2
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kuzindua benki ya Maendeleo ya Kilimo.
3
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza wakati wa uzinduzi wa benki ya Maendeleo ya Kilimo.
1
Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, Thomas Samkyi akizungumza wakati wa uzinduzi wa benki ya wakulima Tanzania (TADB), uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu JK Nyerere.
5
Mwenyekiti wa Bodi ya benki ya Maendeleo ya Kilimo, Bi Rosebud Kurwijila, akizungumza wakati wa uzinduzi wa benki.
4
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akifuatilia uzinduzi wa benki ya Maendeleo ya Kilimo, kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo Bi Rosebud Kurwijila, akifuatiwa na Mkurugenzi Mkuu wa benki, bwana Thomas Samkyi, na kutoka kushoto ni Waziri wa Kilimo, Stephen Wasira akifuatiwa na Waziri wa Fedha, Bi Saada Mkuya.
6
Wageni waalikwa wakifuatilia uzinduzi wa benki ya Maendeleo ya Kilimo.
Rais Jakaya Kikwete leo amezindua benki ya kwanza ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, ambayo inalenga kuanzisha mtizamo mpya wa kukiendeleza kilimo kupitia kushirikisha wadau mbali mbali, kuangalia kila mnyororo wa thamani kwa ukamilifu wake, pamoja na kuwa na ubunifu katika kuchangia kifedha kwenye miradi ya muda mrefu, ya kati na muda mfupi kwenye sekta ya kilimo. Benki hiyo inatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa sekta ya kilimo ambayo imeajiri zaidi ya aslimia 70 ya Watanzania.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais Kikwete amesema changamoto zinazowakabili wakulima nchini ndizo zilizosababisha serikali yake kuanzisha benki hii ili kuwakomboa wakulima kwenye umaskini ili waweze kuzalisha kibiashara na sio kwa kwa kujikimu.
‘Awali huduma za kifedha na mikopo kwa wakulima hazikuwepo kabisa na hivyo kupelekea tija kwenye kilimo kuwa chini, uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo nao ukawa chini ya viwango vya Afrika na hata dunia, hivyo ya uzinduzi wa benki hii unafungua ukurasa mpya wa mapinduzi ya kilimo nchini’ alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia aliwaasa wakulima kutumia vyema fursa ya uanzishwaji wa benki hii akisema kwa sasa kilimo kinachangia asilimia 25 ya pato la taifa, huku asilimia 35 ya bidhaa tunazouza nje ni za kilimo.
‘Serikali imetoa mtaji wa kuanzisha benki wa jumla ya shilingi bilioni 60, na tunatarajia kuingia hati fungani ili kuiongezea benki mtaji kwa jumla ya shilingi bilioni 800’ anasisitiza Waziri wa Fedha, Saada Mkuya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa benki, Bwana Thomas Samkyi, alisema dhumuni kuu la uanzishaji wa benki hiyo ni kuboresha tija katika uzalishaji kwenye sekta ya kilimo kwa kuunganisha nguvu za wadau mbalimbali ili kuwezesha uendelezaji wa miundombinu ya kilimo kama miradi ya umwagiliaji, usafirishaji, uhifadhi, mindombinu ya masoko, n.k. ambayo inachangia maendeleo ya sekta ya kilimo.
‘Uanzishwaji wa benki hii unalenga kuziba mianya mikubwa ya ukopeshaji kwenye kilimo ambayo inaachwa na benki za biashara, ili kuchochea kukua kwa sekta ya kilimo, kwa kutoa mikopo na huduma nyingizezo za uwezeshaji wa kilimo kwa wakulima, ambao wengi wao hawana uwezo wa kupata huduma za kibenki’ alisema Bw. Samkyi.
Akieleza zaidi kuhusu uanzishwaji wa benki hiyo, Bwana Samkyi alisema Benki ya Wakulima itakuwa msitari wa mbele katika kusukuma shughuli za kilimo pamoja na kuchagiza benki na taasisi nyingine za kifedha kushiriki katika kuwezesha shughuli za kilimo.
‘Benki hii imeundwa ili kutoa mikopo kwa masharti nafuu, pamoja na kutoa huduma nyinginezo zitakazoongeza uwezo wa wakulima kukopa na kuzalisha. Ili kufanikisha haya, benki inabidi iwe na vyanzo endelevu vya fedha za kutosha kwani nchi hii ni kubwa na wadau wa benki ni wengi sana. Lengo kuu ni kubadili kilimo cha Tanzania kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara’ alisema Bw. Samkyi.
Benki hii pia inatarajiwa kuwa ni kiungo muhimu cha utekelezaji wa mageuzi ya awamu ya pili ya sekta ya kifedha, na vile vile kuboresha maendeleo ya kilimo nchini ikizingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 pamoja na mipango mbalimbali ya maendeleo ya miaka mitano mitano, Mkakati wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo, na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA), pamoja na sera mbali mbali za Serikali zinazohusu sekta ya kilimo.