Mmoja wa makada wa CCM aliyekuwa rafiki wa karibu na Edward Lowassa wakati wa mchakato wa urais ndani ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, ameibuka na kudai kuwa, hana kinyongo na yaliyotokea Dodoma huku akionesha kuwashangaa wanaoendelea kunung’unika, akisema watu wa aina hiyo hawakuwa pamoja na chama.
Aidha, Nchimbi, mmoja wa makada vijana waliokulia katika mfumo wa kisiasa ndani ya CCM alikoshika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkuu wa Wilaya, Mbunge na Waziri, amesema sasa si wakati wa kuendelea kuwa na makundi, bali kujenga umoja kwa lengo la kukipa chama ushindi.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM jijini Dar es Salaam.
Nchimbi ambaye tangu baada ya uteuzi wa mgombea wa urais wa CCM amekuwa kimya, ikiwa pamoja na kutojitokeza kuwania ubunge katika jimbo lake la Songea Mjini na hata kuhusishwa na mpango wa kukihama chama, amesisitiza hana kinyongo, bali anaunganisha nguvu zake na WanaCCM wengine kuhakikisha ushindi wa Dk John Magufuli, Waziri wa Ujenzi aliyepewa jukumu la kupeperusha bendera ya CCM katika urais.
Alisema ndani ya UVCCM, umoja huo umekubaliana kumaliza makundi na kwamba hivi sasa wapo kitu kimoja kwa ajili ya ushindi wa CCM.
Sadifa Amvaa Lowassa
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, Sadifa Juma Hamisi, ameendelea kutetea uamuzi wa CCM wa kutompitisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea urais kupitia chama hicho, akidai alipoteza sifa ya kuwa Rais tangu enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akifungua Baraza Kuu la UVCCM, Dar es Salaam juzi, Sadifa alisema makada wanaohama chama na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walipoteza sifa za uongozi tangu enzi za Mwalimu Nyerere.
Sadifa alisema Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Chadema, alipoteza sifa ya kuwa rais tangu enzi za Mwalimu Nyerere na kwamba dhamira yake hiyo haitafanikiwa milele.
Aliongeza kuwa, umoja huo haushtushwi na wimbi la wanasiasa maslahi wanaohama chama. Sadifa alisema vijana wa CCM wamejipanga kuueleza umma udhaifu wa wanasiasa hao.
“Hatutatishwa na watu wanaotumia fedha zao kusaka madaraka. Tumeamua kuvunja makundi yetu na tutaeleza uchafu wote…,” alisema Sadifa ambaye inaaminika alikuwa akimuunga mkono Lowassa kuwania urais ndani ya CCM.
Alisema umoja huo utashirikiana na chama, kuhakikisha Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli anapata ushindi mkubwa.
Alisema mwaka huu, umoja huo utawadhihirishia wote wanaodhani chama ni uso wa mtu wakisahau kuwa ni taasisi kwa kukipa ushindi wa kishindo kwenye nafasi zote za uongozi.
Alisema CCM imepata mgombea makini na kwamba hana dosari wala hakuna sababu ya kutafuta sabuni ya kumsafisha.
Sadifa alisema Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM aliendesha vikao vya Chama kwa umahiri mkubwa.
No comments:
Post a Comment