Hatimaye Chama cha ACT – Wazalendo kimempitisha mwenyekiti wake, Anna Mghwira (56) kuwania urais baada ya mshauri wake, Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa amechukuliwa fomu kukataa kubeba jukumu hilo.
Sambamba na Mghwira, mkutano mkuu wa chama hicho uliokutana jana ulimpitisha Hamad Mussa Yusuf kuwa mgombea mwenza.
Chama
hicho kimefikia hatua hiyo baada ya kusota kwa siku kadhaa kutafuta
mgombea na pigo kubwa lilikuwa juzi baada ya Profesa Mkumbo kukataa.
Akisoma
maazimio ya Halmashauri Kuu katika mkutano mkuu jana usiku, mshauri wa
chama hicho, Profesa Mkumbo alisema wameamua kumpitisha Mghwira kwa kuwa
anazo sifa za kuwania urais.
Alisema
mwenyekiti huyo anao uwezo na sifa za kuwa rais, kwa kuwa kazi za rais
ambazo ni kufikiri, kuwa mlinzi mkuu wa umoja, tunu za Taifa na kuwa
mfano bora wa ubinadamu anazimudu.
Alisema
Mghwira anaweza kufikiri na amekuwa akiandika makala mbalimbali, jambo
ambalo baadhi ya wagombea hawaliwezi kwa kuwa hata hotuba wanaandikiwa.
Baada ya kumtangaza, wajumbe wa mkutano huo walishangilia kwa mbwembwe kumpata mgombea huyo.
Kwa
uteuzi huo, Mghwira atalazimika kuachia ule wa awali wa kuwania ubunge
katika Jimbo la Singida Mjini na atakuwa na kibarua ya kutafuta
wadhamini nchi nzima na kukamilisha kazi hiyo kabla ya kurejesha fomu
kwa muda aliopangiwa wa saa 7.30 mchana leo.
Akiwashukuru
wajumbe wa mkutano huo, Mghwira alisema Taifa linahitaji kiongozi
mwenye moyo wa nyama, mwenye upendo, uadilifu na mwenye uwezo wa
kuwaunganisha watu wote bila upendeleo.
Alisema
wamechelewa kumtangaza mgombea kwa kuwa walikuwa wanatafakari kauli ya
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya “Ikulu ni mahali patakatifu”, hivyo
wamempata rais mtakatifu.
Kiongozi
wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe alisema ilani ya uchaguzi ya chama
hicho imejikita katika mambo matano ambayo ni hifadhi ya jamii, elimu,
afya, ajira na utalii.
No comments:
Post a Comment