Siku 64 za mtifuano - LEKULE

Breaking

13 Aug 2015

Siku 64 za mtifuano


Dar es Salaam. 
Zikiwa zimesalia siku tisa kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu, kuna dalili za wazi kuwa vyama vilivyosimamisha wagombea urais vinakabiliwa na kazi ngumu ya kuwafikia wananchi kutokana na muda mfupi uliopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa mujibu wa ratiba ya NEC iliyotolewa Juni mwaka huu, wagombea wote wa nafasi za urais, ubunge na udiwani watalazimika kutumia siku 64 kukamilisha kampeni zao kuanzia Agosti 22 hadi Oktoba 24.
Kwa nchi yenye eneo la kilomita 945,087 za mraba, barabara nyingi mbovu hasa kwenye maeneo ya vijijini na umbali mrefu kutoka wilaya moja hadi nyingine, jimbo na jimbo, muda huo, wa siku zisizopungua 60 zinazotakiwa kisheria, utakuwa mwiba mchungu kwa wagombea wa urais ambao watataka kuifikia sehemu kubwa ya nchi kunadi ilani na sera za vyama vyao na kuwapigia debe wagombea wao wa ubunge na udiwani.
Ukilinganisha na muda wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2010, muda huo ni pungufu kwa siku tano.
Ili kuzifikia kata zote 3,957 za uchaguzi, majimbo 265 au wilaya zote 135, ukiacha wilaya mpya zilizoongezwa na Rais Kikwete mwezi uliopita, wagombea wote watatakiwa wavishinde vikwazo hivyo vya ubovu wa barabara, rasilimali fedha na muda wa kupumzika kutokana na kuhitajika kusafiri usiku na mchana kutumiza azma zao.
Kimahesabu, iwapo watapanga kupita kila kata, watahitajika kuhutubia kata 62 ndani ya saa 12 zinazoruhusiwa na NEC kufanya kampeni kwa siku, hali ambayo itaweka rehani afya zao na kuathiri ufanisi wa kampeni zao.
NEC imebainisha katika tangazo lake la hivi karibuni kuwa Tanzania ina jumla ya kata 3,957 ambazo zitashiriki uchaguzi mwaka huu.
Hata kama wagombea hao wa urais na wagombea wenza watajipanga kufika makao makuu pekee katika kila jimbo nchini, kwa aina yoyote ile ya usafiri, watahitaji kutembelea wastani wa majimbo manne kila siku.
Hata hivyo, ahueni kidogo inaweza kutokea iwapo wagombea hao wataamua kuuza sera zao kwa kuigawa nchi katika wilaya na hivyo kutakiwa kuzunguka wilaya mbili kila siku ili kukamilisha zaidi ya wilaya 133 zilizopo.
Katibu mkuu wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo aliliambia gazeti hili jana kuwa kuna ugumu katika kampeni za mwaka huu, lakini wamejipanga kwa kutumia usafiri wa ardhini na angani kuwafikia wananchi wengi zaidi.
“Kwa mwezi mmoja na nusu tutatumia magari na muda uliobakia mgombea urais na mgombea mwenza wataanza kutumia helikopta. Safari yetu ya kampeni itaanzia mkoani Tanga Agosti 30 na bila shaka tutafanikiwa kwa asilimia kubwa,” alisema Doyo.
Wakati ADC wakijipanga kutumia anga kukimbizana na muda, Chama cha Kijamii (CCK) kilichomsimamisha Dk Godfrey Malisa na mgombea mweza Ali Said Juma, kimesema kitatumia barabara “mpaka kieleweke”.
Mwenyekiti wa CCK, Constatine Akitanda alisema pamoja na siku za kampeni kuwa chache, watajitahidi kuhakikisha kila sehemu ya nchi wanafika kumnadi mgombea wao wa urais.
“Sisi tutashambulia ardhini tu hakuna sababu ya kwenda angani kwa sababu mambo yote ya wananchi yapo chini. Tumeshagawana timu, tutapita nchi nzima hatutaacha jiwe ambalo halijageuzwa,” alisema Akitanda.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Uchaguzi wa Chadema, Benson Kigaila alisema siku 64 zitawatosha wagombea wa ubunge na udiwani lakini si kwa urais.
“Hata useme unafanya kampeni katika majimbo 265 yaliyopo na kupanga kuzunguka majimbo manne kwa siku, hutayamaliza,” alisema Kigaila huku akijigamba kuwa “watamchinja ng’ombe kama alivyolala”.
“Lakini kwa sababu muda umeshapangwa, sisi tutakabiliana nao hivyo hivyo hata kama ni siku 10. Tutatumia magari na chopa kama ilivyo jadi yetu,” alisema.
Hata wakati vyama vya siasa vikihofia muda kuwa mfupi, mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alitetea kuwa muda huo ni halali na zipo ndani ya wigo wa sheria unaotaka kampeni zifanyike kwa siku 60.

“Hakuna cha upungufu wa siku hapo, tulishafanya hesabu za kina ndiyo maana ilitolewa ratiba hiyo. Jaribu kuangalia wanamalizia Agosti, wana mwezi mzima wa Septemba na Oktoba, ni nyingi sana hizo na zipo kisheria japo wengine huwa wanalalamika kuwa wanakuwa ‘exhausted’ (wanapata uchovu),” alisema Lubuva.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Respicius Damian alisema kutokana na mwamko wa kisiasa na ushindani uliopo baina ya vyama, siku hizo ni chache na hivyo zitaathiri vyama na wapiga kura.
Alisema tatizo la ubovu wa miundombinu mara nyingi huchangia mikutano ya kampeni ichelewe kuanza katika maeneo mengi licha ya muda wa kumaliza mikutano hiyo kubaki pale pale.
“Uchaguzi huu unahusisha vigogo wakuu wawili (mgombea wa urais CCM, Dk John Magufuli) na mgombea wa Ukawa kupitia Chadema (Edward Lowassa) ambao wanafahamika, lakini wangehitaji muda zaidi kuzungumza na wananchi.
“Ratiba hiyo inabana kwa sababu kutakuwa na maswali mengi sana kwa wagombea na iwapo wanaojinadi hawatapata muda wa kutosha kujieleza, kuna kila dalili za kuibuka kiwango kikubwa cha propaganda,” alisema Damian.
Pamoja na wanasiasa na wataalamu kueleza kuwepo kwa mikimiki ya kampeni kutokana na uchache wa siku, mkurugenzi mtendaji wa asasi ya kiraia ya Concern For Development Initiative Africa (Fordia), Buberwa Kaiza alisema siku 64 ni nyingi iwapo vyama vitajipanga vizuri.
Buberwa, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uongozi, alisema kama vyama vingejitanua mikoani na kutumia njia nyingine za mawasiliano kama vyombo vya habari, hakuna haja ya wagombea wa urais kufika kila eneo la nchi.
“Jambo la msingi ni kufikisha ujumbe kwa wananchi, waelewe sera na kujibiwa maswali yao yote na siyo wingi wa siku. Mwezi mmoja unatosha kabisa, tatizo vyama havina mipango hata kama wakipatiwa miezi minne haitavitosha,” alisema Kaiza.

No comments: