MWENYEKITI wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema chama hicho sio chama cha mchezo na kuvionya vyama vya upinzani kuwa watakiona cha mtema kuni katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Amesema
CCM itapata ushindi katika uchaguzi huo kwa kuwa imejipanga kwa hoja na
imeleta maendeleo nchini, huku akieleza kuwa wapo watu wenye tamaa ya
uongozi ambayo imekithiri.
Aliungwa
mkono na Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli aliyesema chama hicho
kitashinda na haoni wa kuwashinda, huku akiahidi kuwa atakuwa mtumishi
wa Watanzania kwani anazijua shida zao.
Rais
Kikwete aliyasema hayo jana katika Ofisi Ndogo za CCM, Mtaa wa Lumumba,
Dar es Salaam ambako alikuwapo kumpokea Dk Magufuli na Mgombea Mwenza
Samia Suluhu Hassan baada ya kutoka kuchukua fomu katika Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) katikati ya Jiji ili kuomba kuidhinishwa kuwa
wagombea.
“Sasa
kazi ndio imeanza rasmi. Dodoma zile zilikuwa rasharasha. CCM sio chama
cha mchezo. Watakiona cha mtema kuni. Kama ni mpira wa miguu, basi
tumefunga bao wakiwa wamesimama. Tumejiandaa vya kutosha na kushinda
tutashinda. Uzoefu, maarifa na uwezo wa kushinda tunao,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nawataka
wanaCCM kujipanga, msimdharau yeyote hata mpinzani akiwa mdogo
shughulikeni naye. Tumejipanga kwa hoja, tunazo hoja za kuzungumza. Nchi
tulivu na maendeleo yanaonekana na duniani kote wanajua kuwa Tanzania
inafanya vizuri. Tunao utawala bora, demokrasia na uhuru wa habari.
“Hata
duniani wanajua hilo na wanaona fahari kushirikiana na Tanzania. Lakini
wapo watakaokuwa na tamaa tu, duniani wapo watu wameumbwa hivyo,
wengine wanayo tamaa hadi imekithiri, imevuka mipaka,” alieleza Rais Kikwete mbele ya maelfu ya viongozi, wanachama na mashabiki wa chama hicho tawala.
Rais
Kikwete aliyefuatana na mkewe Mama Salma, alikatiza hotuba yake na
kuliomba kundi la Tanzania One Theatre (TOT) kuimba wimbo wa “Waache
waseme CCM ina wenyewe,” ambao alishiriki kucheza na mwisho wa wimbo
huo, alisema: “Ni ushindi wa uhakika, hauna hatihati. CCM shangilia ushindi unakuja.”
Kabla
ya kumkaribisha Dk Magufuli na Samia, Mwenyekiti huyo wa CCM alisema
uzinduzi wa kampeni za urais kwa chama hicho utafanyika Agosti 22, mwaka
huu na watatangaza wapi uzinduzi huo utafanyika kwani Viwanja vya
Jangwani kwa sasa havina fursa hiyo kwa kujengwa miradi ya mabasi ya
haraka na wafanyabiashara wadogo.
Alishuka
jukwaani saa saba kamili mchana baada ya kuwatambulisha wagombea hao
wawili, ambapo Samia kwa upande wake alisema haoni sababu ya CCM
kushindwa kutokana na jinsi kazi ya jana ya kwenda kuchukua fomu
ilivyokusanya maelfu ya wanachama, wapenzi na mashabiki wa chama hicho
tawala.
Lakini,
Dk Magufuli ambaye aliwasili Lumumba saa 4.47 asubuhi ili kwenda
kuchukua fomu hizo, alisisitiza kauli ya Rais Kikwete kuwa CCM itashinda
kwani chini ya uongozi wa rais huyo anayemaliza muda wake kikatiba,
mambo mengi mazuri yamefanywa ambayo yanawafanya watembee kifua mbele.
“Kujitokeza
kwenu kwa wingi leo ni ushahidi mwingine kuwa CCM itaendelea kutawala.
Niwathibitishie kuwa shida za Watanzania nazijua, mategemeo ya
Watanzania ninayo, na ipo misingi mizuri imewekwa chini ya Rais
Kikwete.
“Nawaahidi
nitakuwa mtumishi wenu sababu ninazijua shida za Watanzania. Watanzania
wana tatizo la ajira, hawataki kero za ovyo kama kukimbizana na mama
ntilie na bodaboda. Wanataka uchumi wao uwe mzuri, wanataka maisha
mazuri zaidi. Nitayasimamia, nawahakikishia sababu kero hizo nazijua,” alisema Dk Magufuli.
“Nimekuwa
mbunge kwa miaka ishirini na nimekuwa Waziri. Nimepata uzoefu kwa Rais
Kikwete, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Nyerere, na viongozi wengine.
Niko tayari kukipokea kijiti kwa mikono miwili. Nataka Mwenyekiti
kukuhakikishia kuwa tutashinda, sioni wa kutushinda,” alisema Dk
Magufuli huku akirudia maneno ya “sioni wa kutushinda” mara tatu.
Alisema
atakuwa mtumishi wa Watanzania wote bila kujali dini, kabila, itikadi
kwa sababu maendeleo ni ya wote, lakini akawataka wadumishe umoja na
amani, na kuwaahidi kuwa hatawaangusha.
No comments:
Post a Comment