Gazeti la MwanaHALISI kuuzwa tena mitaani kuanzia Leo - LEKULE

Breaking

21 Sept 2015

Gazeti la MwanaHALISI kuuzwa tena mitaani kuanzia Leo



Saed Kubenea, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers LTD, inayochapisha na kusambaza gazeti la MwanaHALISI akionesha waandishi wa habari (hawapo pichana) nakala ya gazeti la MwanaHALISI litakalotoka leo.
Gazeti lililokuwa limefungiwa miaka 3 iliyopita, MwanaHALISI limechapwa na leo litakuwa mtaani nchi nzima kwa ajili ya mauzo -- inaripoti tovuti ya MwanaHALISI Online.
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Hali Halisi Publishers (HHPL) inayomiliki na kuchapisha gazeti hilo, Robert Katula nakala moja ya gazeti itauzwa kwa Sh. 1,000.
“Tumeamua kuongeza kidogo bei kwa sababu mbalimbali lakini. Kubwa zaidi ni kupanda kwa kasi kwa gharama za uchapishaji”
Wakili wa MwanaHALISI, Dk. Rugemeleza Nshala amesema gazeti liko huru kuchapishwa baada ya taratibu za kisheria baada ya uamuzi kukamilika.
“Jaji ametoa amri kwamba wahusika kutoingilia kamwe shughuli za uchapishaji wa gazeti la MwanaHALISI na shughuli za kampuni ya Hali Halisi Publishers. Zuio limetolewa dhidi ya vitendo vyovyote vya kuwanyanyasa na kuwatishia waleta maombi ikiwa ni pamoja na kutowafungia au kusimamisha uchapishaji wa gazeti la MwanaHALISI”
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea amesema kwa muda wa miaka mitatu ambao gazeti lilifugwa kampuni yake imepata hasara hivyo kusababisha shughuli za kampuni hiyo kudolola.
“Kwa muda wa miaka mitatu, mwezi mmoja na siku tano kwa makadilio ya hasara tuliyopata ni Sh. 6.8 bilioni. Kitu kinachoskitisha ni kwamba fedha hizo ni za walipa kodi wa nchi hii. Ni fedha ambazo zinapaswa kwenda kuboresha huduma za afya, elimu, kuchimba visima na kujenga barabara,”
Aidha, Mhariri wa MwanaHALISI, Jabir Idrissa ameitaka serikali kutunga sheria ambayo itawalazimisha viongozi wake wanaoisababishia hasara kulipa hasara hizo badala ya fedha za walipa kodi kutumika.
“Waziri Fenella anataka kwenda bungeni kutunga sheria wakati ameshidwa kufuata sheria. Zipo nchi ambazo hasara kama hizi anarudishiwa ofisa wa serikali aliyezisababisha”