Baada kimya cha muda mrefu hatimaye Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilibrod Slaa, anatarajiwa kufungua pazia la kampeni za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Imeelezwa
kuwa, Dk. Slaa ambaye kwa sasa amepewa likizo na chama chake baada ya
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujiunga na chama hicho,
atafungua kampeni za Ukawa mkoani Dar es Salaam mwezi huu.
Kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu zitaanza rasmi Agosti 22, mwaka huu.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chadema, John
Mnyika, alidokeza kwamba Dk. Slaa atazindua kampeni za Ukawa katika
Jimbo la Kibamba, ambalo yeye (Mnyika) anagombea ubunge kwa tiketi ya
umoja huo.
Mnyika
alidokeza hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na viongozi wa matawi na
kata ya Goba, muda mfupi kabla ya kufanyika uchaguzi wa kura za maoni
kumchagua mgombea udiwani katika eneo hilo.
“Dk.
Slaa yupo mapumzikoni na jana nilizungumza naye kwa kirefu na
aliniambia bado anapumzika, lakini atakuja kushiriki kampeni Jimbo la
Kibamba ambalo mimi nagombea ubunge,” alisema Mnyika.
Hata
hivyo, Mnyika alipoulizwa kama Dk. Slaa atashiriki kampeni za nchi
nzima ama ataishia Jimbo la Kibamba pekee kama alivyozungumza naye,
Mnyika hakutaka kufafanua zaidi.
Katibu
huyo wa Chadema hajashiriki katika shughuli mbalimbali za Ukawa ikiwamo
kikao cha Ukawa cha kumkaribisha Lowassa kwenye makao makuu ya Chama
cha Wananchi (Cuf), mapokezi ya mwanasiasa huyo na mkutano mkuu wa
Chadema uliompitisha kugombea urais kupitia Ukawa.
Hata
jana Dk. Slaa hakuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Taifa la Cuf ambao
ulihudhuriwa na viongozi wote wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa vya
Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD.
Waliohudhuria
jana ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi.
Pia
walikuwapo wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Edward Lowassa na
Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad na mgombea mwenza, Juma
Haji Duni.
Akizungumza
katika mkutano mkuu wa Chadema wiki iliyopita, alinukuliwa na vyombo
vya habari akisema kuwa, Dk. Slaa kwa sasa yupo mapumzikoni, lakini
kampeni zitakapoanza ataongoza kampeni za Ukawa kuhakikisha wanaibuka
na ushindi kwa ngazi ya udiwani, ubunge na urais.
Mnyika
aliwaeleza wananchi wa kata hiyo kuwa Ukawa utashinda uchaguzi huu na
kwamba kinachotakiwa ni wao kujiandaa kufanya kampeni za nguvu ili
kuwafikia wananchi wengi.
Hata hivyo, Dk. Slaa alipotafutwa jana kuthibitisha maelezo ya Mnyika, simu yake ya mkononi haikupatikana.
Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms) hakujibu.
Habari
za Dk. Slaa kuzindua kampeni za Ukawa kama zitakuwa ni za kweli itakuwa
faraja kwa wafuasi na viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa.
Katika
hatua nyingine, Chadema imeelezea hofu ya kuwapo kwa waraka wenye
maagizo kwa vyombo vya dola ukitaka wakusanye vitambulisho vyao vya
kupigia kura kwa lengo linalohusishwa na hujuma za uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba 25, 2015.
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi eneo la Kimara Matangini
jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema wamepata taarifa kutoka kwenye
chanzo chao kuwa askari na maOfisa wengine wa vyombo vya dola, wamepewa
maagizo na wakubwa wao kukusanya vitambulisho vyao vya kupigia kura ili
namba zao zisajiliwe.
Alisema
Rais Jakaya Kikwete, kwa nafasi yake kama Amiri Jeshi Mkuu, anatakiwa
kuingilia kati suala hilo na pia kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
kujitokeza kukemea suala hilo.
Hata
hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, alipoulizwa alisema
habari hizo ni za uzushi na kwamba hakuna maagizo kama hayo.
No comments:
Post a Comment