Rais Kikwete Awaaga Wananchi Wa Mtwara....Asema Mtwara ndio Muhimili Mpya wa Uchumi Tanzania Kwa Sasa - LEKULE

Breaking

10 Aug 2015

Rais Kikwete Awaaga Wananchi Wa Mtwara....Asema Mtwara ndio Muhimili Mpya wa Uchumi Tanzania Kwa Sasa


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amewataka wanasiasa mkoani Mtwara kuacha tabia za kuwapotosha wananchi kwa kuwaeleza mambo yasiyo na ukweli, na badala yake wawaeleze juu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa.

Akizungumza katika hotuba fupi aliyoitoa wakati wa kuweka jiwe la msingi katika jengo la Benki Kuu ya Tanzania (B.O.T) tawi la Mtwara, alisema Mtwara ndio muhimili mpya wa uchumi wa Tanzania kutokana na kuwa na rasilimali nyingi zinazotoa fursa za uwekezaji.

Kwa upande wake, Gavana wa B.O.T, Prof. Benno Ndulu, amesema Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya teknolojia ya huduma za simu za mkononi za kibenki zenye gharama nafuu na kufanikiwa kuwa katika nafasi ya 10 duniani kwa nchi zinazoongoza kwa teknolojia hiyo huku ikiwa nafasi ya kwanza barani Afrika.

Wakati huo huo rais Kikwete, amezindua kivuko cha Mv Mafanikio kinachosafirisha abiria kutoka Mtwara-Msangamkuu, chenye uwezo wa kubeba abiria 100 na magari sita kwa wakati mmoja.

Akiwahutubia wakazi wa kata ya Msangamkuu, Rais Kikwete amewaahidi wananchi wa kata hiyo kuwakamilishia mradi wa maji ambao unatekelezwa huku ukikabiliwa na uhaba wa fedha kiasi cha shilingi milioni 400.


Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais, waziri wa ujenzi na mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. John Magufuli, ameagiza wanafunzi wa ngazi zote kusafiri bure kwa kutumia kivuko hicho ambacho ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.5

No comments: