibali cha maneno cha kufukua, maana tuliwapigia simu. Ndipo
tulipozikuta silaha hizo.”
WAIJARIBU SILAHA MOJA
“Silaha hizo zilikuwa zimechakaa kidogo
kiasi kwamba tulihisi hazifanyi kazi. Tukawapigia tena polisi, wakasema
tuijaribu bunduki moja ili kuona kama itafanya kazi au la!
“Kwa sababu wanamgambo wangu wamepitia
mafunzo ya kijeshi, mmoja alifyatua bunduki akiielekeza hewani ambapo
risasi moja ilitoka. Tukaamini zote ziko vizuri, tukawajulisha polisi
ambapo walifika na kuzichukua.”
SILAHA ZILIZOKUTWA
Uwazi lilizungumza na
kamati ya ulinzi na usalama kijijini hapo na kusema silaha zilizokutwa
ni bunduki za kivita aina ya AKA 47 (moja), SRA (mbili), RPG (mbili)
Greana (moja) na risasi 388, tambi za milipuko mikali, kitabu cha
muongozo wa kijeshi, kemikali za kutengeneza mabomu ya kutupa kwa mkono
na kitabu chenye maelekezo ya namna ya kujibadili kuwa mwanamke au
mwanaume.
MTU HUYU ANATUHUMIWAJE?
Koti alizidi kueleza kuwa, katika hali
ya kushangaza, mwanakijiji mmoja (jina linahifadhiwa kwa sasa), ambaye
wakati wa zoezi la ufukuaji hakuwepo, alirudi baada ya polisi kufika na
kuondoka na silaha hizo, akiwa na bodaboda mbili. Moja iliendeshwa na
mtu ambaye si mwenyeji kwenye macho ya wanakijiji hao akiwa amejiziba
sehemu kubwa ya uso wake.
Wawili
hao walisimamisha pikipiki nje ya nyumba ya udongo ya mwenyeji huyo na
kuchukua familia yake yenye mke na watoto. Kisha wakapanda kwa mtindo wa
‘mishikaki.’
“Sasa wakati wanaondoka, wanakijiji
waliwafuata lakini yule mwenyeji akasema anayejiona ni mwanaume kweli
awafuate jambo lililowafanya wanakijiji hao kusita.
“Ndipo wakaenda kuchoma moto nyumba
yake. Lakini ndani ya nyumba ile kulikutwa kofia aina ya kapelo ambayo
ina alama ya sime mbele. Pia kulikutwa magaloni ambayo yanasadikiwa
kubebea kemikali za kutengenezea milipuko.”
HOFU YA WANAKIJIJI
Koti aliendelea kusema kuwa, anaiomba
serikali kuwawekea ulinzi wanakijiji wake kwa kuwa licha ya wengine
kukamatwa, washukiwa hao waliotoroka wanaweza kurudi kinyemela kijijini
hapo na kuwafanyia ugaidi kama njia ya kulipa kisasi baada ya shimo lao
lenye silaha kugunduliwa.
Miongoni mwa mambo waliyoomba wanakijiji
hao ni kupatiwa silaha na pikipiki zitakazotumika na wanamgambo wao
katika kufanyia doria.
TUJIKUMBUSHE
Kwa mujibu wa chanzo chetu, awali baada
ya jeshi la polisi kunyetishiwa kuhusu uwepo wa silaha na magaidi kwenye
Wilaya ya Mkuranga, Kikosi Maalum cha Ulinzi na Usalama (task force)
kiliweka kambi katika kata hiyo kwa ajili ya kuwawinda wahalifu
wanaofanya matukio mbalimbali mijini kisha kukimbilia katika misitu hiyo
kama makazi yao ya kujificha.
Uwekaji wa kambi wa kikosi hicho kulizaa
matunda ambapo wahalifu kadhaa walikamatwa kutokana na matukio
mbalimbali ya vitendo vinavyoashiria ugaidi.
Mbali na hilo, pia kikosi hicho
kilifanikiwa kufukua begi lililokuwa na kiasi cha shilingi milioni mia
moja na hamsini (150,000,000) kitu ambacho mmoja wa wanakijiji hicho
alisema huenda pesa hizo ziliandaliwa kwa ajili ya kufanyia mafunzo
maalum ya kijeshi kwa vijana ambao wangewakusanya ili kufanikisha adhima
yao ya ugaidi.
KAMANDA KOVA AONGEA NA UWAZI
Hivi karibuni, Kamishna wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alitangaza kufukuliwa kwa silaha
zingine za kivita katika msitu huo uliopo kijijini hapo.
Kamishana Kova mbali na kutangaza
mafanikio ya ukamataji wa silaha hizo, pia alisema jeshi hilo
limefanikiwa kuwatia mabaroni watu 38 wanaotuhumiwa kwa ugaidi na
mahojiano yanaendelea kwa kasi kubwa.
“Mpaka sasa tunawashikilia watu 38
lakini sitataja majina yao kwa sababau za kiupelelezi, muda ukifika
tutaweka wazi majina na hata picha zao,” alisema Kamanda Kova.
Imeandaliwa na Haruni Sanchawa na Richard Bukos.
No comments:
Post a Comment