Lowassa Awaonya Polisi.......Ampa Kibarua Kigumu Wenje - LEKULE

Breaking

17 Aug 2015

Lowassa Awaonya Polisi.......Ampa Kibarua Kigumu Wenje


Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema anawatakia kila la heri wanaobeza nguvu ya umma.

Kutokana na umati wa watu waliojitokeza jana kumlaki kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mwanza alikowasili saa saba mchana, iliuchukua zaidi ya saa mbili msafara wake kuingia Viwanja vya Furahisha saa tisa alasiri, ambako ni takriban kilomita nane.

Katika hotuba yake iliyochukua dakika 14 kuanzia saa 11.53 hadi 12.07 jioni, Lowassa alisema anawasikitikia wanaobeza nguvu hiyo ya umma.

“Haya siyo mapenzi, haya ni mahaba. Wanaobeza nguvu hii ya umma nawatakia kila la heri,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati huo.

Akizungumzia idadi hiyo ya wananchi, mke wa mgombea huyo, Regina Lowassa alisema haijawahi kutokea maeneo yote waliyotembelea Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.

“Mwanza nimewapenda, nafikiri baba (Lowassa) akitoka hapa atalala usingizi mzuri mzito,” alisema Regina.

Lowassa aliwataka polisi kutoingilia mchakato wa uchaguzi na kutumiwa na CCM kupambana na wapinzani na kwamba, wakiendelea watakuwa wanajitafutia tiketi ya kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mjini The Hegue.

“Nimesikitishwa sana kuwa watu wamepigwa mabomu asubuhi. Mkiendelea na mchezo huu tukimaliza uchaguzi tutawapeleka The Hague mkakipate cha mtoto na huko hamtarudi tena,” alisema.

Ampa Wenje kibarua
Lowassa alisema ziara yake hiyo inahusu kujitambulisha na asingependa kuwapa nafasi wapinzani wake kumtafsiri kuwa hajui sheria, lakini kero za Mwanza anazifahamu hivyo akaahidi kurejea na mikakati ya kuzitatua.

Alisema anafahamu Wamachinga, meli ya Mv Victoria, kiwanda kikubwa cha kusindika nyama, reli, ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege, bei ndogo ya pamba na tatizo la umeme.

Kuhusu suala la umeme, Lowassa alisema Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje ni kijana anayefanya uamuzi mgumu kama yeye hivyo alimtaka leo kwenda kwa Meneja wa Tanesco Mwanza ili kujua tatizo, asipopewa majibu ya kuridhisha ampigie simu yeye (Lowassa).

No comments: