Waziri
Mkuu Mizengo Pinda, ambaye alianguka katika hatua za awali za mbio za
urais ndani ya CCM, amesema ameishia kuwa “rais wa fikra”.
Pinda,
ambaye amekuwa Waziri Mkuu kwa takriban miaka minane, hakuweza kuingia
katika orodha ya makada watano ambao majina yao yalipelekwa Halmashauri
Kuu kwa ajili ya kupata majina matatu ya kupelekwa Mkutano Mkuu kwa
ajili ya kupata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Baada
ya mchakato huo kumalizika, mbunge huyo wa Katavi amekuwa kimya, lakini
jana aliibuka na kuzungumzia mbio hizo zilizoacha majeraha kwenye chama
hicho kikongwe.
Pinda
alisema mchakato huo ulikuwa hauna kulala, wa haraka haraka, ambao
uliisha kwa CCM kupata mgombea ambaye alimuelezea kuwa “ni chaguo la
Mungu”.
Akizungumza
baada ya kupokea taarifa fupi ya Mkoa wa Mbeya kuhitimisha maonyesho ya
Nanenane jijini hapa, Pinda alisema alitamani sana kuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano Tanzania.
“Mimi
ninaamini Mungu ndiye anayepanga kwani sikuzaliwa kuwa Waziri Mkuu
wala kuwa Rais, lakini nilipangiwa uwaziri mkuu ambao nimefanya kazi
hiyo hadi nimechoka,” alisema Pinda, ambaye alikuwa mmoja wa makada 42 wa CCM waliojitokeza kuwania ridhaa ya chama hicho kugombea urais.
“Baada ya mchakato ule, alipatikana mtu mahiri ambaye Mungu alimpanga, lakini tamaa yangu, ikaishia kuwa rais wa fikra tu.”
Alisema mchakato ulifanyika kwa kasi bila kulala na wakapatikana watano, mara watatu na hatimaye mmoja.
“Suala hilo halitakiwi kuwa sababu ya kugombana, kulaumiana na kutoana macho, kwani ni sawa na kugombana na Mungu,” alisema Pinda.
“Hata
mimi nilitamani sana kuwa Rais, lakini sasa yamekwisha. Sina sababu ya
kuwa na hasira au kuhama chama kwani haina tija na hasira ni hasara.
“Sina
sababu ya kuhama chama, nitabaki CCM na baada ya Oktoba nitakuwa
mkulima mzuri ambaye nitashirikiana na wenzangu kuendeleza nchi.” Pinda
alisema mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ni mzuri na kwamba Mungu
atamsaidia kujua mahitaji mengine ya Taifa na Watanzania.
Alisema ana uhakika kwamba ifikapo mwaka 2025, hali ya umaskini katika kaya itakuwa imepungua.
Aliwataka
wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na maofisa wote wa Serikali waliogombea
urais, ubunge na udiwani ambao walishindwa katika kura mbalimbali,
wakubali matokeo na wachape kazi bila kinyongo na kwamba Serikali ijayo
itawafikiria kwa utendaji mzuri.
Awali,
katika taarifa yake fupi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema
yeye na viongozi wengine waliwania ubunge, lakini wameshindwa na
wataendelea kuchapa kazi ya Serikali.
Kandoro
alizungumzia utekelezaji wa maagizo mbalimbali aliyopewa na Waziri Mkuu
likiwamo la kuwashughulikia wanaume waliowapa mimba wanafunzi wa
sekondari na alisema watu 176 walikamatwa na 53 kati yao, kesi zipo
mahakamani wakati wengine walifungwa na wengine uchunguzi unaendelea.
Kuhusu
agizo la kuhakikisha wanawake wanapimwa ili kujua hali ya kansa mkoani
Mbeya, alisema wanawake 7,241 walipimwa na 200 kati yao walionekana
kuwa na saratani ya shingo kizazi.
No comments:
Post a Comment