Yemba ateuliwa kuwania urais ADC - LEKULE

Breaking

6 Aug 2015

Yemba ateuliwa kuwania urais ADC


Dar es Salaam.
Mkutano mkuu wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) umemteua Chifu Lutalosa Yemba kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenyekiti wa chama hicho, Said Miraaj Abdulla kuwa mgombea mwenza.
Mkutano huo pia ulimpitisha Hamad Rashid Mohamed kuwania urais wa Zanzibar na kuahidi iwapo hatatekeleza ahadi zake kwa wananchi, akimaliza miaka mitano afungwe jela miezi sita kama adhabu ya kudanganya.
Kuteuliwa kwa Chifu Yemba kuwania urais wa Tanzania kunafanya wagombea wa nafasi hiyo ya juu katika siasa nchini kufikia saba baada ya Chadema kumteua Edward Lowassa mapema wiki hii na Chauma kumteua Hashim Rungwe.
Wagombea wa vyama vingine ambao walishapitishwa na tayari wamechukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni Dk John Pombe Magufuli wa CCM, Fahmi Dovutwa (UDPD), Mchungaji Christopher Mtikila (DP) na Maxmillian Lyimo (TLP).
Wagombea hao wa ADC watachukua fomu za kuwania urais kutoka NEC kesho baada ya kuwatambulishwa kwa wanachama kwenye viwanja vya Buguruni Sheli jijini Dar es Salaam kabla ya kuendelea na ratiba za mikoani.
“Msukumo ulionifanya nigombee urais ni nia ya kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kuwasaidia kufikia malengo yao,” alisema Chifu Yemba wakati akihutubia baada ya kupitishwa na mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam.
Alisema ametafakari kwa kina na akaona anaweza kufanya hayo kwa kushirikiana na wananchi badala ya kuamua yeye kama mtawala.
“Sitaki kuwa mtawala, nataka kuwa kiongozi ili kuhakikisha malengo ya wapenda mabadiliko ya kitaifa na yao binafsi yanatimia na hilo ninaliweza,” alisema Yemba.
Yemba alisema hadi sasa hakuna chama chenye nia ya dhati kumkomboa mwananchi wa kawaida badala yake vinajiandalia jinsi ya kutafuna fedha zao pindi vitakapoingia madarakani.
Alisema ADC ina sera na ilani ya uchaguzi inayoendana na maisha halisi ya Mtanzania, “Kwa bahati mbaya vyama vingi vinachanganya sera na ilani au havina hivyo vitu viwili, lakini ilani ya ADC inaendana na maisha halisi ya Watanzania na wanayotaka yafanyiwe kazi au yatatuliwe,” alisema Chifu Yemba.
Alieleza kuwa hadi sasa hajaona upinzani hasa kutoka vyama vikubwa, akisema haoni tofauti ya wanaogombea uongozi kwani ni hao hao walikuwa upande mmoja wameamua kuhamia mwingine.
Alifafanua kuwa chama tawala kimeshapoteza dira hakijulikani kama cha kibepari au kijamaa huku kinachowafuatia kwa karibu kilikuwa cha kibepari, lakini sasa kimejichanganya na kuwa na mtazamo wote kibepari na kijamaa.
“Hivyo vyama vinavyoonekana na kusemwa ni vikubwa naweza kusema sioni upinzani kutoka kwao iwapo wananchi watapima na kutambua wanataka nini ili kuleta mabadiliko ya kweli. Tupeni ADC ridhaa tuonyeshe tunachotaka kuwafanyia kulingana na ilani na sera zetu, ”alisema.

Nifungwe jela

Chifu Yemba haoni upinzani kutoka vyama alivyosema ni vikubwa, lakini mgombea Hamad Rashid, ambaye amekuwa kwenye siasa tangu mwaka 1977 alitaka afungwe jela miezi sita iwapo hatatimiza ahadi zake kwa wananchi atakapochaguliwa na kumaliza kipindi cha miaka mitano.
Alisema adhabu hiyo siyo kwa kosa la kuiba fedha au kufanya ufisadi wa aina yoyote, bali hata akishindwa kutekeleza kitu kimoja katika aliyoahidi, atastahili kufungwa kwa kuwa ni uongo.
Alisema kuwa aliwahi kushindana na kaka yake, Said Rashid Mohamed kwenye uchaguzi wa mwaka 1995 wakati akiwa CUF na kwamba ndugu huyo aliyekuwa CCM alimshinda, lakini hakukutokea ugomvi wala familia kugawanyika.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, anataka kuondoa dhana kuwa Zanzibar kuna vyama viwili tu, CUF na CCM, kwa kuwaonyesha Wazanzibar namna wanavyoweza kunufaika na rasilimali zilizopo nchini mwao badala ya kung’ang’ania itikadi za vyama visivyowasaidia.
Aliyataja maeneo ambayo yanaweza kuwaondolea wananchi umasikini kuwa ni uvuvi, kilimo na utalii.

Kuhama chama siyo dhambi

Alisema anataka pia kupiga vita siasa chafu na kuwachukulia waliohama vyama kuwa wametenda dhambi, wakati ukweli ni kwamba kufanya hivyo siyo dhambi kwa kuwa chama siyo dini.
Alisema siasa siyo ugomvi bali ni kusukuma mbele maendeleo kwa kuwapiga vita wale wote wasiotekeleza ahadi wakiwa kwenye nafasi za uongozi, hivyo wanaweza kuelewana, kusikilizana hata wakiwa nje ya vyama.
“Nilikuwa makamu mwenyekiti wa kamati ya usuluhishi makamu mwingine akiwa Phillip Mangula na mwenyekiti akiwa Kingunge Ngombale Mwilu. Nafahamu madhara ya kupotoshana kisiasa,” alisema akirejea mazungumzo ya kutafuta maridhiano baina ya vyama vya CCM na CUF yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK).

Hali ya kisiasa

Kada huyo wa zamani wa CCM alisema kuwa uchaguzi wa mwaka huu umeonyesha ni kwa namna gani demokrasia imekua kutokana na watu wengi kujitokeza bila woga kuwania uongozi.
Alisema hapo awali wananchi waliingia woga waliposikia watu wanagombea uongozi kwenye vyama vingine na kuamini kuwa hawangeshinda, lakini mwaka huu hofu hiyo haipo.
Alisema pamoja na mafanikio hayo, changamoto iliyopo ni fedha kutawala uchaguzi na kuna kila dalili kuwa washindi watapatikana kwa kutumia fedha badala ya kujivunia kukua kwa demokrasia.
“Ninawaomba Watanzania watambue thamani yao na ya kura yao kwa kutokubali kununuliwa,” alisema. “Wanatakiwa kusimama katika haki, wakiwa makini kuwasikiliza wagombea, sera za vyama vyao ili kujihakikisha usalama wa kutekelezwa kile wanachoambiwa na wagombea.”
Alitoa wito kwa NEC kuwa huru katika utendaji wake ili kuondoa mivutano isiyo ya lazima, huku akikemea kauli za viongozi zinazoashiria kuwapo kwa uvunjifu wa amani. Alisema ADC itakubaliana na matokeo iwapo NEC itaendesha uchaguzi kwa haki na kwa uhuru, lakini akaongeza kuwa kama hawataridhishwa na chochote katika uchaguzi watadai haki kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.

Ilani, sera, miiko ya uongozi

Lakini mwenyekiti wa chama hicho, Abdulla, ambaye ndiye mgombea mwenza, alijikita zaidi katika kueleza mikakati na misingi ya chama hicho.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Abdulla ambaye pia ni mwenyekiti wa ADC alisema kuwa akiwa makamu wa rais atasimamia misingi ya haki, ikiwamo yale yalioanishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya chama chake.
Alisema licha ya kuwapo na shaka ya wananchi wengi kuchagua viongozi kwa mazoea, kujuana, uvyama, maslahi binafsi au fedha, ADC imejipanga kukabiliana na yote hayo ili iweze kutambulika na kuleta mabadiliko ya kweli.
Alifafanua kuwa lengo kuu la ADC ni kuingia katika ushindani wa kweli na vyama ambavyo baadhi yake vina sifa ya kutawala kwa nguvu na kutumia fedha.
“Tunaamini katika uongozi wa haki, na siyo lazima kiongozi mzuri atoke katika vyama vikubwa bali ni yule ambaye anaweza kutimiza ndoto za waliomchagua tu,” alisema Abdulla.
Mgombea huyo mwenza aliwaahidi wananchi wa Bara na Visiwani kuwa ADC itatoa ushindani wa hakika, sera na hoja zenye tija kwa Taifa katika uchaguzi mkuu ujao ikiwa ni pamoja na kuleta mapinduzi ya fikra kwa wananchi ili waache kubweteka na kuamua hatma yao wenyewe.

Ilani ya ADC

Abdulla alitaja baadhi ya mambo muhimu yaliyomo kwenye ilani ya chama kuwa ni pamoja na kutambua mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na katiba za pande hizo mbili za Muungano.
Alisema wanatimiza fungamano lao na utii kwa nchi kutokana na Katiba na Sheria za nchi zilizotungwa na vyombo vyenye mamlaka, huku wakidhamiria kuweka misingi ya kuwawezesha wananchi kupata maendeleo na kuepukana na umasikini, ukandamizwaji, matatizo ya kiuchumi na kijamii.
Alieleza dhamira yao kuwa ni kutandaza misingi yenye mizania ya usawa katika utawala wa sheria, usalama, haki za binadamu, uhuru wa aina zote kulingana na matakwa ya misingi ya utu inayozingatia mila, desturi na silka za Kitanzania, kama vile kudumisha uhuru wa kukusanyika, kutoa mawazo, kufanya harakati za kisiasa, maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni.
Alisema ADC haiamini katika Taifa lisilokuwa huru, hivyo watajenga Taifa linaloheshimu demokrasia, lililo huru, imara, lenye amani, utulivu, nguvu ya kiusalama, watu wenye afya na walioelimika, lenye upendo kwa wote bila kubagua wenye nacho na wasiouwa nacho.
“Anayetakiwa kunufaika na maendeleo ya nchi hii ni Mtanzania kwanza, kama mgeni atalazimika kupata fursa hiyo sharti ashirikiane na Serikali au wenyeji wa eneo husika,” alisema. “Hatutakubali wageni wale matunda ya nchi huku wenyeji wakibaki wanahangaika, hilo ADC hawatalifumbia macho.”

Misingi ya uongozi ya ADC

Abdulla aliitaja misingi ya uongozi ya chama hicho kuwa ni pamoja na kuamini na kumtii Mungu, utii wa Katiba na sheria za nchi, utu, huruma, upendo, kuheshimiana, kujiamini, kujituma, kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika ipasavyo na kwa wakati.


No comments: