Dar es Salaam.
Kuongezeka kwa majeruhi wa ajali za bodaboda kumeifanya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), kuzidiwa na wagonjwa hadi kulazimika kuwalaza wengine sakafuni.
Kuongezeka kwa majeruhi wa ajali za bodaboda kumeifanya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), kuzidiwa na wagonjwa hadi kulazimika kuwalaza wengine sakafuni.
Ofisa Uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi alisema asilimia 53 ya majeruhi wote wanaopokewa na taasisi hiyo ni wa ajali za pikipiki.
Wajumbe
wa Kamati ya Usalama Barabarani, Kanda ya Dar es Salaam jana
walitembelea wodi namba 17 na 18 za Jengo la Sewahaji na Wodi namba
Mbili ya Jengo la Mwaisela na kujionea idadi kubwa ya majeruhi. Majeruhi
wengi waliolazwa Sewahaji ni vijana ambao baadhi yao wamekatika miguu,
mikono na wengine wakiwa na majeraha vichwani.
Mvungi
alisema kila siku taasisi hiyo inapokea majeruhi kati ya 20 na 26 na
kwamba wengi wao ni wa ajali za pikipiki. “Wodi za kulaza majeruhi
zimezidiwa tunalazimika wengine kuwalaza chini lakini wote wanapata
matibabu,” alisema.
Alisema Wodi Namba Mbili, ambayo ni
ya majeruhi wanawake, ina vitanda 33 lakini hadi jana ilikuwa na
wagonjwa 54 na kwamba waliozidi wanalala sakafuni.
Alisema
tatizo la wagonjwa kulala sakafuni liko katika wodi tatu zinazolaza
majeruhi... “Tatizo hilo litamalizika hivi karibuni mara baada ya
kumalizika kwa jengo la taasisi.” Katika wodi ya wanaume namba 17 na 18
ya Jengo la Sewahaji, mmoja wa majeruhi hao, Fikiri Omari (31)
aliyevunjika mguu wa kulia, alisema alipata ajali ya pikipiki tangu Juni
28 na kwamba mipango yake imeharibika.
Alisimulia
kwamba alipata na mkasa huo wakati akisubiri kuruhusiwa kwenye taa za
barabarani baada ya kugongwa na gari ambalo halikusimama.
“Nina
mke na watoto wanaonitegemea lakini miezi inazidi kupita nikiwa
hospitalini huku hali yangu ikiwa bado mbaya,” alisema. Mwenyekiti wa
Kamati ya Usalama Barabarani Kanda ya Dar es Salaam, Fadhili Mgonja
alisema: “Ninasikitika kuwaona vijana wadogo wakiwa wamekatwa viungo kwa
sababu ya ajali za barabarani.”
Alisema madereva, hasa
wa bodaboda, wanatakiwa kuwa makini wanapokuwa barabarani kwa sababu
wengi wao hawafuati sheria. “Madereva wa bodaboda hawafuati sheria na
hata askari wa usalama barabarani wakiwasimamisha hawasimami matokeo
yake ni ajali,” alisema.


No comments:
Post a Comment