Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amewataka wakazi wa jijini
hilo kuchukua hadhari za kiafya ikiwamo kuacha kusalimiana kwa kushikana
mikono kutokana na mlipuko wa kipindupindu ambao mpaka sasa
umeshawapata watu 56, kati yao watatu wamefariki dunia.
Akizungumza
jana ofisini kwake, mbali na kushikana mikono, Sadik aliwataka wananchi
kuacha kunywa maji ya viroba maarufu kama “maji ya Kandoro” na juisi za
mitaani ili kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa huo.
“Masuala
ya kusalimiana mikono kwa mikono katika kipindi hiki tuepukane nayo
lazima tunyanyapaliane wakati huu, ndiyo maana nilipoingia hapa
sikuwapeni mikono kwa sababu nazingatia masharti ya madaktari,”
aliwaambia waandishi wa habari.
Alisema
ugonjwa huo ulilipuka Agosti 15 baada ya mtu mmoja kufariki dunia
katika Hospitali ya Mwananyamala. “Hata familia yake, mke na watoto
walipochukuliwa vipimo na wao walidhihirika kwamba wana maambukizi ya
kipindupindu na mpaka sasa hivi bado tunao katika kituo chetu cha afya
pale Mburahati,” alisema Sadik.
Alisema
idadi ya wagonjwa imeongezeka hadi kufikia 56 lakini mpaka sasa
wamebaki wagonjwa 36 katika kituo maalumu kilichofunguliwa Mbagala baada
ya wengine kutibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Aliwataka
wananchi kuepuka kula chakula kilichopoa na matunda ambayo hayajaoshwa.
Alizitaja dalili za za ugonjwa huo kuwa ni kuharisha mfululizo, choo
kuwa cha majimaji meupe kama ya mchele, kutapika mfululizo, ngozi
kusinyaa, kiu kali, mdomo kukauka, mapigo ya moyo kuongezeka na mwili
kukosa nguvu.
No comments:
Post a Comment