Zahara anena baada ya kushindwa kupata kura za kutosha Tabora - LEKULE

Breaking

4 Aug 2015

Zahara anena baada ya kushindwa kupata kura za kutosha Tabora

Baada ya kura kutotosha kumfanya apite katika kura za maoni kugombea Ubunge kwa viti vya Vijana mkoani Tabora, Zahara Muhidin Issa Michuzi (pichani) amepokea matokeo kwa moyo mkunjufu na kumpongeza mshindi Irene Uwoya na kumuahidi ushirikiano katika mambo yote mema ya kuendeleza vijana mkoani humo.
Zahara ambaye sasa ataelekeza nguvu zake katika kusaka digrii ya pili ya uchumi, amesema kwamba anawashukuru wajumbe wa mkutano wa uchaguzi, baba yake, mama walezi, kaka Mkala Fundikira wa Tanzania Bloggers Network (TBN) kanda ya Magharibi na wana TBN wote wa ndani na nje ya nchi akiwemo kaka Jeff Msangi wa Canada na Mubelwa Bandio na DJ Luke wa Marekani, wanahabari wote wa makundi ya Whatsapp chini ya Francis Godwin na walimu wake pamoja  na wananchi wote kwa ujumla kwa kumpa heshima ya kumuunga mkono kwa kujitokeza kujaribu kuomba nafasi hiyo.
Amesema kushindwa kwake hakumaanishi lolote zaidi ya kwamba demokrasia imechukua mkondo wake na aliyehitajika kuendeleza mapambano amepita na yeye hana kinyongo naye na ataendelea kuutumikia mkoa wa Tabora  katika nafasi yake ya mtu ambaye si kiongozi.
Zahara ametoa mwito kwa wagombea wa nafasi zote kwamba kushindwa ni moja ya matokeo katika ushindani wowote hivyo ipo haja ya kujenga utamaduni wa kukubali matokeo bila ya hasira ama kinyongo kwani dunia i duara, na kwamba mlango mmoja ukifungwa kuna mwingine utafunguka.
Amesema hana mpango wa kuhama CCM ambayo anaiamini kuwa ni chama ambacho kitaenzi na kutunza hadhi na mustakabali wa Taifa la Tanzania kuliko chama chochote.
“Kushindwa kwangu kupata kura za kutosha sio mwisho wa dunia. Nina imani kwamba wapiga kura walijua wanachokifanya. Mimi ni nani kuwaoneshea kidole?  Maisha yaendelee kama kawaida na Mola awajaalie wote kwa yote” alisema.




No comments: