Wakati Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akianguka katika matokeo ya marudio ya kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Meya wa Ilala Jerry Silaa aliyemaliza muda wake ameibuka kidedea.
Dkt Rashid alikuwa anatetea nafasi yake ya ubunge katika jimbo la Rufiji dhidi ya mpinzani wake mkubwa Mohamed Mchengelwa, huku Silaa akiomba ridhaa ya kuteuliwa na chama chake kuwania ubunge kwa mara ya kwanza katika jimbo la Ukonga.
Katibu wa CCM Wilaya ya Rufiji, Masililiyo Iriyo ameliambia Mwananchi Digital toka Ikwiriri mkoani Pwani kuwa Mohamed Mchengelwa amemshinda Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kwa kupata kura 6,002 sawa na asilimia 51.1 ya kura halali 11, 738.
Iriyo alisema Waziri wa Afya, Dkt Seif Rashid alipata kura 5,010 sawa na asilimia 42.7 ya kura halali.
Hata hivyo, taarifa toka Ikwiriri zinasema Dkt Rashid hakuwepo wakati matokeo yanatangazwa, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wakisema huenda alipima upepo na kubaini haukuwa unavuma vizuri kwa upande wake.
Jimboni Ukonga, aliyekuwa Meya wa Ilala, Jerry Silaa amembwaga tena mrufani na mpinzani wake wa karibu Ramesh Patel kwa kupata kura 10, 965 sawa na asilimia 57.1 ya kura zote 19, 187 zilizopigwa.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Ernest Charles ameiambia Mwananchi Digital kuwa Ramesh Patel ambaye amekubali kushindwa kwa kusaini fomu maalumu za chama hicho amepata kura 6, 960 sawa na asilimia 36.27.
Uchaguzi katika majimbo hayo umefanyika baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichoketi mjini Dodoma hivi karibuni kuagiza urudiwe katika majimbo matano yakiwemo Kilolo, Makete na Busega kutokana na dosari kadhaa.
No comments:
Post a Comment