Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiongozana na Balozi wa Tanzania, nchini Misri, Balozi Mohammed Hamza,
wakati wakitoka kwenye Boti baada ya kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa
Mfereji mpya wa Suez Canal, kwa ajili ya meli za mizigo. Hafla hiyo
ilifanyika jana Agosti 6, 2015 jijini Ismailia. (Picha na OMR).
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
jana ameiwakilisha Tanzania katika uzinduzi wa mfereji mpya wa Suez
unaounganisha mabara ya Ulaya, Afrika na Asia. Mfereji huu mpya ambao
Misri inauita “zawadi mpya kwa Dunia” unalenga kukuza uchumi katika
usafiri wa maji na utarahisisha usafirishaji wa mizigo kwa mabara haya
matatu, huku Misri ambayo kijiografia iko jangwani ikitegemea kukuza
uchumi wake kutokana na meli zitakazopita katika mfereji huo.
Mradi
wa ujenzi wa Mfereji huu mpya umejengwa kwa mwaka mmoja licha ya
kupangwa kukamilika baada ya miaka mitatu na umetumia kiasi cha dola za
Marekani Bilioni Nane ambazo zimechangwa kwa njia ya Hisa na wananchi wa
Misri kwa kipindi kisichozidi siku tisa. Mfereji huu ambao umezinduliwa
jana, unatoa fursa kwa Meli kupita bila usumbufu tofauti na zamani
ambapo ilipaswa Meli kusimama ili kupishana lakini sasa kila upande wa
Meli utapita bila kuathiri upande mwingine.
Sherehe
hizo za aina yake zimehudhuriwa na viongozi kadhaa wa nchi mbalimbali
na kupata kuripotiwa na vyombo vyote vikubwa duniani na hivyo kutoa
picha ya kuwa Afrika inapiga hatua katika kukuza uchumi wake pamoja na
kuonesha dunia kuwa fursa mpya za maendeleo zipo Afrika.
Sherehe
hizo za aina yake zilipambwa na maonesho ya ndege za kivita
zilizotanda anga la Mfereji mpya wa Suez huku zingine zikiruka kwa kasi
na kutoa moshi ulioakisi bendera ya Misri, zingine zikipeperusha bendera
ya nchi hiyo.
Katika
tukio hilo la kuathimisha tukio hilo la kihistoria serikali ya Misri
ilitangaza kuwa siku hiyo ni ya mapumziko huku ulinzi mkali
ukiimarishwa katika miji yote mikuu ya nchi hiyo huku jiji la Cairo
walipofikia viongozi mbalimbali wa kimataifa likiwa chini ya uangalizi
wa kijeshi kwenye maoneo yote muhimu. Barabara ya kwenda eneo la
Islamelia zilikofanyika sherehe hizo ilifungwa kwa siku nzima,
walioruhusiwa kupita ni viongiozi na wageni mbalimbali waalikwa
waliotakiwa kuhudhuria tukio hilo la kihistoria.
Rais
wa Misri Abdel Fatah Sisi alisema kufunguliwa kwa Mfereji ni
uthibitisho kwamba Misri inaweza na kueleza kwamba njia hiyo itaimarisha
zaidi shughuli za usafirisha na kufungua fursa zaidi kwa mataifa
duniani.
Katika
moja ya matukio ya uzinduzi huo Rais Fatah na viongozi mbalimbali
waliohudhuria sherehe hizo walisafiri katika meli za kifahari huku
kiongozi huyo wa Misri akivalia mavazi maalumu ya kijeshi akiwa juu ya
sehemu ya uwazi wa meli hiyo pamoja na kijana mdogo mwanafunzi wa miaka
tisa aliyevalia kijeshi na kupeperusha bendera ya Misri kama ishara ya
kufunguliwa rasmi kwa mfereji huo.
Shughuli
ilimazika usiku kwa maonesho mbalimbali ya sanaa na utamaduni wa
Misri na kuhudhuriwa na viongozi na wageni wote waalikwa.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
No comments:
Post a Comment