Zitto Kabwe asema ACT Wazalendo haina hata chembe ya ufisadi, yawataka wananchi kukichagua - LEKULE

Breaking

8 Aug 2015

Zitto Kabwe asema ACT Wazalendo haina hata chembe ya ufisadi, yawataka wananchi kukichagua

ZITO
Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya Peoples Club Mjini Singida.
MGHWIRA
Mgombea Ubunge Jimbo la Singida Mjini kupitia ACT, Anna Mghwira.
MKUU MSAFARA
Mratibu wa ziara za viongozi wa ACT nchini Karama Kaila.
MKITI
Mwenyekiti wa ACT Mkoa wa Singida.
KATIBU
Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Singida akizungumza kwenye mkutano huo.

WANANCHI
Wananchi wakimsikiliza Zitto Kabwe kwenye viwanja vya Peoples Club mjni Singida. 

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo ,Zitto Zuberi Kabwe amewataka wananchi kufanya maamuzi magumu kwa kuchagua wagombea wanaoteuliwa na chama hicho katika kugombea nafasi za Ubunge na Udiwani kwa kuwa chama hicho hakina hata chembe ya ufisadi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Peoples Mjini Singida jana Zitto alisema vyama vya CCM na UKAWA sera zao ni zile zile za kifisadi kwani hazitofautiani kwani wale wanaotoka CCM na kujiunga na UKAWA ni kwenda kuendeleza ufisadi nchini.
Akimzungumzia Mgombea wa nafasi ya Urais kupitia CCM, John Pombe Magufuli alisema nae sio msafi kama ambavyo watu wanamdhania bali na yeye ana uchafu wake ndani ya Wizara ya Ujenzi anayoiongoza.
“Mimi nikiwa Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya mahesabu nilifanya ukaguzi ndani ya Wizara yake na kubaini kiasi cha fedha shilingi bilioni 200 zilizoelekezwa katika Wizara yake kati ya hizo shilingi bilioni 82 hazikujulikana zilifanya nini na wala mahesabu yake hayaonekani, mtasemaje huyo ni kiongozi msafi.” Alisema Zitto na kuongeza.
“Nafasi ya urais ni nafasi nyeti mno….kuiongoza nchi anatakiwa mtu makini.Sasa kama mtu alipewa wizara moja tu, kuiongoza na akaruhusu mabilioni kuliwa na wajanja wachache,je atamudu kuongoza wizara zote zilizopo kwa ufanisi?”,alihoji Zitto kwa mshangao na kushangiliwa kwa nguvu waliokuwa wakimsikiliza.
“Huko Ukawa nako moto unafukuta eti wanadai ufisadi hauhusiani na mtu bali ni mfumo ndio chanzo cha ufisadi, hii haiingii akilini hata kidogo, wanawageuza wananchi kuwa hawaelewi kitu jambo ambalo ni kujidanganya wenyewe.” Alisisitiza.
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo,alisema kuwa Lowassa yeye ametuhumiwa sana kwa ufisadi mbalimbali hadi akalazimka kujiuzulu wadhifa mkubwa wa waziri mkuu.
“Ukihusishwa na harufu kidogo tu ya ufisadi, hufai tena kupewa nafasi ya urais.Rais ni  kiongozi mkuu wa nchi, anapaswa awe ni mtu safi usiyekuwa na doa la aina yo yote,mwaminifu na mtu asiyekuwa mbinafsi,kwa uchache awe na sifa hizo”,alisema.
Aidha alisema chama chake kinataka kujenga siasa mpya katika nchi hii na kufuata miiko ya uongozi kwani ACT iko kwa ajili ya kulikomboa Taifa hili.
“Nimesikia jambo la ajabu sana yani mpaka leo CCM katika Jimbo la Singida Mjini bado wanagombana wenyewe kwa wenyewe kwani hawajampata mgombea wa nafasi ya Ubunge  hadi sasa.”Alisema.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti  ACT – Wazalendo Taifa, Anna Mghwira, ameteuliwa rasmi na chama hicho kupeperusha bendera ya Ubunge katika Jimbo la Singida mjini katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza kwenye mkutano huo Mghwira alisema lengo lake la kutaka kugombea nafasi hiyo ni kutoaka na mfumo mbovu wa kiuongozi ndani ya CCM katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

“CCM imetunyonya vya kutosha, tunahitaji azimio jipya, mji huu unaendeshwa kisanii, vijiji na mitaa haijapangiliwa ipasavyo huku tunasema eti ni Manispaa, huu ni usanii mtupuna kutudanganya waziwazi, mfano mdogo tu ni huu mradi wa maji kutoka Mwankoko kuja mjini, walikotoa mradi kule mwankoko hawana maji hii inashangaza sana.”Alisema .

No comments: