Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akishiriki kwenye
matembezi yaliyotayarishwa na Vikundi vya Mazoezi vya Jimbo la Konde
hapa katika Kijiji cha Msuka, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini
Pemba.kulia
ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mzee Mberwa
Hamad Mberwa na Mkuu wa Mkoa huo Omar Khamis Othman.
Baadhi
ya wanamichezo wa vikundi vya mazoezi wa Jimbo la Konde na wale
waalikwa wa Wilaya ya Wete na Chake chake wakishiriki kwenye matembezi
ya kuimarisha vikundi hivyo yaliyoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif.
Wanamichezo
wa vikundi vya mazoezi wakifanya vitu vyao { Mchaka mchaka na
mazoezi ya viungo } baada ya kumaliza matembezi yao yaliyoongozwa na
Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na wanamichezo
mbali mbali walioshiriki matembezi na mazoezi ya viungo huko katika
Kijiji cha Msuka Jimbo la Konde Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini
Pemba.
Wanamichezo
Nchini ambao ndio kundi kubwa katika Jamii wamekumbushwa wajibu wao wa
kushiriki vyema katika kuimarisha suala la Amani ili kulifanya Taifa
kuendelea kuwa Kisiwa cha Amani Duniani hasa ikizingatiwa kwamba liko
katika kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka
huu.
Kumbusho
hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alipokuwa akizungumza na Wanamichezo tofauti waliounda Kundi la
Mazoezi Jimbo la Konde baada ya kushiriki nao matembezi yaliyoambatana
na mazoezi na kuishia katika uwanja wa Michezo wa Okapi katika Kijiji
cha Misuka Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Balozi
Seif Ali Iddi alisema kwa vile uimarishaji wa Suala la Amani unamgusa
kila mwana Jamii juhudi za ziada zinastahiki kuchukuiliwa ili
kuwawezesha Wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kawaida za kila
siku ikiwemo michezo.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na ile ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania zitahakikisha kwamba Amani ya Taifa inadumu na Wananchi
wote wanaendelea kuwa washirika wa Amani hiyo.
Alitahadharisha
kwamba tabia ya baadhi ya Watu kujaribu kuichezea amani iliyopo kwa
kujaribu kuiga mifano ya Mataifa mengine hasa yale ya jirani ni kujenga
misingi mibaya ya kusababisha migogoro itakayozua balaa na migogoro
isiyokwisha.
“
Tusipendelee kabisa kutaka kuiga wenzetu wa Mataifa jirani katika
kujaribu kuichezea amani ambayo tumekuwa wakati wote tukishuhudia Watoto
na Akina Mama wa Mataifa hayo wanavyopata madhila ikiwemo kudhalilishwa
Kijinsia baada baadhi yao kuichezea ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi wote Nchi kujenga
utamaduni wa kushiriki kwenye mazoezi kwa kujiunga na Vikundi tofauti
ili kujenga afya zao sambamba na kuimarisha Umoja na Mshikamano miongoni
mwao bila ya kujali itikadi na jinsia zao.
Alisema
mazoezi pekee yanatosha kuwa tiba kwa kuondoa maradhi madogo madogo na
pia yanasaidia kuchangia kwa asilimia kubwa akili Timamu kwa mtu
anayeshiriki mazoezi kila siku.
Katika
kuunga mkono vikundi hivyo vya mazoezi Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliahidi kusaidia seti za Jezi na Mipira kwa Timu za Mpira wa
Kandanda na zile za Pete zilizomo kwenye kundi hilo la Mazoezi.
Balozi
Seif alifahamisha kwamba Serikali Kuu kupitia Wizara inayohusika na
shughuli za Michezo itaangalia njia mbadala zitakazosaidia kutatua
baadhi ya changamoto zinazowakabili wanamichezo hao ikiwemo mashine za
kupimia afya na sare za mazoezi.
Aliwapongeza
Wanamichezo hao wa Konde kwa uamuzi wao wa kubuni wazo la kuanzisha
vikundi vya mazoezi ambavyo mbali ya kujenga afya lakini pia kwa kiasi
kikubwa vinasaidia kuimarisha Umoja na Mshikamano miongoni mwao bila ya
kujali tofauti zao za Kisiasa.
Akisoma
Risala ya Wanamichezo hao wa Vikundi vya Mazoezi wa Jimbo la Konde
Laila Ali Omar alisema vikundi hivyo vilivyojumuisha michezo tofauti
vimeamua kuendeleza michezo ili kuimarisha sanaa kama agizo la Wizara ya
Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo linavyoelekeza.
Laila
alisema Wizara inayosimamia Michezo imekuwa ikiwasisitiza wana Jamii
hasa Vijana kushiriki michezo kwa nia ya kujenga afya, kuimarisha umoja,
mshikamano unaojumuisha zaidi Vijana ili wajiepushe na vikundi
vinavyoweza kuwashawishi kujiingiza katika matendo maovu.
Alieleza
kwamba licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuasisiwa kwa
vikundi hivyo likiwemo sauala la umoja lakini bado kundi hilo kubwa
linakabiliwa na changamoto zinazosababisha kudumaza kwa malengo
waliyoyakusudia.
Laila
alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na wanamichezo hao
kukosa sare na jezi za mazoezi na kuiomba Wizara ya Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo Zanzibar kuwa karibu na vikundi hivyo kwa lengo la
kuvipatia huduma na ushauri.
Akimkaribisha
mgeni rasmi katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii
na Michezo Zanzibar Bihindi Hamad alisema Wizara hiyo wakati wote
inaendelea kushirikiana na wanamichezo wote katika kuhakikisha kwamba
Sekta ya michezo inaimarika zaidi.
Bihindi
alisema muendelezo wa Vikundi vya Michezo hasa vile vya mazoezi ni
jumla ya jitihada za Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezi
katika kuwashajiisha Vijana Nchini kushiriki kwenye michezo kwa lengo
la kuenga afya na kupunguza Maradhi.
No comments:
Post a Comment