Singida.
Mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa alishangaza wapinzani wake wakati alipofanya ziara za kushtukiza jijini Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na kupanda daladala, lakini wananchi mkoani Singida walimsaidia kutoa jibu.
Mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa alishangaza wapinzani wake wakati alipofanya ziara za kushtukiza jijini Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na kupanda daladala, lakini wananchi mkoani Singida walimsaidia kutoa jibu.
Lowassa,
Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne aliyejiondoa CCM
mwishoni mwa Julai, alikuwa akizungumza na wananchi wa Manyoni mkoani
Singida kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi ya Tambukareli.
Katika
umati wa watu waliofurika kwenye mkutano huo, kulikuwa na mwananchi
aliyebeba bango lililoandikwa “mnashangaa Lowassa kupanda daladala,
mbona hamshangai twiga kupanda ndege”.
Wakati akimaliza
hotuba yake, Lowassa aligeuka upande wa kushoto na akaliona bango hilo
likiwa limenyanyuliwa juu. Kabla ya kulisoma alicheka, halafu akalisoma
kwa sauti na kuendelea kucheka, kitu kilichowafanya wananchi waungane
naye kucheka na baadaye kushangilia.
Kabla ya kuzindua
kampeni zake kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam mwishoni
mwa mwezi Agosti, Lowassa alifanya ziara kadhaa za kustukiza
alizozielezea kuwa zililenga kufahamu matatizo ya wananchi.
Alipanda
dalkadala kutoka Gongo la Mboto kwenda Chanika wilayani Ilala,
kutembelea sokoni Tandale wilayani Kinondoni na Mbagala wilayani Temeke.
Safari zake, ambazo zilipigwa marufuku na taasisi za Serikali, zilimsha
mjadala, huku wapinzani wake wakimponda kuwa alikuwa wapi kujua
matatizo ya wananchi kabla ya kugombea urais.
Twiga
waliopandishwa ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
na kupelekwa Arabuni waliibwa kwenye moja ya mbuga za mikoa ya
kaskazini, na mtuhumiwa katika kesi hiyo alitoweka nchini na kusababisha
mdhamini wake kuhukumiwa kwenda jela.
Katika mkutano
wa jana, Lowassa pia alikabidhiwa funguo iliyoandikwa “Lowassa ni kiboko
cha makufuli mabovu”, ujumbe unaolenga kumrushia kijembe mgombea wa
CCM, Dk John Magufuli.
Kwenye mkutano huo, Lowassa
alirejea wito wake wa kuwataka wananchi wanaojitokeza kwa wingi kwenye
mikutano yake wahakikishe wanajitokeza kumpigia kura ili kuiondoa CCM
madarakani.
“Msifurike tu kwenye mikutano, bali mnipigie kura,” alisema Lowassa ambaye alikuwa akishangiliwa wakati wote.
“Nimekuja
kuwaombeni kura kila mmoja wenu anipe. Wakatalieni watakaotaka kuchukua
shahada zenu. Nataka kura zaidi ya milioni 10. Mwambieni shangazi,
mama, baba na hata mshikaji akapige kura na kazi ya pili iwe kuzilinda.”
Mwaka 2010 watu waliojitokeza kupiga kura hawakufika milioni 9, lakini
Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakadiria watu milioni 24 kujitokeza
kujiandikisha kupiga kura mwaka huu. Hadi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) haijatangaza idadi ya watu waliojiandikisha.
Akizungumzia
matatizo ya wananchi, Lowassa alisema kwa miaka 50 Serikali ya CCM
imeshindwa kuwapa huduma bora na hivyo kilichobakia ni kuiondoa.
“Hamna
maji, hampati huduma bora ya afya, kilimo bora hamna, sasa mna nini
bora,” alisema Lowassa na wananchi kumjibu, “hamna kitu tunakutaka wewe
utusaidie”.
Lowassa alisema Serikali atakayoiunda
itakuwa ya aina yake, na ambaye hataweza kuhimili vishindo vya utendaji
kazi, atakaa pembeni.
“Watu wanafurika kwenye mikutano
yangu mikoani, hii inaashiria kuwa watu wanataka mabadiliko na hayo
yanatakiwa kufanyika katika kura. Kama CCM wameshindwa kufanya
mabadiliko kwa miaka 50 wataweza sasa,” alihoji na kuamsha shangwe
kutoka kwa maelfu ya wananchi kwenye mkutano huo,
“Muungano huu (Ukawa) utaleta maajabu, wachagueni watu wetu tulete maendeleo.”
Awali,
Lowassa alimuita jukwaani mgombea ubunge wa Jimbo la Manyoni Mjini kwa
tiketi ya Chadema, Emmanuel Mpandagoya kueleza matatizo yanayowakabili
wananchi wa Manyoni.
“Manyoni tuna tatizo kubwa la
maji. Wananchi wameahidi kukupa kura, lakini ukiwa Ikulu kumbuka maji ni
kero kubwa hapa,” alisema Mpandagoya akizungumzia tatizo hilo
linalozungumzwa karibu katika mikutano yote.
“Pia tuna
tatizo la huduma za afya, ukiwa rais, mimi mbunge wako nitakupigia simu
kukukumbusha kuwa hospitali hazina dawa na baadhi ya vijiji havina
zahanati.
“Tuna tatizo kubwa la walimu wa masomo ya
sayansi na wengi wanaidai Serikali ya CCM na hawajalipwa madai yao. Hapa
Manyoni kila kona watu wanatozwa ushuru wa bidhaa, umeme umekuwa
hadithi. Hizo ndizo kero kubwa za watu wa Manyoni.”
Akieleza jinsi atakavyomaliza matatizo hayo Lowassa alisema atashughulikia tatizo la maji hadi suluhisho lipatikane.
“Nawahakikishia
wakazi wa Manyoni mkinichagua, kero ya maji itakuwa historia katika
wilaya yenu nitalishughulikia tatizo hili mpaka maji yapatikane,
haiwezekani tangu uhuru hamna maji sasa mnafaidi nini na haya ndio
maisha bora kwa kila Mtanzania?” alihoji.
Kwa mujibu wa
takwimu za Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), takriban asilimia 80 ya
watu wanaoishi mijini wanapata maji ya bomba wakati takriban asilimia 50
ya watu wanaoishi vijijini ndiyo wanaopata maji ya bomba. Inakadiriwa
kuwa idadi kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini.
Sumaye
Akizungumza
kabla ya Lowassa kupanda jukwaani, Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya
Tatu, Frederick Sumaye alisema kuwa chini ya utawala wa CCM wananchi
hawapati dawa katika hospitali, akina mama wanalala chini wakati wa
kujifungua, huku meno ya tembo na dawa za kulevya vikisafirishwa nje ya
nchi.
“Yote hayo yanatokea, hawasemi biashara hizo ni
za nani, hawa lazima waondoke,” alisema Sumaye, ambaye amekuwa akipewa
nafasi kubwa ya kuzungumza kwenye mikutano ya Lowassa.
“Tumetoka
CCM na nyinyi msiogope wanaposema kuwa nchi itaingia katika vita kama
upinzani ikiingia madarakani. Lowassa ataunda Serikali itakayowajali
wananchi, si vinginevyo,” alisema.
Sumaye aliwataka
wananchi kutokubali kutoa kadi za kupigia kura kwa kisingizio cha
kuogopa kunyanyaswa, kusisitiza kuwa safari hii watawadhibiti CCM
wasiibe kura, akisisitiza kuwa ni vigumu kwa chama hicho tawala
kushindana na nguvu ya umma.
Awali, mwanasheria mkuu wa
Chadema na mbunge wa Singida Mashariki aliyemaliza muda wake, Tundu
Lissu alisema Lowassa analipwa asilimia 80 ya mshahara wa Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, lakini yeye na wenzake wameamua kujiondoa CCM na kupoteza
stahiki zao nyingi kwa ajili ya kuwapigania wananchi.n“Sumaye na
Lowassa wanahangaika na sisi ili watusaidie kuvuka kipande kidogo
kilichobakia. Tunachotakiwa ni kushirikiana ili kuiondoa CCM
madarakani,” alisema Lissu.
Lowassa pia alifanya
mikutano Singida Mjini, Kondoa mkoani Dodoma na Ikungi ambako aliwataka
wananchi kumchagua Lissu kwa mara ya pili kuwa mbunge wa jimbo la
Singida Mashariki na kueleza jinsi ilani ya uchaguzi ya Chadema na Ukawa
itakavyokuwa na manufaa kwa wananchi kutokana na kuwajali wakulima na
wafugaji pamoja na elimu kuwa bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo
kikuu.
Mbunge huyo wa zamani wa Monduli leo ataendelea na mikutano mkoani Singida na kesho atakwenda Mkoa wa Shinyanga
No comments:
Post a Comment