Moshi.
Sasa ni dhahiri kuwa mazishi ya mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo yanayofanyika leo yatamkutanisha kwa mara ya kwanza, Rais Jakaya Kikwete na Edward Lowassa tangu waziri huyo mkuu wa zamani ajiondoe CCM na kujiunga na Chadema.
Ingawa ratiba ya JK haikuwekwa wazi, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga alisema Rais atawasili wilayani Mwanga leo mchana.
“Tunatarajia Rais atawasili wilayani kwetu mchana na tunatarajia ibada itaanza saa 7:00 mchana. Shughuli za kuaga mwili hapa Usangi zitaanza saa 3:00 asubuhi katika Usharika wa Kivindu,” alisema.
Habari zaidi kutoka kwa mmoja wa wanafamilia zinasema kuwa Rais atawasili kwa helikopta. Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, anatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro leo saa 2:00 asubuhi na kwenda moja kwa moja na msafara wa magari hadi Usangi wilayani Mwanga kwa ajili ya mazishi hayo.
Vigogo wengine waliothibitisha kuhudhuria mazishi hayo ni pamoja na waziri mkuu mstaafu na baba wa Jimbo la Mwanga, Cleopa Msuya, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro na Lowassa.
Kwa kawaida shughuli za mazishi huwa hazichukui mwelekeo wa kisiasa na ni kawaida mahasimu kukutana, kuongea na kusalimiana, lakini tukio la leo litakuwa likifuatiliwa kutokana na matukio ya hivi karibuni ya wawili hao ambao hawakukutana “barabarani”.
Vigogo hao wanakutana, ikiwa ni siku nne tu baada ya Lowassa kumtaja hadharani Kikwete kuwa ameharibu uchumi wa nchi kwa kushindwa kusimamia mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali ambazo ni muhimu kwa wananchi.
Akimpokea mgombea urais wa CCM, John Mafuguli baada ya kuchukua fomu za urais kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rais Kikwete, bila kumtaja Lowassa, alisema: “Mtoto wako akikukosoa na kuungana na maadui, unamshughulikia pamoja na maadui hao ili kumwonyesha kuwa wewe ni baba yake.”
Kutofautiana kwao kulianza mara baada ya Kamati Kuu ya CCM kumuengua Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Akiwa mwenyekiti wa CCM, Julai 11 mjini Dodoma, Kikwete aliongoza kikao cha Kamati Kuu kilichoengua jina la Lowassa, ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho kutokana na kuwa na uzoefu na kukubalika kwa wanachama kulinganisha na makada wengine 38.
Kuenguliwa kwa jina lake kulisababisha rabsha kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, ingawa baada ya majadiliano wajumbe walikubaliana kuendelea na mchakato.
Baadaye Lowassa alitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema ambayo ilimpa fursa nyingine ya kuendelea na ndoto yake ya kutaka kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Tangu wakati huo, wanasiasa hao wawili, ambao waliwahi kupachikwa jina la Boys ll Men kutokana na kwenda pamoja kuchukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CCM mwaka 1995, hawajawahi kukutana hadharani.
Jina la Lowassa lilikatwa pamoja na makada wengine 32 katika hatua za awali, lakini, kwa mara ya kwanza, wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM walizungumza hadharani kuwa katiba ilikiukwa, wakisema si majina yote yaliyowasilishwa kwenye kikao hicho.
Tamko la wajumbe hao lilifuatiwa na kitendo cha wajumbe wa Halmashauri Kuu kuimba wimbo wa kuwa na imani na Lowassa wakionyesha kupinga uamuzi wa Kamati Kuu, wakati Rais Kikwete na wageni wengine wakiingia kikaoni, tukio ambalo mwenyekiti huyo wa CCM alilielezea kuwa “haijawahi kutokea”.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli, ambaye pia anatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo, ndiye aliyepitishwa kugombea urais baada ya kuwashinda makada wengine wanne waliopitishwa na Kamati Kuu ambao ni Asha Rose Migiro, Amina Salum Ali, January Makamba na Bernard Membe.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoani Kilimanjaro, Peter David amesema kifo cha Kisumo ni pigo kwa CCM hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
“Ni mtu asiyeogopa jambo lolote na hapendi uonevu kwa mtu yeyote wala dhuluma,” alisema David.
Kada huyo alitoa kauli hiyo jana kwenye ibada iliyofanyika Usharika wa Moshi Mjini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kulipofanyika ibada maalumu la marafiki kuaga mwili wa Kisumo.
Askofu Martin Shao, ambaye alikuwa akiongoza Dayosisi ya Kaskazini, alisema Kisumo alikuwa ni mcha Mungu.
No comments:
Post a Comment