RAIS Jakaya Kikwete amesema ukiona Waziri anajisifia kafanya mambo kadhaa kwa uwezo wake, huyo ana matatizo ya ufahamu na ni mpenda sifa, kwa sababu mambo anayoyafanya anatekeleza majukumu aliyopewa na Rais na kwa mujibu wa muongozo aliopewa.
Alisema hayo jana wakati akiagwa jijini Dar es Salaam na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Ujenzi, huku akiongeza kuwa vuguvugu za kisiasa zinazoendelea, ni moto wa mabua ambao hauwaki ukadumu.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ambaye pia ndiye mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), angekuwa kama mawaziri hao, angejisifia kwa mafanikio yote yaliyopatikana katika Wizara alizoziongoza, ikiwemo Wizara hiyo ya Ujenzi.
Katika hotuba hiyo amesema sifa moja ya Dk Magufuli ni kutambua kuwa akiwa Waziri, anafanya kazi kwa niaba ya Rais kwa mujibu wa muongozo na rasilimali alizopewa, ambavyo vimeeleza nini anatakiwa kufanya kama waziri.
“Sijawahi kukusikia ukijisifia binafsi maana na wewe ungeweza kabisa kufanya hivyo kwa sababu barabara zote hizi ungeweza kusema ni mimi nimejenga na sio Rais… Sasa bila Rais kukuteua na kukupa muongozo na rasilimali ungepata nafasi ya kujenga hizo barabara?”Alihoji Rais Kikwete.
Alisema baadhi ya watu wamediriki kusema waliyoyafanya ni wao na sio Rais aliyewapa muongozo huo kufanya yoliyofanyika na kuongeza:
“Unadhani Rais atakuja kujenga nyumba? Amekwambia nimekupa hivi hapa na kila mtu niliyemteua nafanya hivyo na inatangazwa kwenye gazeti la Serikali.”
Rais Kikwete alisema Rais hana ushindani na Waziri wake na pia Waziri hana mashindano na Rais kwa sababu Waziri anafanya kazi kwa niaba yake maana ndiye aliyemteua.
Moto wa mabua
Alisema CCM imemteua Dk Magufuli kugombea nafasi ya Urais kupitia chama hicho na ana imani atapita salama kwa sababu ni mtendaji kazi mzuri na kwamba vurugu zinazoendelea za kisiasa ni moto wa mabua tu
. “Nina imani chama chetu kimekuteua kuwa mgombea wa urais kwa sababu ni mtendaji… Taifa litanufaika likipata kiongozi kama wewe, hao wengine ni moto wa mabua tu hauwaki ukadumu,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema ana imani Mungu akijalia Magufuli kuwa Rais basi yale mambo mazuri aliyoyafanya katika Wizara ya Ujenzi na sekta ulizopata kuongoza, atatumia maarifa na uzoefu huo kusukuma mbele gurudumu la taifa mbele.
Alisema Dk Magufuli kila wizara aliyopelekwa alifanya vizuri, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Miundombinu na Ardhi ambapo alisaidia kuondoa ujanja ujanja na kuimarisha nidhamu lakini hakuwahi kusema ni yeye binafsi ameleta manufaa hayo.
“Kuna wakati sehemu fulani ina matatizo watu wanasema jamani kwa nini msimlete Magufuli, tunasema hawezi kuwa kila mahali… Na sekta hii ya ujenzi ni sekta muhimu na kubwa, nashukuru chini ya uongozi wako tumeifikisha mahali pazuri,” alisema Rais Kikwete.
Aidha Rais Kikwete alisema anajivunia kuunganishwa kwa barabara zote za mikoa na Wilaya nchini katika kipindi cha uongozi wake na hiyo ni kwa jitihada na usimamizi uliofanywa na Waziri Dk Magufuli.
“Katika uongozi wangu tumefanikiwa kuunganisha karibu mikoa yote nchini kwa kiwango cha lami. Jambo hili limewezekana kwa ushirikiano na wafanyakazi wote pamoja na wataalam wa wizara hii ya ujenzi.”
Kikwete alisema alipoingia madarakani, bandari ya Dar es Salaam ilikuwa inasafirisha jumla ya tani milioni 6.7 za mizigo kwa mwaka, lakini hivi sasa bandari hiyo inasafirisha mizigo zaidi ya tani milioni 15 hadi mwishoni mwa mwaka huu, bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kusafirisha zaidi ya tani milioni 18, kitu ambacho kitaongeza ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa pato la taifa.
Aidha alisema kukamilika kwa barabara zote nchini kwa kiwango cha lami kutawezesha uchumi kukua kwa haraka zaidi na kuifanya nchi kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwa siku za usoni.
Rais Kikwete pia alisema katika kipindi chote cha uongozi wake ameweza kupambana na changamoto zilizokuwa zikiikabili wizara ya ujenzi na ndio maana mafanikio haya yamepatikana.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema mara baada ya kumaliza muda wake na kukabidhi madaraka kwa rais ajaye, ataondoka na kurejea kijijini kwao Msoga na kuendesha shughuli za kilimo, ikiwemo kilimo cha mananasi, mahindi na mazao mengine.
“Nikimaliza muda wangu wa uongozi na kukabidhi madaraka, nitarudi kijijini na kwenda kuendesha shughuli za kilimo, na wala sitaki nikiwa kule mnifuatefuate. Niacheni nikawe mkulima hodari,” alisema Kikwete.
Alisema sasa taifa linahitaji kiongozi bora zaidi yake ili aweze kuendeleza pale alipofikia yeye kwani likipata kiongozi dhaifu hata haya mafanikio yaliyopo yatarudi nyuma.
Kwa upande wake, Waziri Dk Magufuli alisema katika kipindi chote cha uongozi wake katika wizara ya ujenzi, ameweza kuyatekeleza vyema majukumu aliyopewa na rais kwa kushirikiana na wafanyakazi wenzake ndio maana wamepata mafanikio.
Alisema japokuwa wizara yake bado inakabiliwa na changamoto kadhaa, lakini imeweza kupambana nazo na kufanikisha ujenzi wa miundombinu yote muhimu iliyokuwa ikihitajika, Magufuli alisema anatumaini atakapokuwa Rais atatatua changamoto hizo zaidi kwa sababu anazifahamu vizuri.
Awali wakiwasilisha mafanikio yaliyofikiwa na taasisi zao zilizopo chini ya wizara ya ujenzi, watendaji wa taasisi hizo walisema awamu ya nne imeweza kufanya mambo mengi na ya kuingwa.
Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema barabara zenye urefu wa kilomita 5,568 zimejengwa kwa kiwango cha lami katika serikali ya awamu ya nne na kugharimu Sh trilioni 4.9.
Mfugale alisema barabara zinazoendelea kujengwa hadi hivi sasa zina urefu wa kilomita 3,875 ambazo pia zitagharimu Sh trilioni 4 na bilioni 535 na kwamba jumla ya barabara zenye urefu wa kilomita 8,600 zimejengwa kwa kiwango cha lami nchini nzima ambazo ni sawa na asilimia 86 na nyingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Imeandikwa na Regina Kumba na Emmanuel Ghula.
No comments:
Post a Comment