Chenge kuhojiwa na Baraza la Maadili leo - LEKULE

Breaking

6 Aug 2015

Chenge kuhojiwa na Baraza la Maadili leo



Dar es Salaam.
Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge leo atapandishwa kizimbani kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuhusika katika kashfa ya ‘kuchota’ fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Chenge ni mmoja wa viongozi waliopata mgawo wa fedha kutoka kwenye akaunti hiyo jambo ambalo ni ukiukaji wa sheria namba 13 ya maadili ya viongozi wa umma.
Watuhumiwa wengine ni aliyekuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mkurugenzi wa sheria, Wizara ya Ardhi, Rugonzibwa Mujunangoma na Mnikulu wa Ikulu, Shaaban Gurumo. Chenge alifungua kesi Mahakama Kuu akipinga kuhojiwa dhidi ya tuhuma za kukiuka maadili ya viongozi baada ya kupokea Sh1.6 bilioni kutoka kwa mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemalira, fedha ambazo zinahusishwa na akaunti hiyo.
Katika vikao vilivyopita, Chenge alilitaka baraza kutojadili shauri lake kwa sababu kesi yake ya msingi kuhusu fedha za escrow ilikuwa imefunguliwa Mahakama Kuu.
Alisisitiza kuwa kuendelea kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama.
Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma lilisitisha kumhoji mtuhumiwa huyo ili kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu.
Hata hivyo, Mahakama Kuu ilitupilia mbali shauri lake la kuzuia kujadiliwa na kutoa nafasi kwa Baraza la Maadili kuendelea na kazi yake kuchunguza uvunjifu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Taarifa ya baraza iliyotolewa kabla ya kuanza kusikiliza mashauri hayo, ilibainisha kuwa vikao vyake vinafanyika baada ya Mahakama kutupilia mbali shauri la kikatiba lililofunguliwa kuzuia taasisi za Serikali pamoja na baraza hilo kuendelea kufanya uchunguzi wa aina yoyote unaohusiana na sakata la escrow.
Baadhi ya viongozi wa umma wanatuhumiwa kuhusika katika sakata hilo kwa sababu walipokea fedha katika akaunti zao kupitia Benki ya Mkombozi.
Kashfa ya escrow ilisababisha aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na waziri wa Ardhi, Profesa Tibaijuka kuondolewa katika nyadhifa zao.


No comments: