Rais Kikwete atoa kauli kuhusu kupunguza gharama za kutuma pesa kwa kutumia simu - LEKULE

Breaking

14 Aug 2015

Rais Kikwete atoa kauli kuhusu kupunguza gharama za kutuma pesa kwa kutumia simu


RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali  imekusudia kupunguza gharama huduma za kutuma pesa katika mitandao ya simu kutoka nje ya nchi ili kuwawezesha Watanzania waishio ughaibuni (DIASPORA) kutumia fursa ya kijamii na kiuchumi zilizopo nchini ili kuliletea taifa maendeleo ya haraka.

Alisema utaratibu huo utawezesha Watanzania hao kumudu gharama za ununuzi na uendeshaji wa rasilimali mbalimbali nchini, hatua itayosaidia kukuza wigo wa sekta ya uwekezaji nchini.

Rais Kikwete aliyasema hayo alhamisi (Agosti 13, 2015) Jijini Dar es Salam katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Bernard Membe wakati wa ufunguzi wa kongamano lililohusisha Watanzania waishio Nje (Diaspora) na Taasisi binafsi na Umma katika kubaini mchango wa Viwanda vidogo na vya kati katika kuongeza wigo wa uwekezaji na ajira nchini.

“Kwa sasa tuna huduma za Tigo pesa, M-Pesa, Airtel Money na Easy Pesa katika mitandao yetu ya simu, hii ni hatua kubwa kimaendeleo, Watanzania waliopo nje wanaweza  kutuma kwa ndugu na jamaa kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali nchini” alisema Rais Kikwete.

Akifafanua zaidi Rais Kikwete alisema lengo la kongamano hilo ni kuwawezesha Watanzania hao kubaini fursa zilizopo nchini katika sekta za umma na binafsi na hivyo kusaidia kutengeneza wigo wa masoko katika mataifa wanayoishi.

Aidha Rais Kikwete aliwataka DIASPORA kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini ikiwemo ardhi, ambapo kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imeanzisha dawati maalum la kuwasaidia DIASPORA kupata viwanja vitakavyopangwa kuuzwa na Serikali katika sehemu mbalimbali nchini.

“Taifa letu limepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika Nyanja mbalimbali, nawaomba mtumie ujuzi na maarifa mliyonayo katika kuongeza zaidi maendeleo haya, kwa mfano hivi karibuni tulipokea madaktari Watanzania waishio nchini Marekani walioendesha huduma za matibabu katika hospitali za hapa nchini” alisema Rais Kikwete.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula alisema Watanzania waishio Ughaibuni ni rasilimali katika maendeleo ya nchi,  kwa kutambua umuhimu Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo uimarishaji wa mifumo ya biashara na uchumi.

Balozi Mulamula alisema Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Biashara kimeandaa kongamano hilo ili kuwawezesha Diaspora kwa kushirikiana na taasisi za uzalishaji mali nchini katika kukuza biashara ndogondogo na kati.

Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Filiberto Sebregondi alisema Umoja huo upo tayari kushirikiana kwa karibu zaidi na Tanzania katika jitihada za kukuza uchumi kupitia jumuiya za Watanzania waishio Ughaibuni (Diaspora).

Kongamano hilo linatarajia kumalizika siku ya Jumamosi tarehe 15 Agosti, 2015 limebeba kauli mbiu ya “mtu kwao,wekeza nyumbani”

No comments: