Watu
watatu (wanawake 2, mwanaume 1) wamefariki dunia na wengine 34 wamelazwa
katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na hospitali ya Mburahati
jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kipindupindu.
Hospitali ya Sinza Palestina imeripotiwa kuwa na wagonjwa walio na dalili za ugonjwa huo zaidi ya 50.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Bw. Paul
Makonda amezitaja Kata zilizoathirika na ugonjwa huo kuwa ni
Kijitonyama, Kimara, Manzese, Tandale, Saranga, Makumbusho na
Mwananyamala.
Mkuu wa
mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, amesema kuna ripoti ya
wagonjwa waliolazwa 71 hadi sasa, na kwamba Wilaya ya Ilala na Temeke
bado hazijakumbwa na ugonjwa huo.
Akizungumza
na wanahabari Jijini Dar es Salaam, Mganga Mkuu wa Minispaa hiyo, Dk.
Aziz Msuya, amesema kuwa mgonjwa wa kwanza aligunduliwa katika maeneo ya
Kijitonyama kwa Ally Maua na kufia nyumbani kwake katika eneo hilo na
kuambukiza ndugu zake wawili ambao walikufa wakati wanapelekwa
Hospitali.
Dk. Msuya
amesema kumetayarishwa kambi za muda katika Hospitali za Kijitonyama,
Mwananyamala na Sinza Palestina pamoja na kambi kuu iliyopo katika
Hositali ya Mburahati. Amewataka wananchi wa Jiji hilo kuchukua
tahadhari kwa kuweka mazingira safi kunywa maji yaliyochemshwa na
kujiepusha kula vyakula vilivyopikwa katika mazingira yasiyo safi na
salama.
“Ukipata
huu ugonjwa tutakupa dawa lakini kwa sasa tumetoa dawa katika maeneo
yale ambayo tumeona yameathirika zaidi ambayo ni Manzese na Kijitonyama.
Tumeshazipa dawa kaya zile ambazo tunazitilia mashaka kwamba
zinawezikawa zimepata maambukizi, na wale waliopo katika maeneo mengine
ambayo sio maeneo hayo niliyokutajia hapo awali, wanapoona hizo dalili
za kutapika na kuhara basi wafanye haraka kukimbia Hospitali.”
Mwakilishi
wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dk. Rufaro Chatora, katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari amethibitisha kupokea taarifa kutoka
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiijulisha WHO kuwepo kwa ugonjwa
huo, na kwamba ugonjwa huo uliibuka tangu Agosti, 15, 2015.
Hata
hivyo, ametaja maeneo yaliyobainika kuwa na wagonjwa hadi sasa kuwa ni
Tandale, Kijitonyama, Saranga, Kimara, Manzese, Makumbusho na
Mwananyamala.
Timu ya
wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inafanya uchunguzi
wa kina katika Wilaya ya Kinondoni ambayo ndiyo imeshambuliwa kwa sasa
na ugonjwa huo kwa kasi ambapo pia timu hiyo itaendelea kutoa njia za
kujikinga.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Musa Nati, amesema watu
wengine ambao hadi sasa idadi yao haijathibitishwa wamethibitika kuugua
kipindupindu na wamelazwa katika hospitali hizo za manispaa hiyo.
Ameeleza kuwa wodi mbili zimetengwa katika hospitali ya Mwananyamala kwa
ajili ya wagonjwa wenye dalili hizo.
Mathalani, amesema wameanza kuchukua tahadhari kwa kupuliza dawa katika maeneo yaliyoripotiwa kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
Historia ya kipindupindu Dar es Salaam
Ugonjwa
wa kipindupindu umekuwa ukiutesa mara kwa mara mkoa wa Dar es Salaam
kila mwaka licha ya jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na
serikali licha ya kila mwaka ugonjwa huo ambao umekuwa ukilipuka na
kuwaathiri watu wengi na wakati mwingine kupoteza maisha.
Mamlaka
za serikali zimekuwa zimekaririwa mara kadhaa na vyombo vya haabri kuwa
zinachukua hatua kwa kuweka tahadhari mbalimbali kwa lengo la kudhibiti
kipindupindu. Miongoni mwa hatua hizo ni kuzuia mikusanyiko ya watu kama
sherehe, misiba na unywaji wa pombe za kienyeji.
Hata
hivyo, pamoja na hatua hizo na nyingine nyingi kumekuwepo na hatua ya
upigaji marufuku uuzaji wa vyakula katika maeneo yasiyoruhusiwa hali
ambayo inatajwa kusababisha ugonjwa huo wa kipindupindu kuendelea
kuutesa mkoa huo kila mwaka.
Kufuatia
hali hiyo, Halmashauri ya Jiji hilo, imelazimika kufungua kambi maalumu
za kuhudumia walioathirika na ugonjwa huo, katika Manispaa za Temeke,
Kinondoni na Ilala ili wanaporipotiwa wagonjwa wapatiwe tiba kwa haraka.
No comments:
Post a Comment